Katika maisha ya kila siku yawezekana umewahi kukutana na
mtu ambaye ukiwa karibu naye akiongea au kutoa pumzi kinywani au puani utasikia
harufu mbaya.
Kwa kawaida mdomo na pua huweza kutoa pumzi nje ambayo huwa
na harufu asilia ambayo haiwezi kumkera mtu mwingine, lakini mara zingine hali
hiyo inaweza kujitokeza kutoa pumzi yenye harufu mbaya.
Watu wa karibu au wanaokutana na mwathirika wa hali hii
wanaweza wakadhani kuwa ni mchafu mwenye tabia ya kutopiga mswaki au
kutosafisha kinywa chake vizuri.
Pasipo kujua kuwa upo uwezekano mtu huyo akawa na tatizo
linalojulikana kitabibu kama Halitosis,maana
yake ni kutoa pumzi aidha kwa mdomoni au puani yenye harufu mbaya isiyo
vumilika.
Mtu mwenye tatizo hili anaweza kukumbana na kunyanyapaliwa
na wanajamii wanaomzunguka kiasi cha kuweza kumsababishia matatizo ya
kisaikolojia.
Muathirika anaweza kupatwa na tatizo la woga/hofu iliyopitiliza
anapokuwa kwenye kundi la watu, anaweza akajiondoa kutoka katika kundi hilo na
kujitenga na vilevile, baadaye huweza kupata sonona (depression).
Tatizo hili linalowakumba asilimia 20 ya wajamii duniani, ni
moja ya tatizo linalowafanya kufika katika huduma za afya kuwaona madaktari wa
kinywa na meno.
Hufika kwa wataalam hawa wakidhani wana magonjwa ya kinywa
ikiwamo mashimo katika meno, kulika kwa meno, kuoza kwa meno na magonjwa ya
fizi.
Si wagonjwa wote wenye kutoa pumzi yenye harufu mbaya wana
tatizo halisi la halitosis, kati ya
asilimia 5 hadi 72 wanaofika katika huduma za afya hugundulika kuwa hawana
tatizo hilo moja kwa moja.
Tatizo la kutoa pumzi yenye harudu mbaya ambalo ndiyo
halitosis halisi huwa linasababishwa na uwapo wa mrundikano wa bakteria katika
uvungu wa mafizi na nyuma ya ulimi jirani karibu na koo.
Kinywa kwa ujumla, ikiwamo meno, fizi, ulimi na vifuko vya
mate yanaweza kuwa ni maficho mazuri kwa mamia ya bakteria.
Ndio maana inaaminika tatizo la harufu mbaya mdomoni ni
kinywa chenyewe.
Kinywani pekee kuna karibu jamii 600 za bakteria ambao
huambatana na mabaki ya vyakula tunavyokula kila siku. Uwapo na protini ya kwenye mate na protini ya
vyakula tunavyokula, uvunjwaji wa mabaki yake na bakteria waliopo mdomoni ni
chanzo cha kuwapo kwa harufu mbaya.
Mabaki ya protini mdomoni ambayo huvunjwavunjwa na bakteria
na kuwa tindikali ya amino na hapo baadaye inapovunjwa, hutoa gesi yenye harufu
mbaya.
Mfano mzuri ni pale protini ijulikanayo kama methionine na cysteine inapovunjwa vunjwa kinywani huweza kutoa gesi yenye harufu
mbaya ijulikanayo kama hydrogen sulphide.
Mara nyingi harufu ya kinywa inaweza kuwa nzito Zaidi baada
ya kuamka ni kwa sababu wakati wa kulala mdomoni kunakuwa na kiasi kidogo cha
hewa ya oksijeni.
Bakteria waliopo mdomoni ni wale wasiohitaji hewa ya
oksijeni, hivyo kipindi cha usiku tuiwa tumelala ndipo huvunjavunja mabaki ya
chakula ambayo huambatana na kutolewa gesi zenye harufu mbaya.
Vilevile, harufu ya kinywa inaweza kubadilika kutokana na
vyakula tunavyokula vikiwamo vitunguu maji, vitunguu swaumu, iliki, tangawizi
na pia uvutaji sigara na unywaji wa pombe.
Hivyo si mara zote kupumua harufu isiyo ya kawaida, bali
mara nyingine inakuwa tatizo la muda tu lililochangiwa na vyakula na matumizi
mengine ya vitu.
Kwa asilimia 10 zilizobaki mara nyingi husababishwa na
matatizo mengine ikiwamo magonjwa ya kooni, puani, shambulizi za nyufa za
mifupa iliyopo usoni, magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa katika mapafu,
magonjwa ya masikioni na madhara ya ugonjwa sugu wa mafindofindo (tonsillitis).
Pia, uwapo wa majipu ya fizi/meno, vidonda mdomoni au
michubuko, vidonda vya kooni, huambukiza virusi vya herpes simplex na HPV. Mara chache pia tatizo hili linaweza
kuchangiwa na magonjwa ya ini ikiwamo kuharibika kwa ini na majipu katika ini.
Mara nyingine wanaolalamika tatizo hili hubainika kuwa ni
tatizo la usafi wa kinywa. Na
wanaposhauriwa kuboresha usafi wa kinywa kwa kutumia dawa za meno, au kusukutua
na dawa maalum za kusafisha kinywa nyuma ya ulimi, tatizo huweza kuisha haraka.
Inapotokea tatizo hilo chanzo chake sio mdomoni, ni vigumu
kuweka bainisho sahihi na vilevile hata kutibika kwake inakuwa vigumu.
Uchunguzi wa tatizo hili huanzia kwa mhusika mwenye we kwa
kueleza historia ya tatizo kisha wataalam wa kinywa au daktari wa kawaida
humchunguza kwa kumfanyia majaribio na vipimo kadhaa.
Baada ya wataalam wa afya kujua bainisho la ugonjwa ndipo
ushauri na matibabu huanza. Kama chanzo
cha harufu mbaya ni maradhi ambayo si ya kinywani, wataalam wa afya watakupa
matibabu ya kutibu chanzo hicho.
Kama chanzo cha kutoa pumzi yenye harufu mabya ni kinywa, wahudumu
wa afya watamuelekeza mgonjwa mambo mbalimbali kama ifuatavyo;
Kuhakikisha kupiga mswaki katika ulimi mara mbili kwa siku
kwa kutumia mswaki laini, kifaa kama kijiko kwa ajili ya kukwangua uso wa
ulimi, vilevile kutumia dawa yenye kiambata cha kuua bakteria.
Ulaji wa kifungua kinywa chenye afya ikiwamo kula matunda na
mboga za majani yenye nyuzi nyuzi husaidia kusafisha kinywa eneo la nyuma ya
ulimi wakati wa kumezwa.
Utafunaji wa bazooka unasaidia kuufanya mdomo usiwe mkavu na
hewa ya oksijeni kuingia kinywani kwa wingi, vilevile utafunaji wa bazooka
huweza kusaidia kutiririka kwa mate kwa wingi yanayosaidia kusafisha kinywa na
kuua vimelea vya maradhi.
Mdomo ukiwa mkavu na hautafuni chochote huchangia
kujiimarisha kwa bakteria wasihitaji hewa ya oksijeni.
Sukutua kwa maji mengi ikiwezekana ya uvuguvugu kila mara
baada ya kula chakula, na kabla ya kwenda kulala. Unaweza pia kutumia dawa maalum za
kusukutulia kinywa zenye dawa ya kuulia vimelea.
Jaribu kuboresha usafi wa kinywa kwa kuusafisha ulimi,
safisha meno kwa mswaki kila unapomaliza kula chakula, ondoa mabaki ya chakula
yaliyojibana katika meno na fizi na safisha na sukutua kinywa chako kwa dawa
maalum kabla ya kulala.
Unaweza kutumia vitu asilia vikiwamo majani ya miti na
karafuu kama njia ya kupunguza kupumua hewa yenye harufu mbaya.
Vizuri kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa mara kwa mara
angalau kwa miezi sita mara moja ili kuweza kubaini magonjwa mbalimbali ya kinywa
mapema.
No comments:
Post a Comment