Mtindo bora wa maisha ni kuishi kwa kuzingatia kanuni za
afya na kwamba, mtindo bora wa maisha unahusisha kuzingatia ulaji bora, kufanya
mazoezi ya mwili, kuepuka matumizi ya pombe, kuepuka matumizi ya sigara na
bidhaa zinazotokana na tumbaku ikiwamo dawa za kulevya pamoja na kuepuka msongo
wa mawazo.
Mojawapo ya faida ya mtindo bora wa maisha kwa afya ni
kuzuia kupata maradhi hasa yanayotokana na mtindo wa maisha usiofaa na kwamba,
ulaji bora kwa kufuata mtindo bora wa maisha utakuepusha na shinikizo kubwa la
damu, ugonjwa wa moyo, kisukari pamoja na saratani mbalimbali.
Njia bora ya ulaji
unaofaa kwa afya
Daktari bingwa wa afya ya jamii na familia kutoka Chama cha
Afya ya Jamii (TPHA) Ali Mzige,
anasema moja ya njia bora za ulaji unaofaa ni kula mlo kamili ambao una
mchanganyiko wa aina mbalimbali za vyakula.
“Mlo huu hukuwezesha kupata virutubishi muhimu vya kukidhi
mahitaji ya mwili, lakini mlaji anatakiwa kuwa makini na mwangalifu asile chakula
chochote kwa wingi kupindukia na anatakiwa kubadilishana aina za vyakula katika
kila mlo”, anasema Dk Mzige.
Anasema vyakula hivyo husaidia mwili kujikinga na maradhi
mbalimbali pamoja na kutupatia makapi mlo ambao humfanya mtu ajisikie kushiba
na kupunguza uwezekano wa mtu kuwa na uzito au unene uliozidi.
Anasema uzito au unene uliopitiliza huongeza hatari ya
kupata maradhi kama shinikizo kubwa la damu, kisukari, maradhi ya moyo na
baadhi ya saratani.
Chagua asusa zenye
virutubishi muhimu
Mtalaam huyo anasema ni vyema mlaji akachagua asusa zenye
virutubisho muhimu, hivyo ni lazima mtu awe makini katika kuchagua asusa zenye
virutubishi vingi na muhimu kama matunda, maziwa, sharubati ya matunda (juisi
halisi), karanga, vyakula vilivyochemshwa, vyakula vilivyookwa au kuchomwa kama
ndizi, mihogo, mahindi na viazi.
Asusa ni chakula kinachoweza kuliwa kati ya mlo mmoja na
mwingine.
“Epuka asusa zenye mafuta mengi, chumvi nyingi au sukari
nyingi kwa sababu huweza kusababisha ongezeko kubwa la uzito, huweza pia kusababisha
kupata kisukari, shinikizo la damu au maradhi ya moyo” anasema.
Neema Joshua ni mtaalam wa masuala ya lishe kutoka Taasisi
ya Chakula na Lishe (TFNC) anafafanua kuwa ulaji unaofaa ni kuongeza kiasi cha
makapimlo ambayo yatasaidia katika mfumo wa chakula lakini pia huchangia katika
kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya saratani, matatizo ya moyo na ugonjwa
wa kisukari.
“Kupitia makapi-mlo unayokula unaweza kuongeza kiasi cha
makapi-mlo kwa kula matunda badala ya sharubati (juisi), kupika mboga kwa muda
mfupi, kutumia unga wa nafaka ambazo hazijakobolewa na kula vyakula vya jamii
ya kunde mara kwa mara”, anasema Joshua.
Madhara ya mafuta
mengi
Licha ya kuwa mafuta ni muhimu katika mwili wa binadamu,
wataalam wanasisitiza mafuta hayo yanahitajika mwilini kwa kiasi kidogo.
Mafuta yanapoliwa kwa kiasi kikubwa yanaweza kusababisha
madhara mwilini kama kuongeza uzito, kuongeza uwezekano wa kupata maradhi ya
moyo, kisukari pamoja na shinikizo la damu.
“Kutokana na hali hiyo, mtu anaweza kupunguza kiasi cha
mafuta kwa kubadili njia za mapishi kama kuoka, kuchemsha, kuchoma badala ya
kukaanga au kuchagua samaki au nyama isiyokuwa na mafuta pamoja na kuepuka
asusa zenye mafuta mengi Dk Mzige.
Sukari nyingi
Dk Mzige anafafanua kuwa njia hii watu wengi wa rika
mbalimbali hushindwa kujizuia na kutumia vitu vitamu kama biskuti, chocolate,
keki, sharubati bandia, pipi, soda na hata ice cream bila kujua madhara yake.
Anasema licha ya sukari kuongeza nishati mwilini, huongeza
uzito ambao huweza kusababisha mtu kupata maradhi mbalimbali ikiwamo kisukari,
lakini huchangia kuleta madhara kwenye meno.
Matumizi ya sukari nyingi unaweza pia kuipunguza kwa kunywa
vinywaji visivyokuwa na sukari kama sharubati ya matunda halisi na hivyo
kuepuka vyakula vyenye sukari.
Chumvi nyingi
Hata hivyo, mlaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi huchangia kuongeza uwezekano wa kupata
shinikizo kubwa la damu, hivyo kukabiliana na hali hiyo, jamii inashauriwa kula
vyakula ambavyo havijasindikwa kwa chumvi nyingi pamoja na kupunguza kiwango cha
chumvi wakati wa kupika na kuwa na utamaduni wa kutoongeza chumvi ya ziada
iliyopo mezani.
Wataalam wa lishe wanaeleza kuwa maji yana umuhimu mkubwa
katika lishe na afya ya binadamu na mchakato wote wa lishe hauwezi kufanya
vizuri bila maji.
Watu wanashauriwa kunywa maji angalau lita mbili
kwa siku kwa sababu maji ni muhimu.
No comments:
Post a Comment