Unapougua maana yake kinga zako za mwili zimeelemewa na
vijidudu vya maradhi vilivyoingia mwilini.
Licha ya kuelemewa huko, mfumo wa kinga unayo namna ya kujibadili na
kukabiliana vyema.
Endapo adui atakuwa mkubwa au mgonjwa anataka kupona haraka,
dawa huhitajika ili kuziongezea nguvu. Dawa
hizi, zisipotumika vizuri hasa zikizidishwa, huweza kusababisha kifo.
Miili yetu imeundwa kwa chembe ndogondogo zinazoitwa seli
ambazo hutengeneza viungo vyote vya mwili kama vile moyo, ubongo, ini, figo,
ngozi, mapafu na ngozi.
Kufanikisha chochote, miili hufanya kazi kwa kutegemea
kemikali mbalimbali kama vile protini, vichocheo vya kikemikali, vitamin au
madini ambazo husaidia kuuambia mwili ufanye nini au ufanyeje kazi.
Seli za mwili pia husaidia kuhamisha taarifa na kuusaidia
kufanya kazi azitakazo mhusika kama kawaida.
Shughuli hizi zote hufanywa na homoni pamoja na vichocheo vinavyoundwa
na seli.
Ili mwili ufanye kazi vizuri na maisha yaendelee ni lazima
kusiwe na kitu ambacho kinaingilia na kuingilia ufanisi wa seli na kemikali
mbalimbali zinazoratibu maisha na afya ya mwili.
Mtu akimeza kiasi kikubwa cha dawa ambazo, ikumbukwe, zote
ni kemikali, anakuwa amezidisha uwezo wa mwili kuzidhibiti kemikali hizo, hivyo
seli za mwili huathirika, kudhoofu hata kufa.
Dawa pia huweza kuingilia utendaji kazi wa kemikali za mwili
hatimaye kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.
Inategemea kiasi cha dawa ambacho mtu amezidisha. Ikiwa ni kiasi kidogo basi mwili utazidiwa
kwa muda, baadhi ya seli zitakufa na ufanyaji kazi wa viungo utaathirika
kidogo. Madhara ya kiasi kidogo cha dawa
yanaweza kumalizwa hospitalini.
Endapo mtu atazidisha kiasi kikubwa cha dawa basi seli
nyingi zaidi za viungo vya mwili vitaathirika.
Kwanza, seli zitakufa na viungo vitashindwa kufanya kazi. Mfano wa kiungo muhimu kinachoathirika na
kuweza kuhatarisha maisha ni ini. Endapo
kazi zote za ini zitasimama na hali ikaendelea kuwa hivyo kwa muda, basi
mhusika anaweza kupoteza maisha.
Kingine kinachoweza kutokea baada ya kuzidisha kiasi kikubwa
cha dawa kuzizuia seli na viungo husika.
Hili likidumu kwa muda mrefu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha. Mfano wa viungo vinavyoathiriwa sana ni figo,
ubongo, moyo na mapafu.
Kuzidisha dawa za kupunguza au kuongeza presha, mapigo ya
moyo au kisukari husababisha kushuka au kuongezeka zaidi kwa presha, mapigo ya
moyo au kisukari na kusababisha kupasuka kwa mishipa ya damu kwa dawa za
kuongeza presha.
Madhara mengine ya kuzidisha dawa hizi ni damu kuvujia
mwilini jambo ambalo ni hatari zaidi kwani inaweza kwenda kwenye ubongo na
kusababisha kiharusi, mapigo ya moyo kwenda kasi au kupungua zaidi, sukari
kuzidi au kupungua sana.
Likitokea lolote kati ya hayo yaliyoelezwa huweza
kusababisha kushindwa kwa viungo muhimu vya mwili na kuleta madhara makubwa.
Paracetamol au Panadol huweza kuharibu ini ndio maana mtu
anashauriwa asimeze zaidi ya vidonge vinane kwa siku. Ini likifa, maisha ya mgonjwa huwa
hatarini. Digoxin, dawa inayosaidia
kuongeza nguvu ya moyo ikizidishwa huweza kuufanya moyo kusinyaa na kudunda kwa
nguvu zaidi, moyo kushindwa kufanya kazi hatimaye kifo.
Dawa nyinginezo kama vile aspirin, diclofenac,
meloxicam au piroxicam zinazosaidia kupunguza maumivu mwilini huweza
kusababisha kufeli kwa figo hatimaye mwili hushindwa kufanya kazi vizuri na
ikiendelea mwili huzidiwa na hatimaye kifo.
asante sana kwa elimu hii, ni jambo kubwa sana nimejifunza hapa
ReplyDeletekazi yako ni njema sana