Wakati gari likitegemea injini kuendeshwa barabarani, mwili
wa binadamu hutegemea moyo na endapo utasimama kwa tatizo lolote basi shughuli
zote hukoma.
Magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukizwa. Inakadiriwa, mpaka ifikapo mwaka 2020
magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza yatakuwa na uwiano sawa. Asilimia 50 kwa 50 kwa kusababisha vifo
duniani.
Magonjwa huwakumba zaidi watu wenye kipato kizuri kutokana
na tabia yao ya kutozingatia lishe bora.
Wananchi wa mataifa yaliyoendelea wapo kwenye hatari zaidi ya kupata
magonjwa haya. Licha ya ulaji holela,
watu hawa hawafanyi mazoezi kama inavyoshauriwa. Wanakula zaidi vyakula vya wanga na mafuta,
wanakunywa pombe na kuvuta sigara bila kujali athari zake.
Shambulizi la moyo au pigo la moyo kama wengine wanavyoliita
ni moja ya magonjwa ambayo yanaweza kumpata mtu yeyote. Limo miongoni mwa yanayoongoza kwa
kusababisha vifo vya wanaume na wanawake duniani.
Kwa kawaida, ugonjwa huu hutokea baada ya sehemu ya nyama ya
moyo kuharibika au kufa kutokana na kukosa damu ya kutosha. Yote yanaweza kusababishwa na kuziba kwa
mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye moyo kutokana na mafuta mwilini.
Waliohatarini
Watu walio kwenye hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu ni
pamoja na wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 45 kwa wanaume na 55 kwa wanawake,
wavuta sigara na wale wenye mafuta mengi mwilini.
Wengine ni wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, wenye
unene wa kupitiliza au kitambi na wenye matatizo ya figo. Wanywaji wa pombe kupindukia na wanaotumia
dawa za kulevya pia hasa cocaine na methamphetamine. Wengine ni wenye msongo wa mawazo wa muda
mrefu au upungufu wa vitamin B2,B6, B12 na folic acid.
Dalili
Maumivu makali ya ghafla kifuani ambayo husambaa kwenye
taya, shingo, bega na mkono wa kushoto ni dalili za awali. Kupumua kwa shida na kutokwa jasho kwa wingi
au kuhisi mapigo ya moyo kwenda haraka.
Kichefuchefu, kutapika na kuchoka haraka pamoja na kupoteza fahamu. Vichomi hasa vinavyosababishwa na vimelea vya
chlamydophila pneumonia. Tafiti mbalimbali
zinalihusisha shambulizi la moyo na msongo wa mawazo.
Matibabu
Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya
dharura. Lisipotibiwa kwa haraka huweza
kusababisha kifo ndani ya muda mfupi tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha kumuongezea
mgonjwa oksijeni na kupewa vidonge vya Aspirini ndogo vinavyozuia damu kuganda
pamoja na kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyoziba.
Kujikinga
Zipo njia kadhaa za kujikinga na shambulio la moyo ambazo
zinajumuisha kutovuta sigara, kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kupunguza
unywaji pombe. Kubadilisha aina ya mlo
kwa kupunguza mafuta na chumvi, kutumia mafuta ya samaki zaidi na baadhi ya
tafiti zinasema uchangiaji damu hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo hasa kwa
wanaume.
Madhara
Kifo kinaweza kutokea endapo moyo utashindwa kufanya
kazi. Upo uwezekano wa shambulio la moyo
kurudia mara ya pili.
Ili kutambua tatizo hili, mwaka 1979, Shirika la
Afya Duniani (WHO) liliweka vigezo vinavyojumuisha maumivu ya kifua kwa Zaidi ya
dakika 20.
No comments:
Post a Comment