Tuesday, November 29, 2016

ZIPO TIBA NYINGI ZA JINO SIYO LAZIMA ULING'OE

meno kutoboka

Idadi ya wagonjwa wanaong’oa meno inazidi kuongezeka kadri siku zinavyokwenda.  Wengine hubadili meno yaliyotoboka na kununua bandia ili kuwa na mwonekano wao.

Kutoboka kwa jino ni hali ya kuwa na tundu.  Wakati mwingine meno kadhaa huwa na matundu ambayo ni matokeo ya sababu mbalimbali zikiwemo bakteria wa kinywa, ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kutosafisha kinywa vizuri.

Licha ya uwepo wa tiba ya tatizo hili, ipo haja ya watu kubadili mfumo wa maisha ili kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi yatakayochangia meno kutoboka yanayozidi kuenea duniani yakiathiri kila mtu, wakiwamo watoto wadogo.


Kutoa taarifa ya maumivu ili kuchunguza meno na kinywa chote ni moja ya namna sahihi za kutambua jino au meno yaliyotoboka ama kuoza.  Endapo kutakuwa na haja kwa ushauri wa daktari, mgonjwa anaweza akafanyiwa X-ray.  Kila mwenye meno ana uwezekano wa kupata matundu kwenye meno kutokana na sababu tofauti ambayo yasipotibiwa mapema huweza kuathiri matabaka ya jino na kusababisha maumivu makali ambayo yakizidi mgonjwa huweza kuling’oa endapo jitihada za kulitibu hazitafanikiwa.

Sababu

Zipo sababu nyingi zinazochangia meno kutoboka.  Nyingi zinaepukika na mhusika kuwa na uhakika wa afya ya kinywa chake.

Mara nyingi meno yanayotoboka ni ya nyuma.  Yanaitwa magego au masagego.  Kwa umbile, yana mifereji ambayo ni rahisi kwa mabaki ya chakula kujishika.  Yapo nyuma ukilinganisha na meno mengine hivyo kuongeza ugumu wa kuyasafisha.  Wengi hawafikishi mswaki maeneo ya nyuma ya kinywa.

Kutokana na hilo, tindikali huweza kujikusanya na kuyashambulia kwa urahisi zaidi kuliko meno ya mbele.  Hii haimanishi ya mbele hayawezi kutoboka kwani watu ambao meno ya mbele yametoboka wakati ya nyuma ni mazima.

Vyakula na vinywaji

Baadhi ya vyakula na vinywaji huweza kujishika kwenye meno kwa muda mrefu.  Hivi ni maziwa, ice cream, keki, na mkate hivyo kusababisha meno kutoboka kuliko vinywaji na vyakula ambavyo vinaweza kusafishika na kusafirishwa na mate kiurahisi.

Sukari

Unapotumia vinywaji vya sukari mara kwa mara unatoa fursa nzuri kwa bakteria walioko kinywani kushambulia meno yako kwa sababu unatoa fursa ya meno yako kukutana na tindikali muda mwingi ukilinganisha na mtu asiyetumia.

Kumlisha mtoto wakati wa kulala

Wazazi wanapaswa kuepuka kuwalisha watoto wadogo vyakula hasa vyenye sukari ili kuwafanya walale kwa sababu vitaendela kuwapo kinywani kwa muda mrefu baada ya mtoto kusinzia hivyo kuozesha meno yake mapema.

Inashauriwa, si vizuri kumuacha mtoto kutwa nzima akiwa anakula ama anakunywa vitu vya sukari kwa faida ya afya ya kinywa chake.

Kutopiga mswaki

Ingawa inaripotiwa kuwa karibu kila mtu duniani anapiga mswaki, ukweli ni kwamba kuna upungufu kwenye upigaji huo miongoni mwetu.  Watu wengi wana haraka kwenye kupiga mswaki hivyo kujikuta hawaufikishi sehemu zote za kinywa.

Kukosa floridi

Madini ya floridi huzuia kutoboka kwa meno na kusaidia kuliponya jino lililotoboka likiwa hatua za mwanzo.

Kutokana na faida yake madini haya huongezwa kwa makusudi kwenye maji ya kunywa kwa viwango stahiki.

Kutokana ukweli huo, unywaji wa maji ya kutosha kila siku, licha ya faida nyinginezo mwilini, huimarisha ubora wa meno.

Vilevile dawa za meno huwekwa madini hayo ili kuyaimarisha meno yetu.  Ni muhimu kuhakikisha dawa ya meno unayotumia ina madini ya floridi.

Kinywa kikavu

Kinywa kikavu ni matokeo ya upungufu wa mate ambayo kiasili huzuia kutoboka kwa meno kwa kuondoa mabaki ya chakula na utando mlaini kwenye meno.

Vilevile kemikali zilizomo kwenye mate husaidia kupambana na tindikali izalishwayo na bakteria na kutoboa meno.

Ukavu wa kinywa huweza kuleta vitu vinavyoathiri meno kama vile baadhi ya dawa za kutibu magonjwa mbalimbali, magonjwa yanayoathiri matezi, matibabu ya mionzi ya saratani kichwani au shingoni.

Haya yote huongeza uwezekano wa kutoboka kwa meno kutokana na kupunguza uzalishaji wa mate ambayo ni kinga ya kwanza kuepuka kutoboka.

Matibabu

Tiba ya jino siyo kung’oa kama inavyoaminika.  Ukweli ni kwamba kung'oa jino kutokana na sababu nyingi za kitabibu ambazo zinajitosheleza kwenye muktadha husika.

Kwenye tasnia ya tiba ya kinywa na meno, kung’oa jino lenye tatizo huwa ni hatua ya mwisho baada ya matibabu mengine kushindikana kutokana na sababu tofauti.

Sababu hizi zinaweza kuwa mgonjwa kushindwa kumudu gharama za kutibu jino lake pasipo kung’olewa au kutokua tayari kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya kuendelea na kukamilisha matibabu.

Nyingine ni mgonjwa husika kwenda hospitali wakati ana maumivu makali na huenda usiku wa siku hakula.

Baadhi ya wagonjwa huwa na aina ya matibabu wanayoyataka vichwani mwao.  Hawa ni ngumu kuwabadilisha na kuwapa tiba mbadala kwa tatizo alilonalo.

Ili ufaidike na matibabu ya kitaalamu ni vizuri kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kinywa na meno mara kwa mara kabla ya mambo hayajaharibika. Kumuona daktari mapema kunaongeza uwezekano wa kuokoa meno yenye tatizo.

Mara nyingi kutibu jino lililotoboka ambalo halina maumivu ni nafuu Zaidi ukilinganisha na jino lenye maumivu.

Licha ya kung’oa, mgonjwa anaweza kuondokana na tatizo la jino lililotoboka endapo atazingatia ushauri wa daktari.  Ushauri ni moja ya matibabu muhimu kwa watu wenye meno yaliyotoboka.

Kwa ushauri wa daktari mgonjwa atapata elimu ambayo wakati mwingine huweza kuwa msaada mkubwa kuliko kung’oa jino husika kama wengi wanavyofikiria.  Elimu hii hutolewa kulingana na ukubwa wa athari zilizobainishwa na vipimo.

Kuziba matundu

Kuziba meno ama kufanya ukarabati ni matibabu yanayoaminika Zaidi kwa meno yaliyotoboka hasa kwa matundu ambayo yamepevuka.

Hili hutakiwa kufanywa mapema kwani mgonjwa akichelewa atalazimika kuling’oa ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.

Dawa zinazotumika kuziba meno hutofautiana kulingana na mahali lilipo jino bovu hivyo gharama za dawa husika.

Kulijengea

Hapa ni kwa meno ambayo yameliwa na matundu na haiwezekani kuyaziba kikawaida.  Matibabu haya huwa na hatua kadhaa.  Pia yanaweza yasifahamike sana miongoni mwa watu wa kipato cha chini maana ni gharama.

Endapo njia hizo zimeshindikana jino linaweza likang’olewa.  Hili hufanywa kwa meno ambayo yametoboka, kuoza na kuisha kiasi ambacho huwezi kufanya ukarabati wowote.


Meno hayo yanashauriwa yaondolewe kwa usalama wa yanayobaki kwani uwepo wake wakati huwezi kusababisha maambukizi kwenye kinywa.
Share:

3 comments:

  1. Kutana na mtaalamu wa mitishamba anatibu ugumba na uzazi..kukuza uume..kukuza shape na hips ...masikio...kutibu jino bila kung'oa mpigie 0744903557 tanga

    ReplyDelete
  2. mimi pia nina dada anguuu anasumbuliwa na meno yote sijui tatizo nini

    ReplyDelete