Makengeza au strabismus ni moja ya magonjwa ya macho ambayo
huwakumba watu wengi. Makengeza ni hali
ya macho yote mawili kushindwa kuangalia upande mmoja kwa wakati. Yaani kila jicho kuangalia upande au uelekeo
wake.
Changamoto hii hutokea zaidi kwa watoto hususan wenye umri
chini ya miaka sita. Kuna aina mbili za
makengeza ambazo hujitokeza kwa watoto wenye umri huo.
Maradhi haya husababishwa na udhaifu wa misuli hii michache
husababisha ukosefu wa uwiano kati ya misuli inayoshikilia jicho.
Ukosefu huu wa uwiano huifanya misuli kuwa na nguvu zaidi ya
mingine hivyo kulielekeza jicho upande ambao ubongo haujapangwa.
Makengeza hutokea baada ya misuli inayoshikilia macho
kushindwa kufanya mawasiliano na kuyaelekeza kutazama eneo moja kutokana
kutokuwa na nguvu sawa za uoni.
Kwa kawaida ubongo ndio unaoratibu upande na kitu ambacho
jicho au macho yataangalia kwa wakati fulani kulingana na mahitaji ya mtazamaji
lakini itilafu inayokuwepo husababisha hili lisitokee. Chini ya uratibu wa kawaida, macho yote
mawili hutakiwa kuangalia sehemu moja ili kupata taswira ya kilichotazamwa.
Kwa mtu mwenye makengeza hilo halitokei kwa sababu kila
jicho hutazama upande wake hivyo kutuma taswira mbili tofauti kwa wakati
mmoja. Kutokana na mkanganyiko huu,
ubongo huitafsiri taswira iliyotoka kwenye jicho lenye misuli yenye nguvu zaidi
na kuiacha taswira iliyotoka kwenye jicho lenye misuli dhaifu.
Hali hii hutokea mara zote na ubongo hufanya kazi ya
kutafsiri taswira inayotoka kwenye jicho lenye misuli yenye nguvu.
Kutokana na ubaguzi huu wa kutafsiri taswira baada ya muda
jicho lenye misuli dhaifu huanza kupoteza uwezo wa kuona, endapo hatua za
kuyarekebisha makengeza hazitafanyika hatimaye jicho dhaifu hupoteza kabisa
uwezo wa kuona.
Aina
Kuna makengeza ambayo huwapata watoto wachanga walio chini
ya mwaka mmoja au infantile esotropia yaani estropia ya watoto wachanga. Wengi wa watoto wenye aina hii ya makengeza,
jicho moja huathirika zaidi ya jingine.
Estropia ya watoto |
Makengeza huweza kuambukiza pia. Hii hutokea kwa watoto wenye umri kati ya
miaka miwili mpaka mitano. Kitaalamu
huitwa acquire esotropia au esotropia ya kuambukizwa. Makengeza haya huweza kurekebishwa kwa
kutumia miwani ya macho.
Makengeza pia huweza kutokea kwa watu wazima na mara nyingi
husababisha maradhi ya kisukari, uvimbe kwenye ubongo au jicho na majeraha ya
jicho.
Kwa wasioona mbali nao wanaweza kupata makengeza kwa kuwa
mara nyingi hutumia nguvu nyingi kutazama.
Watu wenye maradhi yanayohusiana na mfumo wa fahamu au wenye mtindio wa
ubongo wapo kwenye uwezekano wa kupata maradhi haya pia.
Walio hatarini
Kuna sababu zinazochangia makengeza ambazo hutofautiana
kulingana na mazingira ya kila mmoja.
Zipo sababu zinazozuilika na zile zisizoepukika ambazo ni nyingi zaidi.
Ugonjwa huu hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi
kingine. Familia au ukoo wenye ndugu
mwenye makengeza, tafiti upo uwezekano mkubwa wa kuwa na mtoto atakayekuwa na
tatizo hilo pia kutokana na upungufu katika uumbaji wa misuli ya macho
yanayotokana na hitilafu kwenye vinasaba.
Watu wenye uvimbe kwenye ubongo ni kundi jingine ambalo lipo
kwenye hatari ya kupata maambukizi ya makengeza kwa sababu uvimbe huo huathiri
taarifa kutoka kwenye ubongo kwenda machoni kwa ajili ya utambuzi wa taswira
zinazotumwa.
Waliopata kiharusi au ajali iliyosababisha majeraha kwenye
ubongo nao wanaingia kwenye orodha hii.
Kiharusi hushambulia mishipa ya fahamu na kuifanya ishindwe kufanya kazi
ipasavyo kama ilivyo kwa ajali yenye majeraha kwenye ubongo. Moja ya haya likitokea, huongeza uwezekano wa
kupata makengeza.
Wanaougua kisukari ambacho huathiri mishipa ya fahamu na
macho moja kwa moja wanaweza kupata makengeza endapo hatua za makusudi
hazitochukuliwa. Hawa wanalingana na
wenye matatizo ya kushindwa kuona mbali.
Dalili
Dalili za makengeza hutofautiana. Inaweza kuwa kutokana na umri au sababu
zilizochangia maradhi hayo. Wengi huanza
kuziona dalili wanapokuwa wamechoka. Wazazi
wachunguzi kwa watoto wao huweza kuziona dalili hizo pia. Kwa mzazi anayependa kumchunguza mtoto ni
rahisi kwake kugundua makengeza kwa urahisi zaidi kuliko mzazi asiyefanya hivyo
kwa mtoto wake.
Kwa watu wazima huanza kuhisi changamoto wakati wa kutazama
kitu kwa kuwa huwa kuna taswira mbili zinatumwa kwenda kwenye ubongo. Hii husababisha ugumu kwa ubongo kutafsiri na
mgonjwa hugundua tatizo kutokana na ugumu huu wa kutambua taswira anayoitazama.
Wakati mwingine hutokea mgonjwa akaona taswira zaidi ya moja
kwa wakati. Kama mara kwa mara unaona
taswira zaidi ya moja kwa wakati mmoja ni vyema ukafanya uchunguzi wa kugundua
kama ni makengeza ama laa.
Ni kawaida kwa watoto kuwa na makengeza mara tu
wanapozaliwa. Hali hii haitakiwi kuwatia
wasiwasi wazazi ila ikiendelea kwa zaidi ya miezi mine au mitano basi ni vyema
kumpeleka mtoto hospitalini kwa ajili ya vipimo na ushauri wa daktari.
Ugunduzi
Licha ya kujichunguza na kugundua hitilafu kwenye utazamaji
wako au kumuangalia mtoto na kubaini hali isiyo ya kawaida, ni daktari pekee
mwenye mamlaka ya kuthibitisha makengeza.
Hivyo, inashauriwa kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo vinavyostahili.
Hospitalini daktari wa macho atachukua vipimo maalumu vya
kubaini uwezo wa macho kuona. Vipimo
hivi vitaonesha kama kuna tatizo ama la.
Ugunduzi wa mapema wa tatizo ni muhimu ili kuepusha
uwezekano wa kupoteza uwezo wa kuona. Ni
vyema kumpeleka mtoto hospitali kama amefikisha umri wa miezi mitano au zaidi
na bado ana makengeza. Inashauriwa mtoto
asifikishe umri wa miaka mitatu akiwa bado ana makengeza na hajapelekwa
hospitali.
Inashauriwa kumpeleka mapema ili hatua za kumuepusha na
madhara yatokanayo na makengeza zichukuliwe.
Madhara
Endapo matibabu ya makengeza hayatofanywa mapema na kwa
wakati upo uwezekano wa mgonjwa kupoteza uwezo wa kuona kwa kutumia jicho lenye
tatizo. Kwa wale wanaofanyiwa upasuaji
ili kurekebisha tatizo wanashauriwa waendelee kuvaa miwani ili kupunguza
uwezekano wa kujirudia kwa tatizo.
Kwa wale wasioona mbali wanahitaji miwani maalumu ya macho
kuwasaidia kufanya hivyo. Miwani hizi
hutolewa na kuuzwa hospitalini kutokana na ushauri wa daktari.
Mahitaji ya kufanya hivyo yakiwepo, madaktari wanaweza
kufanya upasuaji maalumu kwa lengo la kukaza misuli iliyolegea au iliyo dhaifu
na kurekebisha tatizo. Mgonjwa anaweza
kufanyiwa mazoezi maalum ya macho ili kumaliza tatizo alilonalo. Hili linaweza kufanyika kwa kuziba jicho
lisilo na tatizo ili kulazimisha ubongo kufanya kazi na jicho lenye misuli
dhaifu ili lisipoteze uwezo wa kuona.
Habari mwisho mtoto wa umri gani anaweza kutibwa makengeza ?
ReplyDeleteKengeza la kurithi linatibika pia??
ReplyDeleteMim nin kengez jich moja tib ni ip
DeleteMimi Nina kengeza ila sijazaliwa nalo kwenye jicho moja je nitumie dawa gani
ReplyDeleteTiba ni ipi
ReplyDelete