Joe alikuwa
amechoka na kuishiwa na pumzi. Hata kazi
rahisi kabisa kama vile kutembea kuzunguka nyumba au kwenda kwenye gari,
ilimfanya apumue kwa shida. Alikaa
ofisini kwa daktari, akiwa amekata tamaa na kufadhaika. Alikuwa hajapunguza uzito tangu alipokuja
miezi miwili iliyopita. Kufanya mambo
yawe mabaya zaidi, alikuwa bado anavuta sigara, na kiwango cha sukari katika
damu yake kilikuwa kikubwa. Lakini
alikuwa bado hawezi kuacha kula donati zenye sukari ambazo alikuwa anazila kila
asubuhi, akishushia na kahawa yenye sukari au vinywaji vya kola. Kwa sababu ya kisukari chake namba 2, kuvuta
sigara, unene kupita kiasi, na maisha ya kukaa bila kazi za kutumia nguvu, Joe
alikuwa ameshikwa na ugonjwa wa moyo miaka miwili kabla, akiwa na miaka
35. Ulikuja kwa nguvu na kumwacha na
kovu kubwa katika msuli wa moyo wake na tatizo la kushindwa kwa moyo kufanya
kazi vizuri.
Akiwa na
haya kidogo, Joe alielezea wasiwasi wake kwa daktari wake. “Ndiyo Daktari, nilikuwa najua kuwa
hutafurahia kushindwa kwangu kupunguza uzito, na kwa kuwa bado ninavuta sigara
kidogo naomba unielewe, sivuti mpaka mapafuni!
Samahani daktari; sipendi kukuangusha.”
Daktari
alimtia moyo kwa upole ili azidi kujitahidi, alieleza kuwa kutokana na kasoro
ya kusukuma damu iliyotokana na ugonjwa wa moyo, kisukari kisichodhibitiwa, na
uvutaji wa sigara, pamoja na uzito wake uliopita kiasi, asipofanya mabadiliko
makubwa atakufa akiwa kijana.
Jibu la Joe
lilikuwa la ajabu, “Je daktari, inawezekana kubadilishwa moyo? Nimesikia huwa unabadilishwa. Je, ninaweza kupata moyo mwingine?”
“Laiti
ingekuwa rahisi na sahihi kiasi hicho,” daktari wake alisema. “Mioyo inayotolewa kwa ajili ya kubadilisha
ni adimu sana, na bado kuna kutumia dawa kwa miaka mingi baada ya hapo. Hiyo ni njia ya mwisho inayoweza kusaidia,
lakini inayowezekana kwa watu wachache tu.
Inakupasa kubadili mtindo wa maisha tena mara moja.” Hatimaye Joe alielewa hatari ya hali yake na
kuanza kubadili namna alivyokuwa anaishi.
Mamilioni ya
watu huwa wanahangaika na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ulimwenguni kote kama
Joe: Magonjwa ya moyo, saratani,
magonjwa ya njia ya hewa, na kisukari.
Yote haya yanasababishwa na mambo makuu manne:- Matumizi ya tumbaku, kutoshughulisha mwili,
pombe na vyakula visivyofaa. Unaweza kuwa
hatarini bila kujua.
No comments:
Post a Comment