Wednesday, January 11, 2017

VIRUTUBISHO MUHIMU KWA WATU WAZIMA

virutubisho muhimu kwa watu wazima


Watu wengi wenye elimu na umri zaidi ya miaka 20 wanafahamu umuhimu wa chakula katika miili yao.  Wanaelewa kuwa ili miili yao ipate virutubisho (nutrients) muhimu vya kujenga na kuimarisha afya zao lazima wale vyakula mchanganyiko ili kuvipata.

Watu wengi wakiwemo wasomi wenye maarifa hawana habari ya upungufu wa virutubisho katika miili yao.  Ukosefu unatokana na kutokula kwa mpangilio unaohitajika.  Mtu anapokula kiasi fulani cha chakula, haina maana mwili wake unapata mahitaji yote ya virutubisho kwa kiwango sahihi.  Ndiyo maana wataalamu wa lishe na afya wanahimiza kupima afya mara kwa mara kujua kiwango cha virutubisho kilichomo mwilini.  Vipo virutubisho vingi ambavyo kutokana na kutozingatia lishe bora, huwa vinapungua bila watu wengi kujua.

Madini ya Calcium

Umuhimu wa madini ya Calcium ni kujenga na kuimarisha mifupa na meno.  Mjamzito anahitaji madini haya kwa wingi zaidi ili kutengeneza mifupa ya mtoto aliye tumboni.  Mwili ukiyakosa madini haya kutoka kwenye vyakula hulazimika kuyapunguza kutoka kwenye mifupa na meno na kusababisha mifupa hiyo kuwa dhaifu na kuvunjika kwa urahisi.  Calcium inapatikana kwa wingi kwenye maziwa, dagaa, mifupa, maharage ya soya na mboga za majani zenye ukijani sana mfano spinachi.

Nyuzilishe

Chanzo kikubwa cha nyuzi lishe ni mboga za majani.  Matunda na nafaka zisizo kobolewa pia ni chanzo kizuri cha nyuzilishe.  Hata hivyo, watu wazima wengi hawali mboga za majani kiwango cha kutosha kila siku.  Nyuzi lishe ni muhimu kwa afya ya binadamu kutokana na kuhitajika kusaidia usagaji wa chakula, kuzuia magonjwa ya moyo, kisukari, uzito kupita kiasi, saratani ya utumbo mpana na kukosa choo kikubwa.  Nyuzi lishe zinaondoa sumu na uchafu kutoka tumboni, zinasafisha tumbo na ni chakula cha bakteria wasio na madhara wanaopatikana tumboni.  Watu wazima wanahitaji vikombe vitatu vya mboga za majani kila siku.  Kimoja asubuhi, mchana na jioni.

Madini ya Potassium

Madini ya potassium yanafanya kazi nyingi mwilini hivyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu.  Miongoni mwa kazi zake ni kusaidia moyo kufanya kazi vizuri na kuzuia magonjwa ya moyo na kisukari.  Watu wanaokula zaidi vyakula vilivyosindikwa wana nafasi finyu ya kupata madini haya.  Mara nyingi vyakula vilivyosindikwa vina madini ya sodium kwa wingi, hivyo huchukua nafasi ya madini ya potassium.  Hivyo ili kuwa na kiwango sahihi cha potassium unashauriwa kupunguza aina hiyo ya vyakula. Miongoni mwa vyakula vya hivyo ni maharage, mboga za majani zenye kijani zaidi, viazi mbatata, maziwa ya mtindi, parachichi, uyoga, ndizi na samaki.

Madini ya Magnesium

Yana kazi zaidi ya 300 mwilini, zikiwamo kusaidia kuweka sawa shinikizo la damu na kiwango cha sukari mwilini.  Bila ya madini haya mwili hauwezi kuzalisha nishati ya kutosha na kuifanya misuli ishindwe kukuchunjuka.  Vilevile, mwili hautaweza kudhibiti kiwango cha ziada cha lehemu kinachozalishwa na kuingizwa katika mzunguko wa damu.  Lehemu ikizidi ina madhara kiafya.  Spinachi, mbegu za maboga, maharage meusi, ndizi, korosho na nafaka zisizokobolewa ni miongoni mwa vyakula vyenye magnesium kwa wingi.
Share:

No comments:

Post a Comment