Thursday, November 24, 2016

KULA EMBE NA MAGANDA YAKE KWA AFYA ZAIDI

embe na maganda yake

Embe ni miongoni mwa mazao yanayolimwa kwenye mikoa karibu kutokana na uwezo wake wa kustawi katika udongo wa aina mbalimbali na kustahimili aina tofauti ya hali ya hewa.

Kutokana na ladha tamu na wingi wa virutubisho, embe inajulikana kama mfalme wa matunda duniani.  Linapatikana maeneo mengi na kuliwa na watu kada zote kwa namna tofauti kulingana na maandalizi yake.

Kuna njia kuu tatu za ulaji wa matunda ya embe kwa ngazi ya familia.  Njia ya kwanza ni kuondoa ganda la nje au kumenya na kuitumia kutengeneza juisi.


Juisi nyingine au matunda mengine na mboga mboga ni kinywaji na chakula kizuri sana kwa wagonjwa hasa wasioweza kutafuna chakula vizuri na wale ambao matumbo yao hayawezi kusaga chakula kwa urahisi.

Juisi inaongeza maji mwilini na kumsaidia mgonjwa kukojoa mara nyingi zaidi hivyo kusafisha damu na kuondoa sumu mwilini kila afanyavyo hivyo.  Hata hivyo, juisi hupoteza nyuzilishe (dietary fibers) wakati wa kuichuja.

Njia ya pili ni kula embe lililomenywa.  Yaani unaondoa maganda na kuikata vipande na kula nyama yake.  Ulaji wa namna hii unatumiwa na watu wengi.  Hata hivyo, virutubisho vingi vinavyopatikana kwenye maganda ya embe kama vile nyuzilishe, madini, vitamini na “phytochemicals” vinapotea wakati wa umenyaji.

Njia ya tatu, ni kula embe na maganda yake.  Ulaji wa aina hii ni mzuri hasa kwa watu ambao sio wagonjwa.  Ulaji huu unaupa mwili virutubisho vingi zaidi vilivyomo kwenye nyama na maganda ya embe husika.  Hata hivyo, kabla ya kula lazima embe lioshwe vizuri na lisuuzwe kwa maji safi na salama; yaliyochemshwa au ya chupa.  Baada ya hapo ndipo liliwe na maganda yake.

Kama embe halitaoshwa vizuri, mlaji anaweza kupata maambukizi ya magonjwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, kuhara na minyoo.  Kwa yale yanayopuliziwa dawa za kuua wadudu, yakiliwa bila ya kuoshwa vizuri dawa hizo zinaweza kudhuru afya ya walaji.

Maganda ya embe ni chanzo kizuri cha virutubisho vya phytochemicals ambavyo ni kemikali zenye manufaa mwilini kama vile anthocyanins, carotenoids na polyphenol.

Kemikali hizi zinajulikana kama antioxidants zina nguvu kubwa ya kuufanya mwili usizeeke mapema na usipate magonjwa mfano kisukari na saratani.

Vilevile, maganda ya embe yana virutubsho vya nyuzilishe kwa wingi ambazo zinaondoa kukosa choo kubwa, zinasaidia kukabiliana na magonjwa ya moyo na saratani ya utumbo mpana, zinapunguza wingi wa sukari kwenye damu na mafuta mwilini.

Zaidi ya hayo, embe ina vitamin A, C, E na madini ya selenium.  Virutubisho hivi vinaimarisha afya ya macho ni kinga kwa magonjwa ya moyo na saratani za aina mbalimbali ikiwemo tezi dume.

Embe ina vimeng’enyo (enzymes) ambavyo husaidia mmeng’enyo wa chakula hivyo kuwafaa zaidi wenye tatizo la tumbo kushindwa kusaga chakula vizuri.

Embe pia, lina sukari ya asili, mafuta kidogo, madini ya chuma, shaba, potassium na calcium.  Vilevile embe lina vitamin B-6, na folate ambazo ni muhimu kwa afya ya kila mmoja wetu. 
Share:

No comments:

Post a Comment