Monday, February 19, 2018

MADHARA YA UTOAJI MIMBA


Utoaji mimba (abortion) ni kitendo cha kusitisha mimba kabla ya wiki 22 hadi 24 za ujauzito kamili wa mwanamke.  Utoaji mimba upo wa aina kuu mbili, kuna kutoa mimba kiharamu na kutoa mimba kutokana na matatizo ya kiafya kupitia ushauri wa daktari.

Leo tutazungumzia aina ya kwanza ya utoaji mimba ambayo inahusisha kutoa mimba kiharamu, bila ushauri kutoka kwa daktari, bila matatizo yoyote ya kiafya yaani ni kile kitendo cha kuchukua uamuzi binafsi kusitisha ujauzito.

Kutokana na utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), inathibitisha kwamba wanawake milioni 21.6 duniani hutoa mimba kiharamu, utafiti huu unawahusisha wanawake milioni 18.1 kutoka nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2008, unathibitisha kutokea kwa vifo 47,000 vya wanawake duniani kutokana na matatizo yanayotokana na utoaji mimba kiharamu hasa walio na umri kati ya miaka 15 – 44.

Hali ya utoaji mimba kiharamu imekuwa ikichangiwa na mambo mbalimbali.

Imeelezwa miongoni mwa sababu ni woga kwa wazazi na walezi wao.  Mabinti wengi huwaogopa wazazi na walezi wao kama watajua kuwa ni wajawazito hasa kabla hawajaolewa.  Wengi huwaza kuwa wanaweza kuadhibiwa hasa kama watakuwa wanasitisha masomo kwa sababu hiyo.  Pia huhofia kupoteza uaminifu kwenye familia zao.  Hali hii inasababisha mabinti wengi kutoa mimba kiharamu kwa kutumia dawa mbalimbali bila kujua madhara yake kiafya.

Kupata mimba bila matarajio na mipango, hali hii imejithibitisha kwa wasichana wengi walioko masomoni kama shule za msingi na sekondari na hata wa vyuoni, huku hali ikionekana kuwa kubwa kwa walio shule za sekondari na msingi kutokana na kuwa na uoga mkubwa wa kufukuzwa shule hivyo kukosa nafasi za kuendelea na masomo shuleni wengi majukumu haya yamekuwa yakiwashinda hali inayowalazimu kusitisha masomo yao.

Kushindwa kwa njia ya uzazi wa mpango ni moja ya sababu iliyosababisha wanawake wengi kujihusisha na kutoa mimba kiharamu.

Hutokea hasa pale mwanamke anapokuwa hana mpango wa kupata mtoto, hivyo kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa ajili ya kuzuia mimba.

Inapotokea kupata ujauzito huiondoa mimba hii kiharamu.

Hali ya kujiona mdogo sana kiumri, mabinti wengi wanaopata ujauzito hasa walio rika kati ya miaka 17 na 24 hujiona bado wapo katika umri mdogo sana wa kubeba mimba, hivyo wengi wao huamua kuitoa kiharamu jambo ambalo ni hatari kiafya.

Kutokuwa tayari na uhusiano wa baadaye na mwanaume aliyemtia ujauzito, huwafanya mabinti wengi hasa walio katika umri wa kuolewa, kuamua kutoa mimba kiharamu kwa sababu ya kutokuwa tayari kuwa katika uhusiano wa kindoa na mwanaume husika.

Hali mbaya ya kiuchumi

Mabinti wengi hufikia uamuzi wa kutoa mimba kiharamu kutokana na hali yao na wazazi wao kiuchumi kuwa mbaya.  Wengi wao huogopa gharama za kuilea mimba, kujifungua na kulea mtoto.

Shinikizo kutoka kwa wapenzi wao, hii pia imejidhihirisha hasa kwa mabinti walio bado katika uhusiano wa kimapenzi.  Wapenzi wao huwalazimisha kutoa mimba kutokana na sababu zao binafsi bila kufahamu uzito wa madhara yanayoweza kutokea.

Kuwa na aibu kwa marafiki na majirani, hali hiyo nayo huwafanya mabinti wengi wafanye kitendo hicho haramu kwa kuhisi kuwa watachekwa kuwa wameshajihusisha na tendo la ndoa kabla ya muda.

Madhara yake

Inamuweka mhusika katika hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi, ovary na ini.

Utafiti mbali mbali wa kisayansi unaonesha kuwa wanawake wenye historia ya kutoa mimba mara moja, wapo katika hatari mara mbili ya kupata saratani ya shingo ya uzazi ukilinganisha na wasio na historia ya kutoa mimba.

Wanawake waliotoa mimba zaidi ya mbili huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hizi kutokana na mabadiliko ya kiwango cha homoni hasa zile za ujauzito na kuharibika kwa shingo ya uzazi bila kupatiwa matibabu.

Ugumba ni moja ya madhara yanayotokana na kutoa mimba; hali hii imedhihirika kwa wanawake wengi wenye historia ya kutoa mimba katika kipindi cha nyuma.  Hii inatokana na madhara makubwa katika mfumo wa uzazi hasa katika mfuko wa uzazi.  Kujifungua watoto wenye matatizo katika mfumo wa fahamu yaani akili; hii inatokana na wanawake hawa kutoweza kubeba mimba kwa kipindi chote cha miezi tisa, hivyo kujifungua kabla ya wakati watoto (njiti), ambao huwa na mifumo ya mwili ambayo haijakomaa ukiwamo wa fahamu, hivyo kusababisha watoto hawa kuwa na matatizo ya akili maishani mwao.

Kupoteza damu nyingi kunakoambatana na homa kali, kutunga usaa kwenye kizazi, hali ambayo hupelekea kufanyiwa upasuaji wa dharura kuepusha kifo.

Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi; hali hii hutokea kwa sababu ya kuharibika kwa mirija ya uzazi inayofahamika kama fallopian tubes, kwani hupoteza utando unaoozesha yai baada ya kukutana na mbegu ya kiume kuelekea kwenye mfuko wa uzazi.  Hali hii husababisha mimba kukulia kwenye mirija hii ya uzazi badala ya kwenye mfuko wa uzazi.

Madhara kisaikolojia; wanawake wengi hujikuta wakiwa wagumba, au kupata maradhi ya saratani ya shingo ya uzazi pamoja na matatizo mbalimbali ya kwenye mfumo wa uzazi.

Na wengine hujiweka katika hatari kubwa ya kupoteza maisha.

Kutokana na utafiti mbalimbali uliofanywa na madaktari wa Finland 1997 umegundua kuwa wanawake wanaotoa mimba wana uwezekano wa kufa mara nne zaidi kuliko ambao hawatoi mimba.  

Vifo baada ya wiki moja ya kutoa mimba hutokana na kuvuja damu nyingi, madhara ya dawa za usingizi, mabonge ya damu kwenye mishipa ya damu na mimba iliyotunga nje ya uzazi.

Tutambue kwamba watoto wana haki ya kuishi hivyo kutoa mimba ni kosa la jinai.
Share:

No comments:

Post a Comment