Kabichi ni mboga inayopatikana maeneo maeneo mengi nchini
kutokana na urahisi wa kilimo chake. Inaliwa
ikiwa mbichi au ikipikwa sanjari na vyakula vingine vya aina tofauti.
Wapo wanaopenda saladi au kachumbari yake. Wengine wanataka iwepo kwenye kila mlo. Wapo wakulima wanaondesha maisha yao kutokana
na kilimo cha hii kutokana na kuiona fursa iliyopo.
Pamoja na matumizi yake mapana, wengi hawajui faida za
kiafya za mboga hii ambayo huuzwa kwenye masoko yote; ya mabwanyenye na
walalahoi na kuliwa na watu wa kada zote kwa uzito uleule. Inapatikana sokoni mwaka mzima, si mboga ya
msimu.
Tafiti zinabainisha virutubisho vinavyopatikana kwenye
kabichi vina uwezo wa kuzuia saratani ya matiti, utumbo mpana na tezi dume kwa
sababu huzuia viashiria vya saratani.
Mbali na viini hivyo kuzuia saratani, huimarisha ini
pia. Vitamin C inayopatikana katika
majani hayo husaidia ngozi na kuboresha uwezo wa kuona huku Vitamini K iuliyopo
ikiwa ni chakula cha ubongo ambao humfanya mlaji kuwa na uwezo mzuri wa
kufikiri.
Pale inapotumika ipasavyo, kabichi hupunguza au kutibu
kikohozi sugu na kusaidia usagaji wa chakula.
Wataalamu wa masuala ya lishe wanasema kabichi husaidia kutibu minyoo,
pumu na kusafisha tumbo kwa kumsaidia mtu kuharisha.
Mboga hii huondoa lehemu kwenye damu na huzuia uwezekano wa
kupata magonjwa ya moyo. Kabichi pia ina
vitamini A, B, C ambazo ni muhimu mwilini kwani husaidia kuimarisha kinga ya
mwili.
Faida nyingine ni kupunguza uzito na unene kutokana na
kiwango kidogo cha wanga ilichonacho.
Kabichi hupunguza tatizo la kufunga choo au choo kigumu
kwani ina kambakamba zinazosaidia kukilainisha na madini ya salfa na chuma
yanayosafisha tumbo.
No comments:
Post a Comment