Licha ya umuhimu wake, yasipotunzwa vizuri, masikio huweza
kupata maambukizi yatokanayo na fangasi au bakteria. Mara nyingi maambukizi ya fangasi
hufananishwa na yanayosababishwa na bakteria.
Leo tunaangalia maambukizi ya fangasi sikioni ambayo mara nyingi
hutokea nje ya sikio. Hutokana na
maambukizi ya fangasi. Vimelea vya
fangasi vinavyosababisha maradhi haya kwa watu wengi huwa vinatoka kwenye jamii
mbili ambazo ni aspergillus na candida.
Huweza pia kutoka kwenye jamii nyingine na fangasi kama vile
actinomyces, phycomycetes na rhizopus. Jamii
zote hizi hupatikana kwenye mazingira yaliyotuzunguka lakini kwa wengi huwa
hawana madhara kwa sababu kinga ya kawaida ya mwili huwa na uwezo wa
kukabiliana nao na kuwazuia wasilete tatizo lolote.
Fangasi hawa huweza kuleta madhara kwenye masikio pale
inapotokea kinga ya mwili imeshindwa kuwazuia wasifanye hivyo. Mara nyingi maradhi haya hutibiwa kama
yamesababishwa na vimelea aina ya bakteria kwa mgonjwa kupewa dawa aina ya
antibiotiki ambazo hazina uwezo wa kukabiliana na vimelea aina ya fangasi. Matibabu sahihi hutolewa baada ya dawa za
antibaiotiki kushindwa kutibu tatizo.
Walio hatarini
Ingawa kila mmoja anaweza kuugua fangasi wa sikio, kuna
walio kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya. Wanaooga au kuogelea kwenye maji yasiyo safi
yaani maji machafu wanajiweka kwenye kundi hili. Yanaweza kuwa maji ya bwawa la kuogelea ambayo
hayatibiwi au kubadilishwa siku nyingi au yaliyotuhama. Ikiwezekana, inashauriwa kuyaepuka.
Wengine ni wanaotumia dawa kutibu maradhi mbalimbali kwa
muda mrefu. Hii ni kwa sababu matumizi
ya dawa kwa muda mrefu hushusha kinga za mwili hivyo kuufanya mwili usiweze
kukabiliana na maradhi yatakayojitokeza.
Watoto wadogo wapo katika hatari zaidi ya kupata maradhi
haya kutokana na kutokua na kinga imara pamoja na kujihusisha kwao na michezo
ambayo inawaweka kwenye mazingira yenye vimelea vingi vya maradhi haya.
Watu wenye umri mkubwa au wenye maradhi ya muda mrefu kama
vile kisukari ambayo hushusha kinga ya mwili nao wapo kwenye hatari ya kupata
maambukizi ya fangasi wa sikio.
Dalili
Maumivu ya sikio hasa linapoguswa, muwasho wa kuvimba ni
miongoni mwa dalili za fangasi hawa. Baadhi
ya wagonjwa hutoa usaha mweupe au wenye rangi ya manjano sikioni.
Baadhi ya wahusika hushindwa kusikia vizuri kwenye sikio
lenye tatizo, kama lililopata maambukizi ni moja, wengine hupata hisia kama
kuna kitu kimekaa sikioni na wapo ambao sikio au masikio huziba.
Endapo mgonjwa atahisi moja ya dalili hizi inashauriwa aende
hospitali kuonana na daktari ambaye atamfanyia vipimo maalum vya maabara.
Baada ya kujiridhisha kuwa ugonjwa unatokana na maambukizi
ya fangasi daktari atatoa matibabu yanayostahili.
Matibabu
Kwanza kabisa ni vyema kusafisha sikio na kuondoa usaha au
chochote kilichoko kwenye sikio. Hii husaidia
kuondoa baadhi ya fangasi waliosababisha tatizo.
Utaratibu wa kusafisha sikio lililoathirika unatakiwa
urudiwe mpaka pale atakapopona. Usafishaji
huu hufanywa kwa kutumia dawa ya hydrogen peroxide ambayo huondoa uchafu
uliojishikiza kwenye kuta za mfereji wa sikio.
Kama maradhi yamesababisha ngoma ya sikio kuchanika basi ni
vyema usafishaji huu ukafanywa na daktari bingwa wa masikio, koo na pua.
Zaidi ya kusafisha masikio yaliyoathirika, daktari atatoa
dawa aina fangasi (antifungal agents) ambazo zina uwezo wa kukabiliana na
fangasi. Kumbuka dawa za antibaiotiki
(antibiotics) hazina uwezo wa kukabiliana na vimelea vya fangasi.
Dawa zinazotolewa huwa ni za matone ambayo mgonjwa ataweka
kwenye masikio yake kwa kufuata maelekezo ya daktari. Haishauriwi kutoa dawa za kunywa kwa lengo la
kutibu maradhi haya. Kama mgonjwa ni mtu
mzima na kuna hatari ya maradhi kusambaa huwa inashauriwa kutibiwa kwa dawa za
kunywa au zile zinazowekwa kwenye mishipa.
Hii ina lengo la kuzuia uwezekano wa vimelea vya fangasi
kusambaa mpaka ndani ya sikio na mfupa wa fuvu na kusababisha madhara makubwa Zaidi.
Kwa walio mbali na hospitali na ambao wanashindwa kwenda
hospitali kuna namna nyingine za kutibu maradhi haya. Wanaweza kuhakikisha wanakausha sikio muda
wote ili kuwanyima fangasi nafasi ya kushamiri kwani hufanya hivyo maeneo yenye
joto na majimaji.
Kama utaweza kuhakikisha sikio ni kavu muda wote utasaidia
kuzuia fangasi wasiongezeke. Jambo la
tahadhari ni kutoingiza chochote sikioni kwani unaweza kukausha eneo la nje tu
la sikio.
Ukiingiza kijiti cha kuondoloea nta ya sikio utasaidia
kuvisukuma ndani zaidi vimelea vya maradhi na kuhatarisha afya ya ngoma ya
sikio.
Unaweza kuweka siki vilevile. Vimelea vya fangasi hushindwa kushamiri na
kuongezeka kwenye mazingira yenye tindikali.
Siki (vinegar) ina tindikali hivyo ukiiweka kwenye sikio basi huondoa
mazingira rafiki kwao.
Habari!
ReplyDeleteAsante kwa somo lako.Mimi naomba kujua hii wiki uliyosena ni siki ya aina yoyote,au kuna wiki maalum.Kuna siki inaitwa simba,nyeupe inatengenezwa hapa Tanzania inafaa hata hiyo?
Habari!
ReplyDeleteAsante kwa somo lako.Mimi naomba kujua hii wiki uliyosena ni siki ya aina yoyote,au kuna wiki maalum.Kuna siki inaitwa simba,nyeupe inatengenezwa hapa Tanzania inafaa hata hiyo?