Sehemu kubwa ya mbogamboga (vegetables) inachukuliwa na maji
kwa asilimia 84-96. Kwa upande wa
virutubisho vingine, mbogamboga ni chanzo kizuri cha madini ya Phosphorus na
Calcium. Vilevile ni chanzo kizuri cha
Vitamin A na C.
Vitamin C inapatikana zaidi kwenye mbogamboga za majani
ambazo zina rangi ya kijani, kama vile mchicha, kisamvu, matembele, majani ya
kunde na yale ya maboga na kadhalika.
Kwa upande wa vitamin A inapatikana kwa wingi kwenye karoti.
Zaidi ya hayo, baadhi ya mbogamboga zina protini na
kabohaidreti (wanga) kwa mapeyasi, maharage na viazi.
Nyuzi nyuzi za kilishe (dietary
fibres) pia zinapatikana kwa wingi hasa katika mbogamboga za majani.
Vitamin C ni kirutubisho kinachopotea kwa haraka wakati wa
upikaji wa mbogamboga. Ili kupunguza
tatizo hilo, mbogamboga zipikwe kwa dakika chache, kama tano mpaka kumi. Kwa utaratibu huu, maji yachemshwe
kwanza. Yaani osha mboga zako vizuri kwa
maji safi halafu zitie katika maji yaliyochemka. Baada ya dakika hizo tano mpaka kumi zitakuwa
zimeiva kwa kiasi ambacho hakitapoteza vitamin C kwa wingi.
Sambamba na hatua hiyo, mbogamboga lazima zipikwe kwenye
chombo kilichofunikwa ili vitamin zisiondoke na mvuke. Pia, watu wajilazimishe kunywa ule mchuzi
(supu) unaopatikana baada ya kupika hizo mbogamboga. Hii ni kwa sababu, mchuzi huo una vitamin
nyingi inayotoka kwenye mbogamboga.
Vitamin na madini ni muhimu sana mwilini. Kwa sababu zinasaidia kuupa mwili kinga ya
maradhi mbalimbali na madini kama ya chuma, yanahitajika kwa utengenezaji wa
damu. Bila damu hakuna binadamu
atakayeweza kuishi.
Nyuzinyuzi za kilishe nazo ni muhimu ili chakula kiweze
kusagwa vizuri tumboni. Pia, zinasaidia kunyonya
sumu iliyoko tumboni ambayo inaweza kusababisha ugonjwa wa saratani
(kansa). Nyuzinyuzi hizo zinasaidia mtu
kupata choo kikubwa mara kwa mara. Yaani
huondoa tatizo la kutopata choo.
No comments:
Post a Comment