Monday, February 19, 2018

KILA RIKA HUPATA UTAPIAMLO


Utapiamlo ni hali ambayo hutokana na kupata chakula ambacho virutubishi vyake havitoshi au viko vingi hadi kusababisha matatizo ya kiafya.

Neno hili hutumika mara kwa mara hasa kurejelea hasa ukosefu wa lishe ambapo hakuna kalori, protini au lishe ya kutosha hata hivyo, hujumuisha pia kupata lishe kupita kiasi (yaani obesity).

Utafiti uliofanyika umeonesha kwamba kulikuwa na watu milioni 925 waliokuwa na utapiamlo duniani miaka saba iliyopita (2010), ongezeko la milioni 80 tangu 1990.

Watu wengine bilioni moja wanakadiriwa kukosa vitamin na madini.  Katika mwaka 2010 utapiamlo wa protini (kwashiorkor) inayoleta nguvu ulikadiriwa kuwa kusababisha vifo 600,000, vilivyo chini kutoka vifo 883,000 katika mwaka wa 1990.

Ukosefu mwingine wa lishe, ambao unaweza kujumuisha ukosefu wa aidini na anemia kutokana na ukosefu wa madini ya aidini na chuma, ulisababisha vifo vingine 84,000.

Ukosefu wa lishe hadi mwaka wa 2010 ulikuwa sababu kwa asilimia 1.4 ya miaka ya maisha kubadilika kwa sababu ya ulemavu.

Takribani theluthi moja ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano huaminika kutokana na utapiamlo.  Katika mwaka wa 2010 ilikadiriwa kwamba ilichangia takribani vifo  milioni 1.5 kwa wanawake na watoto, ijapokuwa baadhi ya makadirio ya idadi hiyo huenda yanatakiwa kuwa zaidi ya milioni 3.

Watoto wengine milioni 165 wana matatizo ya kukua kutokana na ugonjwa huu (stanted growth).  Tatizo la ukosefu wa lishe ni wa kawaida sana katika nchi zinazoendelea sababu kuu zikiwa umasikini na ukosefu wa elimu lishe, ikiwamo Tanzania.

Aina za lishe

Aina ya kwanza ni ukosefu wa lishe ya protini inayojega mwili (kwashiorkor) na hutambulika kwa dalili kama za kubadilika kwa rangi ya ngozi na nywele (rangi ya kutu), uchovu wa mara kwa mara, kuharisha, kushindwa kukua au kuongeza uzito, kuvimba kwa kisigino, miguu (yaani edema) na tumbo (ascites) pia kinga dhidi ya magonjwa kushuka.

Vyanzo vya protini ni kama maharage, mayai, maziwa, nyama, samaki pia protini ya kwenye mboga za majani kama vile kabeji, spinachi, uyoga salama na matango.

Aina ya pili ni ukosefu chakula cha kutosha kwa ujumla (marasmus) huambatana na uso mwembamba, mbavu na mabega kuonekana kwa urahisi kwa sababu ya kukonda, kuharisha, ukosefu wa maji mara kwa mara, kuharisha, macho kuingia ndani na ngozi kuwa laini kupita kiasi.

Ukosefu wa kawaida wa lishe ni pamoja na madini, aidini inayopatikana kwenye chumvi na vitamin A kama vile karoti, parachichi, viazi vitamu, samaki, papai na mboga za majani kama vile mchicha.  Wakati wa ujauzito, kwa sababu ya hitaji kuongezeka kwa kiasi kikubwa, ukosefu huo hutokea kwa asilimia kubwa.

Katika baadhi ya nchi zinazoendelea lishe kupita kiasi kwa njia ya unene (obesity) imeanza kutokea katika jamii sawa kama za walio na upungufu wa lishe.

Sababu nyingine za utapiamlo hujumuisha anorexia nervosa (hali ya kukataa kula kwa lengo la kupunguza uzito) na bariatric surgery (kupunguza uzito kwa kupunguza saizi ya tumbo kwa njia ya upasuaji).

Kwa wazee utapiamlo hutokea zaidi kwa sababu ya mambo ya kimwili, kisaikolojia pia kijamii.

Chanzo

Kwa njia ya chakula mwili unapokea virutubishi vya lazima kama vile kalori, protini, mafuta, wanga (kabohidrati), vitamin na madini.  Hivyo uhaba au wingi wa vitu hivi kwa muda fulani unasababisha utapiamlo.

Hivyo, kuna aina mbili za utapiamlo: kukosa kiwango cha kutosha cha chakula na kukosa uwiano wa virutubishi katika chakula (hasa ule wa protini).

Utapiamlo hutokea kama mtu hana chakula cha kutosha, yaani uhaba wa chakula kwa ujumla na kuwa na hali ya njaa ya kudumu (marasmus).

Hutokea kama mtu anakosa sehemu muhimu za vyakula kwa mfano protini, vitamin au minerali hata kama vinginevyo anakula chakula kingi na pia hutokea kama mtu anazoea kushiba vyakula bila kujali uwiano wa virutubishi ndani ya chakula (obesity).

Kukosa lishe ya kutosha hutokana na kukosa chakula kizuri cha kutosha.  Hii hutokana na bei ya juu ya chakula na umaskini.

Kukosa kunyonya maziwa ya matiti mapema kwa kutosha kunaweza kuchangia, pia maradhi ya kuambukiza kama vile homa ya matumbo, nimonia, malaria na ukambi ambao huongeza mahitaji ya lishe.

Ikiwa ukosefu wa lishe utatokea wakati wa ujauzito au kabla ya umri wa miaka miwili huenda ukasababisha matatizo ya kudumu katika ukuaji wa mwili ikiwemo na akili.

Ukosefu mkali wa lishe, unaojulikana kama kukosa chakula (marasmus), unaweza kuwa na dalili ambazo zinajumuisha kimo cha chini; wembamba, viwango vya chini sana vya nguvu, na miguu na tumbo kuvimba.

Watu hawa huumwa na kuwa baridi mara kwa mara.  Dalili za ukosefu wa lishe hutegemea hasa lishe ambayo inasemekana.

Tiba

Juhudi za kuboresha lishe ni kati ya njia nzuri zaidi za kusaidia kukua hasa upande wa watoto.  Kunyonyesha kunaweza kupunguza viwango vya utapiamlo na vifo katika watoto, na juhudi za kukuza tabia hii hupunguza viwango vya utapiamlo hasa kwa watoto.

Katika watoto wadogo kuwapa chakula kwa kuongezea maziwa ya matiti kati ya miezi sita na miaka miwili huboresha matokeo.

Kuna pia ushahidi mzuri unaounga mkono virutubishi vya lishe kadhaa wakati wa ujauzito na kati ya watoto wadogo katika nchi zinazoendelea.  Njia zinazofaa ni kuwapa chakula watu wanachokihitaji sana, kuwasilisha chakula na kutoa pesa ili watu waweze kununua chakula katika masoko yao.

Kwa wale ambao wana utapiamlo mkali unaosababishwa na matatizo mengine ya afya wanapendekezwa kupata matibabu hospitalini.  Mara kwa mara hii huhusisha kudhibiti kiwango cha chini cha sukari kwenye damu, halijoto ya mwili, ukosefu wa maji, na kupata lishe polepole.

Viuavijisumu vya mara kwa mara vinapendekezwa kwa sababu ya hatari ya juu ya maabukizo.

Hatua za muda mrefu zinajumuisha kuboresha kilimo, kupunguza ufukara, kuondoa uchafu katika mazingira, na kuwawezesha wanawake hasa kielimu juu ya suala hili la lishe.
Share:

CHANZO CHA HARUFU MBAYA MDOMONIKatika maisha ya kila siku yawezekana umewahi kukutana na mtu ambaye ukiwa karibu naye akiongea au kutoa pumzi kinywani au puani utasikia harufu mbaya.

Kwa kawaida mdomo na pua huweza kutoa pumzi nje ambayo huwa na harufu asilia ambayo haiwezi kumkera mtu mwingine, lakini mara zingine hali hiyo inaweza kujitokeza kutoa pumzi yenye harufu mbaya.

Watu wa karibu au wanaokutana na mwathirika wa hali hii wanaweza wakadhani kuwa ni mchafu mwenye tabia ya kutopiga mswaki au kutosafisha kinywa chake vizuri.

Pasipo kujua kuwa upo uwezekano mtu huyo akawa na tatizo linalojulikana kitabibu kama Halitosis,maana yake ni kutoa pumzi aidha kwa mdomoni au puani yenye harufu mbaya isiyo vumilika.

Mtu mwenye tatizo hili anaweza kukumbana na kunyanyapaliwa na wanajamii wanaomzunguka kiasi cha kuweza kumsababishia matatizo ya kisaikolojia.

Muathirika anaweza kupatwa na tatizo la woga/hofu iliyopitiliza anapokuwa kwenye kundi la watu, anaweza akajiondoa kutoka katika kundi hilo na kujitenga na vilevile, baadaye huweza kupata sonona (depression).

Tatizo hili linalowakumba asilimia 20 ya wajamii duniani, ni moja ya tatizo linalowafanya kufika katika huduma za afya kuwaona madaktari wa kinywa na meno.

Hufika kwa wataalam hawa wakidhani wana magonjwa ya kinywa ikiwamo mashimo katika meno, kulika kwa meno, kuoza kwa meno na magonjwa ya fizi.

Si wagonjwa wote wenye kutoa pumzi yenye harufu mbaya wana tatizo halisi la halitosis, kati ya asilimia 5 hadi 72 wanaofika katika huduma za afya hugundulika kuwa hawana tatizo hilo moja kwa moja.

Tatizo la kutoa pumzi yenye harudu mbaya ambalo ndiyo halitosis halisi huwa linasababishwa na uwapo wa mrundikano wa bakteria katika uvungu wa mafizi na nyuma ya ulimi jirani karibu na koo.

Kinywa kwa ujumla, ikiwamo meno, fizi, ulimi na vifuko vya mate yanaweza kuwa ni maficho mazuri kwa mamia ya bakteria.

Ndio maana inaaminika tatizo la harufu mbaya mdomoni ni kinywa chenyewe.

Kinywani pekee kuna karibu jamii 600 za bakteria ambao huambatana na mabaki ya vyakula tunavyokula kila siku.  Uwapo na protini ya kwenye mate na protini ya vyakula tunavyokula, uvunjwaji wa mabaki yake na bakteria waliopo mdomoni ni chanzo cha kuwapo kwa harufu mbaya.

Mabaki ya protini mdomoni ambayo huvunjwavunjwa na bakteria na kuwa tindikali ya amino na hapo baadaye inapovunjwa, hutoa gesi yenye harufu mbaya.

Mfano mzuri ni pale protini ijulikanayo kama methionine na cysteine inapovunjwa vunjwa kinywani huweza kutoa gesi yenye harufu mbaya ijulikanayo kama hydrogen sulphide.

Mara nyingi harufu ya kinywa inaweza kuwa nzito Zaidi baada ya kuamka ni kwa sababu wakati wa kulala mdomoni kunakuwa na kiasi kidogo cha hewa ya oksijeni.

Bakteria waliopo mdomoni ni wale wasiohitaji hewa ya oksijeni, hivyo kipindi cha usiku tuiwa tumelala ndipo huvunjavunja mabaki ya chakula ambayo huambatana na kutolewa gesi zenye harufu mbaya.

Vilevile, harufu ya kinywa inaweza kubadilika kutokana na vyakula tunavyokula vikiwamo vitunguu maji, vitunguu swaumu, iliki, tangawizi na pia uvutaji sigara na unywaji wa pombe.

Hivyo si mara zote kupumua harufu isiyo ya kawaida, bali mara nyingine inakuwa tatizo la muda tu lililochangiwa na vyakula na matumizi mengine ya vitu.

Kwa asilimia 10 zilizobaki mara nyingi husababishwa na matatizo mengine ikiwamo magonjwa ya kooni, puani, shambulizi za nyufa za mifupa iliyopo usoni, magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa katika mapafu, magonjwa ya masikioni na madhara ya ugonjwa sugu wa mafindofindo (tonsillitis).

Pia, uwapo wa majipu ya fizi/meno, vidonda mdomoni au michubuko, vidonda vya kooni, huambukiza virusi vya herpes simplex na HPV.  Mara chache pia tatizo hili linaweza kuchangiwa na magonjwa ya ini ikiwamo kuharibika kwa ini na majipu katika ini.

Mara nyingine wanaolalamika tatizo hili hubainika kuwa ni tatizo la usafi wa kinywa.  Na wanaposhauriwa kuboresha usafi wa kinywa kwa kutumia dawa za meno, au kusukutua na dawa maalum za kusafisha kinywa nyuma ya ulimi, tatizo huweza kuisha haraka.

Inapotokea tatizo hilo chanzo chake sio mdomoni, ni vigumu kuweka bainisho sahihi na vilevile hata kutibika kwake inakuwa vigumu.

Uchunguzi wa tatizo hili huanzia kwa mhusika mwenye we kwa kueleza historia ya tatizo kisha wataalam wa kinywa au daktari wa kawaida humchunguza kwa kumfanyia majaribio na vipimo kadhaa.

Baada ya wataalam wa afya kujua bainisho la ugonjwa ndipo ushauri na matibabu huanza.  Kama chanzo cha harufu mbaya ni maradhi ambayo si ya kinywani, wataalam wa afya watakupa matibabu ya kutibu chanzo hicho.

Kama chanzo cha kutoa pumzi yenye harufu mabya ni kinywa, wahudumu wa afya watamuelekeza mgonjwa mambo mbalimbali kama ifuatavyo;

Kuhakikisha kupiga mswaki katika ulimi mara mbili kwa siku kwa kutumia mswaki laini, kifaa kama kijiko kwa ajili ya kukwangua uso wa ulimi, vilevile kutumia dawa yenye kiambata cha kuua bakteria.

Ulaji wa kifungua kinywa chenye afya ikiwamo kula matunda na mboga za majani yenye nyuzi nyuzi husaidia kusafisha kinywa eneo la nyuma ya ulimi wakati wa kumezwa.

Utafunaji wa bazooka unasaidia kuufanya mdomo usiwe mkavu na hewa ya oksijeni kuingia kinywani kwa wingi, vilevile utafunaji wa bazooka huweza kusaidia kutiririka kwa mate kwa wingi yanayosaidia kusafisha kinywa na kuua vimelea vya maradhi.

Mdomo ukiwa mkavu na hautafuni chochote huchangia kujiimarisha kwa bakteria wasihitaji hewa ya oksijeni.

Sukutua kwa maji mengi ikiwezekana ya uvuguvugu kila mara baada ya kula chakula, na kabla ya kwenda kulala.  Unaweza pia kutumia dawa maalum za kusukutulia kinywa zenye dawa ya kuulia vimelea.

Jaribu kuboresha usafi wa kinywa kwa kuusafisha ulimi, safisha meno kwa mswaki kila unapomaliza kula chakula, ondoa mabaki ya chakula yaliyojibana katika meno na fizi na safisha na sukutua kinywa chako kwa dawa maalum kabla ya kulala.

Unaweza kutumia vitu asilia vikiwamo majani ya miti na karafuu kama njia ya kupunguza kupumua hewa yenye harufu mbaya.

Vizuri kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa mara kwa mara angalau kwa miezi sita mara moja ili kuweza kubaini magonjwa mbalimbali ya kinywa mapema.

Share:

HAYA NI MATATIZO YA KUTOPATA HEDHI


Ni Dhahiri kuwa kukosa au kutopata kabisa hedhi ni tatizo linalowapata wanawake wengi.

Kwanza kabisa ni vyema mwanamke akatambua ukweli kuwa, kukosa hedhi ni tatizo la kiafya, hata kama lisipoambatana na maumivu yoyote lakini mwanamke anapaswa kulitilia umakini wa hali ya juu.

Kwa sababu, kibaiolojia hedhi ya kila mwezi inatokana na mfumo unaojiendesha wenyewe ndani ya mwili pasipo ridhaa ya mwanamke husika, hivyo kutopata hedhi kunaashiria kuwa kuna tatizo kwenye moja ya mifumo aidha wa homoni au wa uzazi na kusababishwa na matatizo mengine.

Tatizo hili kwa kitaalam linaitwa amenorrhea, ni kukosekana kwa mzunguko mmoja au zaidi ya hedhi.  Kwa mwanamke aliyekosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo na kwa wasichana walio na umri zaidi ya miaka ya wastani wa 15-18 ambao hawajapata hedhi kwa pamoja, wapo kwenye kundi hili.

Sababu kuu ya kukosa hedhi ambao wengi pia tumeizoea ni ujauzito.  Kwa kawaida mwanamke hapati hedhi kwa kipindi chote cha ujauzito, kutokana na sababu za kibaiolojia.

Lakini sababu zingine zinaweza kuwa ni matatizo ya kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla au tezi zinazosaidia kuratibu viwango vya homoni mwilini kama nilivyoeleza hapo awali.  Ni muhimu kupata ushauri wa daktari ili kuchunguza moja ya matatizo haya.

Mwanamke hupitia dalili mbalimbali zinazoashiria kuwa ananyemelewa na tatizo hili, ikiwamo kutoa kiasi kidogo cha damu wakati wa hedhi, lakini pia mwanamke anaweza kupata dalili zingine kama vile uke kutoa ute wenye rangi ya maziwa mara kwa mara na hata wakati wa hedhi, maumivu ya kichwa, matatizo ya kuona maumivu kwenye kiuno na mgongo na kutokwa na chunusi usoni.

Tatizo la kutopata hedhi linaweza kutokea kwa sababu tofauti, baadhi ni za kawaida zinazojitokeza kwenye maisha ya mwanamke wakati mwingine yakisababishwa na matumizi ya dawa na matatizo mengine kiafya.

Kwanza kabisa, tatizo hili husababishwa na sababu za asili.  Katika kipindi tofauti, mwanamke anaweza kujikuta anakosa hedhi kutokana na sababu za ujauzito na kufikia umri wa kupoteza uwezo wa kuzaa kutokana na sababu za kiumri.

Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango.  Baadhi ya wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango wanaweza kukosa hedhi kwa kipindi fulani.  Na hata njia nyingine za uzazi wa mpango kama vile sindano na vipandikizi vinaweza kusababisha kukosa hedhi.

Aina fulani ya dawa ni kama vile dawa za magonjwa ya akili, tiba ya magonjwa ya saratani, dawa za sonona, dawa za shinikizo la damu na dawa za aleji.

Hivyo ni kawaida kwa mwanamke anayetumia dawa hizi kukosa hedhi kwa kipindi chote cha tiba.  Lakini pia sababu za aina ya maisha pia zinachangia kukosa hedhi.  Mathalani uzito uliopungua kupita kiasi.
Share:

MBOGAMBOGA ZINALETA AFYA BORA KWA ANAYETUMIASehemu kubwa ya mbogamboga (vegetables) inachukuliwa na maji kwa asilimia 84-96.  Kwa upande wa virutubisho vingine, mbogamboga ni chanzo kizuri cha madini ya Phosphorus na Calcium.  Vilevile ni chanzo kizuri cha Vitamin A na C.

Vitamin C inapatikana zaidi kwenye mbogamboga za majani ambazo zina rangi ya kijani, kama vile mchicha, kisamvu, matembele, majani ya kunde na yale ya maboga na kadhalika.  Kwa upande wa vitamin A inapatikana kwa wingi kwenye karoti.

Zaidi ya hayo, baadhi ya mbogamboga zina protini na kabohaidreti (wanga) kwa mapeyasi, maharage na viazi.

Nyuzi nyuzi za kilishe (dietary fibres) pia zinapatikana kwa wingi hasa katika mbogamboga za majani.

Vitamin C ni kirutubisho kinachopotea kwa haraka wakati wa upikaji wa mbogamboga.  Ili kupunguza tatizo hilo, mbogamboga zipikwe kwa dakika chache, kama tano mpaka kumi.  Kwa utaratibu huu, maji yachemshwe kwanza.  Yaani osha mboga zako vizuri kwa maji safi halafu zitie katika maji yaliyochemka.  Baada ya dakika hizo tano mpaka kumi zitakuwa zimeiva kwa kiasi ambacho hakitapoteza vitamin C kwa wingi.

Sambamba na hatua hiyo, mbogamboga lazima zipikwe kwenye chombo kilichofunikwa ili vitamin zisiondoke na mvuke.  Pia, watu wajilazimishe kunywa ule mchuzi (supu) unaopatikana baada ya kupika hizo mbogamboga.  Hii ni kwa sababu, mchuzi huo una vitamin nyingi inayotoka kwenye mbogamboga.

Vitamin na madini ni muhimu sana mwilini.  Kwa sababu zinasaidia kuupa mwili kinga ya maradhi mbalimbali na madini kama ya chuma, yanahitajika kwa utengenezaji wa damu.  Bila damu hakuna binadamu atakayeweza kuishi.

Nyuzinyuzi za kilishe nazo ni muhimu ili chakula kiweze kusagwa vizuri tumboni.  Pia, zinasaidia kunyonya sumu iliyoko tumboni ambayo inaweza kusababisha ugonjwa wa saratani (kansa).  Nyuzinyuzi hizo zinasaidia mtu kupata choo kikubwa mara kwa mara.  Yaani huondoa tatizo la kutopata choo.

Share:

NJIA BORA ZA ULAJI WA CHAKULA KWA AFYA BORA


Mtindo bora wa maisha ni kuishi kwa kuzingatia kanuni za afya na kwamba, mtindo bora wa maisha unahusisha kuzingatia ulaji bora, kufanya mazoezi ya mwili, kuepuka matumizi ya pombe, kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku ikiwamo dawa za kulevya pamoja na kuepuka msongo wa mawazo.

Mojawapo ya faida ya mtindo bora wa maisha kwa afya ni kuzuia kupata maradhi hasa yanayotokana na mtindo wa maisha usiofaa na kwamba, ulaji bora kwa kufuata mtindo bora wa maisha utakuepusha na shinikizo kubwa la damu, ugonjwa wa moyo, kisukari pamoja na saratani mbalimbali.

Njia bora ya ulaji unaofaa kwa afya

Daktari bingwa wa afya ya jamii na familia kutoka Chama cha Afya ya Jamii (TPHA) Ali Mzige, anasema moja ya njia bora za ulaji unaofaa ni kula mlo kamili ambao una mchanganyiko wa aina mbalimbali za vyakula.

“Mlo huu hukuwezesha kupata virutubishi muhimu vya kukidhi mahitaji ya mwili, lakini mlaji anatakiwa kuwa makini na mwangalifu asile chakula chochote kwa wingi kupindukia na anatakiwa kubadilishana aina za vyakula katika kila mlo”, anasema Dk Mzige.

Anasema vyakula hivyo husaidia mwili kujikinga na maradhi mbalimbali pamoja na kutupatia makapi mlo ambao humfanya mtu ajisikie kushiba na kupunguza uwezekano wa mtu kuwa na uzito au unene uliozidi.

Anasema uzito au unene uliopitiliza huongeza hatari ya kupata maradhi kama shinikizo kubwa la damu, kisukari, maradhi ya moyo na baadhi ya saratani.

Chagua asusa zenye virutubishi muhimu

Mtalaam huyo anasema ni vyema mlaji akachagua asusa zenye virutubisho muhimu, hivyo ni lazima mtu awe makini katika kuchagua asusa zenye virutubishi vingi na muhimu kama matunda, maziwa, sharubati ya matunda (juisi halisi), karanga, vyakula vilivyochemshwa, vyakula vilivyookwa au kuchomwa kama ndizi, mihogo, mahindi na viazi.

Asusa ni chakula kinachoweza kuliwa kati ya mlo mmoja na mwingine.

“Epuka asusa zenye mafuta mengi, chumvi nyingi au sukari nyingi kwa sababu huweza kusababisha ongezeko kubwa la uzito, huweza pia kusababisha kupata kisukari, shinikizo la damu au maradhi ya moyo” anasema.

Neema Joshua ni mtaalam wa masuala ya lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) anafafanua kuwa ulaji unaofaa ni kuongeza kiasi cha makapimlo ambayo yatasaidia katika mfumo wa chakula lakini pia huchangia katika kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya saratani, matatizo ya moyo na ugonjwa wa kisukari.

“Kupitia makapi-mlo unayokula unaweza kuongeza kiasi cha makapi-mlo kwa kula matunda badala ya sharubati (juisi), kupika mboga kwa muda mfupi, kutumia unga wa nafaka ambazo hazijakobolewa na kula vyakula vya jamii ya kunde mara kwa mara”, anasema Joshua.

Madhara ya mafuta mengi

Licha ya kuwa mafuta ni muhimu katika mwili wa binadamu, wataalam wanasisitiza mafuta hayo yanahitajika mwilini kwa kiasi kidogo.

Mafuta yanapoliwa kwa kiasi kikubwa yanaweza kusababisha madhara mwilini kama kuongeza uzito, kuongeza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo, kisukari pamoja na shinikizo la damu.

“Kutokana na hali hiyo, mtu anaweza kupunguza kiasi cha mafuta kwa kubadili njia za mapishi kama kuoka, kuchemsha, kuchoma badala ya kukaanga au kuchagua samaki au nyama isiyokuwa na mafuta pamoja na kuepuka asusa zenye mafuta mengi Dk Mzige.

Sukari nyingi

Dk Mzige anafafanua kuwa njia hii watu wengi wa rika mbalimbali hushindwa kujizuia na kutumia vitu vitamu kama biskuti, chocolate, keki, sharubati bandia, pipi, soda na hata ice cream bila kujua madhara yake.

Anasema licha ya sukari kuongeza nishati mwilini, huongeza uzito ambao huweza kusababisha mtu kupata maradhi mbalimbali ikiwamo kisukari, lakini huchangia kuleta madhara kwenye meno.
Matumizi ya sukari nyingi unaweza pia kuipunguza kwa kunywa vinywaji visivyokuwa na sukari kama sharubati ya matunda halisi na hivyo kuepuka vyakula vyenye sukari.

Chumvi nyingi

Hata hivyo, mlaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi  huchangia kuongeza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu, hivyo kukabiliana na hali hiyo, jamii inashauriwa kula vyakula ambavyo havijasindikwa kwa chumvi nyingi pamoja na kupunguza kiwango cha chumvi wakati wa kupika na kuwa na utamaduni wa kutoongeza chumvi ya ziada iliyopo mezani.

Wataalam wa lishe wanaeleza kuwa maji yana umuhimu mkubwa katika lishe na afya ya binadamu na mchakato wote wa lishe hauwezi kufanya vizuri bila maji.

Watu wanashauriwa kunywa maji angalau lita mbili kwa siku kwa sababu maji ni muhimu.
Share:

UMUHIMU WA TOHARA KWA WANAUME


Tohara ni kitendo kinachokubalika kijamii, kidini na kwa baadhi ya tamaduni. 

Kwanza ni vizuri kujua tohara ni nini?

Tohara ni upasuaji wa kitabibu ambao huiondoa ngozi ya mbele iliyochomoza kufunika kichwa cha uume.  Tohara haikuanza leo, ilianza tangu zama za kale, chanzo chake ni Imani za kidini.  Mpaka leo utaratibu huo umekuwa ukiendelea kurithiwa wazazi ambao huwatahiri watoto wa kiume.

Tohara inaweza kufanyika kwa mtu aliyezaliwa siku ya kwanza au ya pili.  Vile vile inaweza kufanyika nyakati za watoto wakubwa mpaka utu uzima.

Upasuaji huu huchukua dakika 10 tu kwa vijana na watoto, kwa watu wazima huweza kuchukua dakika 30 mpaka saa moja.  Jeraha huweza kupona kwa siku 5-7.

Kwa namna ilivyofunika huweza kuhifadhi unyevu nyevu na joto, mazingira haya ni makaribisho mazuri ya vimelea kuzaliana na kuleta madhara ya kiafya.

Mtu asiyetahiriwa, kwa ndani huzalisha vitu fulani mwilini yenye mwonekano mweupe kama maziwa yaliyokatika, uzalishaji wa taka mwili hiyo ambayo ni kisababishi cha saratani ya mlango wa uzazi kwa mwenza wa kike unayeshirikiana naye tendo la ndoa bila kutumia kinga yoyote.

Vilevile, ni kisababishi cha saratani ya uume ingawa inatokea mara chache.  Hivyo aliyetahiriwa huepushwa na mambo haya mawili.

Uwapo wa ngozi hiyo huweza kutengeneza hifadhi kwa vimelea mbalimbali kuzaliana kirahisi ikiwamo bakteria, fangasi/yeast.

Wanaume wasiotahiriwa huweza kupata maambukizi ya VVU kirahisi pamoja na magonjwa ya zinaa hii ni kutokana na eneo hilo kuwa na tishu laini ambayo ni rahisi kupata michubuko.

Hupata magonjwa mbalimbali ikiwamo shambulizi la mrija wa mkojo, uambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI), shambulizi la ngozi iliyozidi ya uume na shambulizi la sehemu ya kichwa cha uume.

Mara kwa mara mtu ambaye hajafanyiwa tohara hupata maradhi mbalimbali yanayochangia kupata muwasho kwenye uume, kuhisi muwasho kama moto na kutokwa na harufu mbaya.

Tohara inakuepusha na tatizo la kushindwa kurudisha nyuma ngozi iliyofunika uume mbele, kitabibu hujulikana kama phimosis.  Faida nyingine ya tohara ni pamoja na kuyafanya mazingira ya uume kuwa masafi hivyo pia kuongeza mvuto na hamasa kwa mwenza wake.

Tohara inakufanya kuwa na muonekano mzuri na kukuongezea kujiamini.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanaume wasiofanya tohara ndio wanaopata maambukizi ya VVU kirahisi, kutahiriwa kunapunguza hatari ya kupata VVU kwa asilimia 50 – 60  kama utajamiiana na mwanamke mwenye maambukizi.

Pia, kunapunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwamo yale yatokanayo na virusi vya herpes na papilloma.

Madhara machache ya tohara ambayo yanaweza kujitokeza ikiwamo maumivu, kupoteza damu, kidonda kupata maambukizi, uambukizi wa mlango wa uume na kukereketa kwa uume.

Madhara haya machache hayashindi faida za kiafya za tohara, ni vizuri kwa wasiotahiriwa kujitokeza ili wafanyiwe tohara.

Baadhi ya sehemu, huduma hii inatolewa bure kama sehemu ya vita dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya VVU.
Share:

MADHARA YA UTOAJI MIMBA


Utoaji mimba (abortion) ni kitendo cha kusitisha mimba kabla ya wiki 22 hadi 24 za ujauzito kamili wa mwanamke.  Utoaji mimba upo wa aina kuu mbili, kuna kutoa mimba kiharamu na kutoa mimba kutokana na matatizo ya kiafya kupitia ushauri wa daktari.

Leo tutazungumzia aina ya kwanza ya utoaji mimba ambayo inahusisha kutoa mimba kiharamu, bila ushauri kutoka kwa daktari, bila matatizo yoyote ya kiafya yaani ni kile kitendo cha kuchukua uamuzi binafsi kusitisha ujauzito.

Kutokana na utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), inathibitisha kwamba wanawake milioni 21.6 duniani hutoa mimba kiharamu, utafiti huu unawahusisha wanawake milioni 18.1 kutoka nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2008, unathibitisha kutokea kwa vifo 47,000 vya wanawake duniani kutokana na matatizo yanayotokana na utoaji mimba kiharamu hasa walio na umri kati ya miaka 15 – 44.

Hali ya utoaji mimba kiharamu imekuwa ikichangiwa na mambo mbalimbali.

Imeelezwa miongoni mwa sababu ni woga kwa wazazi na walezi wao.  Mabinti wengi huwaogopa wazazi na walezi wao kama watajua kuwa ni wajawazito hasa kabla hawajaolewa.  Wengi huwaza kuwa wanaweza kuadhibiwa hasa kama watakuwa wanasitisha masomo kwa sababu hiyo.  Pia huhofia kupoteza uaminifu kwenye familia zao.  Hali hii inasababisha mabinti wengi kutoa mimba kiharamu kwa kutumia dawa mbalimbali bila kujua madhara yake kiafya.

Kupata mimba bila matarajio na mipango, hali hii imejithibitisha kwa wasichana wengi walioko masomoni kama shule za msingi na sekondari na hata wa vyuoni, huku hali ikionekana kuwa kubwa kwa walio shule za sekondari na msingi kutokana na kuwa na uoga mkubwa wa kufukuzwa shule hivyo kukosa nafasi za kuendelea na masomo shuleni wengi majukumu haya yamekuwa yakiwashinda hali inayowalazimu kusitisha masomo yao.

Kushindwa kwa njia ya uzazi wa mpango ni moja ya sababu iliyosababisha wanawake wengi kujihusisha na kutoa mimba kiharamu.

Hutokea hasa pale mwanamke anapokuwa hana mpango wa kupata mtoto, hivyo kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa ajili ya kuzuia mimba.

Inapotokea kupata ujauzito huiondoa mimba hii kiharamu.

Hali ya kujiona mdogo sana kiumri, mabinti wengi wanaopata ujauzito hasa walio rika kati ya miaka 17 na 24 hujiona bado wapo katika umri mdogo sana wa kubeba mimba, hivyo wengi wao huamua kuitoa kiharamu jambo ambalo ni hatari kiafya.

Kutokuwa tayari na uhusiano wa baadaye na mwanaume aliyemtia ujauzito, huwafanya mabinti wengi hasa walio katika umri wa kuolewa, kuamua kutoa mimba kiharamu kwa sababu ya kutokuwa tayari kuwa katika uhusiano wa kindoa na mwanaume husika.

Hali mbaya ya kiuchumi

Mabinti wengi hufikia uamuzi wa kutoa mimba kiharamu kutokana na hali yao na wazazi wao kiuchumi kuwa mbaya.  Wengi wao huogopa gharama za kuilea mimba, kujifungua na kulea mtoto.

Shinikizo kutoka kwa wapenzi wao, hii pia imejidhihirisha hasa kwa mabinti walio bado katika uhusiano wa kimapenzi.  Wapenzi wao huwalazimisha kutoa mimba kutokana na sababu zao binafsi bila kufahamu uzito wa madhara yanayoweza kutokea.

Kuwa na aibu kwa marafiki na majirani, hali hiyo nayo huwafanya mabinti wengi wafanye kitendo hicho haramu kwa kuhisi kuwa watachekwa kuwa wameshajihusisha na tendo la ndoa kabla ya muda.

Madhara yake

Inamuweka mhusika katika hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi, ovary na ini.

Utafiti mbali mbali wa kisayansi unaonesha kuwa wanawake wenye historia ya kutoa mimba mara moja, wapo katika hatari mara mbili ya kupata saratani ya shingo ya uzazi ukilinganisha na wasio na historia ya kutoa mimba.

Wanawake waliotoa mimba zaidi ya mbili huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hizi kutokana na mabadiliko ya kiwango cha homoni hasa zile za ujauzito na kuharibika kwa shingo ya uzazi bila kupatiwa matibabu.

Ugumba ni moja ya madhara yanayotokana na kutoa mimba; hali hii imedhihirika kwa wanawake wengi wenye historia ya kutoa mimba katika kipindi cha nyuma.  Hii inatokana na madhara makubwa katika mfumo wa uzazi hasa katika mfuko wa uzazi.  Kujifungua watoto wenye matatizo katika mfumo wa fahamu yaani akili; hii inatokana na wanawake hawa kutoweza kubeba mimba kwa kipindi chote cha miezi tisa, hivyo kujifungua kabla ya wakati watoto (njiti), ambao huwa na mifumo ya mwili ambayo haijakomaa ukiwamo wa fahamu, hivyo kusababisha watoto hawa kuwa na matatizo ya akili maishani mwao.

Kupoteza damu nyingi kunakoambatana na homa kali, kutunga usaa kwenye kizazi, hali ambayo hupelekea kufanyiwa upasuaji wa dharura kuepusha kifo.

Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi; hali hii hutokea kwa sababu ya kuharibika kwa mirija ya uzazi inayofahamika kama fallopian tubes, kwani hupoteza utando unaoozesha yai baada ya kukutana na mbegu ya kiume kuelekea kwenye mfuko wa uzazi.  Hali hii husababisha mimba kukulia kwenye mirija hii ya uzazi badala ya kwenye mfuko wa uzazi.

Madhara kisaikolojia; wanawake wengi hujikuta wakiwa wagumba, au kupata maradhi ya saratani ya shingo ya uzazi pamoja na matatizo mbalimbali ya kwenye mfumo wa uzazi.

Na wengine hujiweka katika hatari kubwa ya kupoteza maisha.

Kutokana na utafiti mbalimbali uliofanywa na madaktari wa Finland 1997 umegundua kuwa wanawake wanaotoa mimba wana uwezekano wa kufa mara nne zaidi kuliko ambao hawatoi mimba.  

Vifo baada ya wiki moja ya kutoa mimba hutokana na kuvuja damu nyingi, madhara ya dawa za usingizi, mabonge ya damu kwenye mishipa ya damu na mimba iliyotunga nje ya uzazi.

Tutambue kwamba watoto wana haki ya kuishi hivyo kutoa mimba ni kosa la jinai.
Share: