Wednesday, November 16, 2016

MAKENGEZA YANAEPUKIKA UKIFUATA TIBA

tiba ya makengeza

Makengeza au strabismus ni moja ya magonjwa ya macho ambayo huwakumba watu wengi.  Makengeza ni hali ya macho yote mawili kushindwa kuangalia upande mmoja kwa wakati.  Yaani kila jicho kuangalia upande au uelekeo wake.

Changamoto hii hutokea zaidi kwa watoto hususan wenye umri chini ya miaka sita.  Kuna aina mbili za makengeza ambazo hujitokeza kwa watoto wenye umri huo.

Maradhi haya husababishwa na udhaifu wa misuli hii michache husababisha ukosefu wa uwiano kati ya misuli inayoshikilia jicho.


Ukosefu huu wa uwiano huifanya misuli kuwa na nguvu zaidi ya mingine hivyo kulielekeza jicho upande ambao ubongo haujapangwa.

Makengeza hutokea baada ya misuli inayoshikilia macho kushindwa kufanya mawasiliano na kuyaelekeza kutazama eneo moja kutokana kutokuwa na nguvu sawa za uoni.

Kwa kawaida ubongo ndio unaoratibu upande na kitu ambacho jicho au macho yataangalia kwa wakati fulani kulingana na mahitaji ya mtazamaji lakini itilafu inayokuwepo husababisha hili lisitokee.  Chini ya uratibu wa kawaida, macho yote mawili hutakiwa kuangalia sehemu moja ili kupata taswira ya kilichotazamwa.

Kwa mtu mwenye makengeza hilo halitokei kwa sababu kila jicho hutazama upande wake hivyo kutuma taswira mbili tofauti kwa wakati mmoja.  Kutokana na mkanganyiko huu, ubongo huitafsiri taswira iliyotoka kwenye jicho lenye misuli yenye nguvu zaidi na kuiacha taswira iliyotoka kwenye jicho lenye misuli dhaifu.

Hali hii hutokea mara zote na ubongo hufanya kazi ya kutafsiri taswira inayotoka kwenye jicho lenye misuli yenye nguvu.

Kutokana na ubaguzi huu wa kutafsiri taswira baada ya muda jicho lenye misuli dhaifu huanza kupoteza uwezo wa kuona, endapo hatua za kuyarekebisha makengeza hazitafanyika hatimaye jicho dhaifu hupoteza kabisa uwezo wa kuona.

Aina

Kuna makengeza ambayo huwapata watoto wachanga walio chini ya mwaka mmoja au infantile esotropia yaani estropia ya watoto wachanga.  Wengi wa watoto wenye aina hii ya makengeza, jicho moja huathirika zaidi ya jingine.
Estropia ya watoto

Makengeza huweza kuambukiza pia.  Hii hutokea kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili mpaka mitano.  Kitaalamu huitwa acquire esotropia au esotropia ya kuambukizwa.  Makengeza haya huweza kurekebishwa kwa kutumia miwani ya macho.

Makengeza pia huweza kutokea kwa watu wazima na mara nyingi husababisha maradhi ya kisukari, uvimbe kwenye ubongo au jicho na majeraha ya jicho.

Kwa wasioona mbali nao wanaweza kupata makengeza kwa kuwa mara nyingi hutumia nguvu nyingi kutazama.  Watu wenye maradhi yanayohusiana na mfumo wa fahamu au wenye mtindio wa ubongo wapo kwenye uwezekano wa kupata maradhi haya pia.

Walio hatarini

Kuna sababu zinazochangia makengeza ambazo hutofautiana kulingana na mazingira ya kila mmoja.  Zipo sababu zinazozuilika na zile zisizoepukika ambazo ni nyingi zaidi.

Ugonjwa huu hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.  Familia au ukoo wenye ndugu mwenye makengeza, tafiti upo uwezekano mkubwa wa kuwa na mtoto atakayekuwa na tatizo hilo pia kutokana na upungufu katika uumbaji wa misuli ya macho yanayotokana na hitilafu kwenye vinasaba.

Watu wenye uvimbe kwenye ubongo ni kundi jingine ambalo lipo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya makengeza kwa sababu uvimbe huo huathiri taarifa kutoka kwenye ubongo kwenda machoni kwa ajili ya utambuzi wa taswira zinazotumwa.

Waliopata kiharusi au ajali iliyosababisha majeraha kwenye ubongo nao wanaingia kwenye orodha hii.  Kiharusi hushambulia mishipa ya fahamu na kuifanya ishindwe kufanya kazi ipasavyo kama ilivyo kwa ajali yenye majeraha kwenye ubongo.  Moja ya haya likitokea, huongeza uwezekano wa kupata makengeza.

Wanaougua kisukari ambacho huathiri mishipa ya fahamu na macho moja kwa moja wanaweza kupata makengeza endapo hatua za makusudi hazitochukuliwa.  Hawa wanalingana na wenye matatizo ya kushindwa kuona mbali.

Dalili

Dalili za makengeza hutofautiana.  Inaweza kuwa kutokana na umri au sababu zilizochangia maradhi hayo.  Wengi huanza kuziona dalili wanapokuwa wamechoka.  Wazazi wachunguzi kwa watoto wao huweza kuziona dalili hizo pia.  Kwa mzazi anayependa kumchunguza mtoto ni rahisi kwake kugundua makengeza kwa urahisi zaidi kuliko mzazi asiyefanya hivyo kwa mtoto wake.

Kwa watu wazima huanza kuhisi changamoto wakati wa kutazama kitu kwa kuwa huwa kuna taswira mbili zinatumwa kwenda kwenye ubongo.  Hii husababisha ugumu kwa ubongo kutafsiri na mgonjwa hugundua tatizo kutokana na ugumu huu wa kutambua taswira anayoitazama.

Wakati mwingine hutokea mgonjwa akaona taswira zaidi ya moja kwa wakati.  Kama mara kwa mara unaona taswira zaidi ya moja kwa wakati mmoja ni vyema ukafanya uchunguzi wa kugundua kama ni makengeza ama laa.

Ni kawaida kwa watoto kuwa na makengeza mara tu wanapozaliwa.  Hali hii haitakiwi kuwatia wasiwasi wazazi ila ikiendelea kwa zaidi ya miezi mine au mitano basi ni vyema kumpeleka mtoto hospitalini kwa ajili ya vipimo na ushauri wa daktari.

Ugunduzi

Licha ya kujichunguza na kugundua hitilafu kwenye utazamaji wako au kumuangalia mtoto na kubaini hali isiyo ya kawaida, ni daktari pekee mwenye mamlaka ya kuthibitisha makengeza.  Hivyo, inashauriwa kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo vinavyostahili.

Hospitalini daktari wa macho atachukua vipimo maalumu vya kubaini uwezo wa macho kuona.  Vipimo hivi vitaonesha kama kuna tatizo ama la.

Ugunduzi wa mapema wa tatizo ni muhimu ili kuepusha uwezekano wa kupoteza uwezo wa kuona.  Ni vyema kumpeleka mtoto hospitali kama amefikisha umri wa miezi mitano au zaidi na bado ana makengeza.  Inashauriwa mtoto asifikishe umri wa miaka mitatu akiwa bado ana makengeza na hajapelekwa hospitali.

Inashauriwa kumpeleka mapema ili hatua za kumuepusha na madhara yatokanayo na makengeza zichukuliwe.

Madhara

Endapo matibabu ya makengeza hayatofanywa mapema na kwa wakati upo uwezekano wa mgonjwa kupoteza uwezo wa kuona kwa kutumia jicho lenye tatizo.  Kwa wale wanaofanyiwa upasuaji ili kurekebisha tatizo wanashauriwa waendelee kuvaa miwani ili kupunguza uwezekano wa kujirudia kwa tatizo.

Kwa wale wasioona mbali wanahitaji miwani maalumu ya macho kuwasaidia kufanya hivyo.  Miwani hizi hutolewa na kuuzwa hospitalini kutokana na ushauri wa daktari.


Mahitaji ya kufanya hivyo yakiwepo, madaktari wanaweza kufanya upasuaji maalumu kwa lengo la kukaza misuli iliyolegea au iliyo dhaifu na kurekebisha tatizo.  Mgonjwa anaweza kufanyiwa mazoezi maalum ya macho ili kumaliza tatizo alilonalo.  Hili linaweza kufanyika kwa kuziba jicho lisilo na tatizo ili kulazimisha ubongo kufanya kazi na jicho lenye misuli dhaifu ili lisipoteze uwezo wa kuona.
Share:

5 comments:

  1. Habari mwisho mtoto wa umri gani anaweza kutibwa makengeza ?

    ReplyDelete
  2. Kengeza la kurithi linatibika pia??

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mim nin kengez jich moja tib ni ip

      Delete
  3. Mimi Nina kengeza ila sijazaliwa nalo kwenye jicho moja je nitumie dawa gani

    ReplyDelete