Friday, April 24, 2015

UMEUMBWA KWA AJILI YA JAMBO BORA ZAIDI



Mwandishi wa kimarekani Annie Dillard aliwahi kuandika juu ya mwanamke mmoja mzee ambaye alisema: “Inaonekana tumewekwa tu hapa chini, na hakuna anayejua kwa nini.” Hakuna anayejua kwa nini? Hata katika sarufi mbaya, hisia kali za swali la siku nyingi – sisi ni akina nani? Tumekujaje hapa? Inatupasa tuishije? Makusudi yetu ni yapi? – linajitokeza katika maneno yake.  Ni maneno muhimu pia, kwa sababu hatuwezi kuishi maisha kamili nay a afya bila kujua chanzo na makusudi ya maisha hayo kama mtu anyefikiria kuwa ipad ni ubao tu wa kukatia figili na vitunguu jikoni, anaposhindwa kuitumia ipasavyo.
Wanadamu wamekuwa na nadharia na visa mbalimbali kuelezea chanzo chetu.  Moja kati ya visa vya zamani kabisa kinasema, mungu mmoja alimwangusha mungu mwingine chini ambaye mwili wake ulikuwa dunia, na kwamba kila wakati yule mungu aliyeshinda anapoitemea mate maiti ya adui yake aliyeshindwa, mwanadamu hutokea. Kwa upande mwingine, moja kati ya visa vipya kabisa kinafundisha kuwa hatupo kabisa, bali ni mifano ya kompyuta iliyotengenezwa na jamii yenye akili sana ya viumbe wasiokuwa wa dunia hii.
Katikati ya dhana hizi mbili, ikiwamo ya Alex Rosenberg anayeamini kuwa hakuna Mungu, inayosema kuwa tupo kama vitu visivyo na maana katika ulimwengu wa vitu visivyo na maana.  Makusudi ya ulimwengu ni yapi?  Hakuna.  Makusudi ya uzima ni nini? Hakuna pia.  Hata hivyo, kukosa maana kwa ulimwengu wa vitu kunahuzunisha, usijali, kwani kulingana na Rosenberg, huzuni yako si kitu ila mpangilio wa neva na kemikali ambao unaweza kuubalisha kwa dawa.
Kinyume na nadhalia na visa vya jinsi tulivyotokea hapa duniani, mtazamo wa biblia unaendelea, hata leo kuwa wenye mantiki zaidi, wenye tumaini zaidi, na wenye maelezo yanayofaa juu ya chanzo na makusudi ya kuwepo kwa wanadamu (pamoja na upinzani usiokoma dhidi yake).  Pamoja na kwamba kwa hakika inajumuisha mtazamo wa vitu – na hata kuusherekea  - mtazamo wa Biblia juu ya ulimwengu hauishi kwenye vitu, kwani kufanya hivyo ingekuwa kama kutumia ipad kama ubao wa kukatia mboga.

Makusudi
Kinyume na dhana iliyoenea ya sayansi ya kisasa kwamba viumbe hai vya duniani vilitokea kwa bahati mbaya tu (dhana ambayo kwa kweli inatokana na falsafa na siyo sayansi), Maandiko yanaelezea kutokea kwa uhai kama tendo la moja kwa moja la Mwumbaji.  Katika kitabu cha Mwanzo kila kitu kina makusudi – hakuna kilichotokea kwa bahati.  Sisi si mkusanyiko wa kemikali mbalimbali zilizopangiliwa kwa kudra.  Fomula isemayo “Mungu akasema …iwe …ikawa hivyo” inaonekana kwa kujirudia kote katika maelezo ya uumbaji katika Mwanzo 1 na inaonesha azma ya makusudi ya moja kwa moja.  Kila mstari unakanusha dhana ya kwamba kitu cho chote kilitokea bila mpango.
Makusudi kama hayo ni muhimu hasa inapokuja kwa wanadamu.  Badala ya kutamka tu tukatokea na kuwa hai, kama alivyofanya kwa viumbe hai vya duniani, Mungu alimfanya Adamu kwa udongo na kumpulizia uhai.  “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7).  Ni tendo la uhusiano wa karibu ambalo, pamoja na mambo mengine, limewafanya wanadamu wawe viumbe pekee walioumbwa kwa “mfano wa Mungu” (Mwanzo 1:27).
Uumbaji ulikamilika kwa kuwepo kwa wanadamu, kana kwamba yale yaliyotokea katika zile siku tano kabla yetu yalikuwa kwa ajili yetu tu.  Baada ya kuumba wanadamu siku ya sita, Mungu alipumzika siku ya saba (Mwanzo 2:2), kwa kuwa kazi yake ilikuwa imekwisha: “Basi mbingu na nchi zikamalizika na jeshi lake lote” (aya ya 11).
Mwandishi mmoja wa kikristo, Ellen White aliandika kwamba “baada ya dunia na wanyama na mimea kuumbwa, aliumbwa mwanadamu, ambaye alikuwa kilele cha kazi ya Mwumbaji, na ambaye dunia ya kupendeza ilikuwa imefanywa ifae kwa ajili yake.  Alipewa mamlaka juu ya vyote ambavyo jicho lingeweza kuviona.”  Kinyume na dhana ya kifalsafa iliyoenea sasa, inayosema kwamba tulizuka tu, badala yake tulikusudiwa kuwepo hapa.


Kubadilisha Vipimo
Ingawa kitabu cha mwanzo kinafundisha kuwa Mungu aliiumba dunia maalum kwa ajili yetu, uvumbuzi wa hivi karibuni wa sayansi umefikisha utambuzi huo mpaka nje ya sayari yetu, mpaka kwenye sayari na nyote zingine.  Unaonesha vipimo vingi visivyobadilika ambavyo havirushusu badiliko hata dogo kabisa bila kufanya kuwepo kwetu kusiwezekane.
Kwa mfano, uwiano katika kani ya sumaku-umeme na kani ya uvutano ungebadilika kwa uwiano wa 1:10, wanadamu wasingekuwapo.  Uwiano wa 1:10 inamaanisha nini?  Mwanamahesabu John Lennox anaelezea: Lifunike bara la Amerika kwa sarafu na kuzipanga kwenda juuhadi mwezini (umbali wa kilometa 380,000), Kisha fanya hivyohivyo kwa mabara mengine bilioni moja yanayolingana na bara la Amerika.  Ipake rangi nyekundu sarafu moja kasha uiweke mahali katika moja ya yale marundo.  Mfunike rafiki yako macho na kumwambia aiokote ile sarafu.  Uwezekano wake wa kuiokota ni 1 katika 10.  Vipimo vingine vilivyowekwa kwa usahihi mkubwa angani, kama vile umbali kati ya dunia na jua, mwendokasi wa mzunguko wa dunia, kiasi cha nishati katika atom za kaboni, na kiwango cha kupanuka cwa ulimwengu, vilitakiwa view sahihi kabisa, vinginenvyo wanadamu wasingeumbwa.  Wanasayansi wameuita uwiano huu wa ajabu “anthropic concidence” – “anthropic” kutoka katika neon la kigiriki anthropos (“mtu”), na coincidences” kwa sababu, bila uwiano huo unaotatanisha akili, kusipokuwa na mwumbaji, zingekuwa kitu gani sasa?
Hata hivyo “coincidences” hizo zilikosewa sana kuitwa, zinasaidia kuthibisha mambo ambayo kitabu cha Mwanzo kinafundisha: Tunaishi katika viumbe vilivyokuwa vinatutarajia.  Hoja hii ni muhimu kwa kuwa msingi wa afya na furaha yetu kwa ujumla ni kutambua umuhimu na makusudi ya kuwepo kwetu.  Mhanga wa mateso ya vita kuu ya pili na mtaalamu wa magonjwa ya akili Viktor Frankl alisema kuwa, kimsingi, sisi wanadamu hatuna budi kuona umuhimu wa kuwepo kwetu, vinginevyo tutaishi bila tumaini, na tumaini ni nyeti kwa uzima wa mwanadamu.
Kwa kifupi, Kitabu cha Mwanzo kinatuambia kuwa badala ya kuwa “mkusanyiko wa kemikali” kwenye uso wa dunia (Stephen Hawking), sisi ni viumbe tulioumbwa kwa mfano wa Mungu na inatupasa kuakisi tabia yake na kuonesha wema na uwezo wake wakati sisi wenyewe tukistaajabu katika uwezo na wema na kukua na kukomaa humo.  Tukitambua kuwa tumeumbwa kwa sababu maalum, tunaona umuhimu na makusudi, ikiwa ni pamoja na afya na uzima, kwa kuyatafuta na kuyafuata makusudi na matakwa ya Mungu kwa ajili yetu.

Uzima mchanganyiko
Pamoja na kufundisha kuwa tulikusudiwa kuwa tulivyo, Kitabu cha Mwanzo pia kinaonesha tulivyo.  Kinyume na mtazamo wa kale wa kipagani unaotenganisha mwili na roho katika maeneo tofauti (mwili ukiwa mwovu na roho njema), Maandiko yanafundisha kile ambacho wengine wanakiita “uzima mchanganyiko”, dhana ya kwamba vipengele vyote  vya mwanadamu – kimwili, kiakili na kiroho – vinaunda kitu kimoja, na hakuna kipengele kinachoweza kuwepo bila kingine.  Mungu alipompulizia Adamu pumzi ya uhai, Biblia haiseami kwamba Adamu alipokea nafsi, kana kwamba roho ilikuwa kitu tofauti na yeye, bali alikuwa “nafsi hai” (nephesh hayah).  Alikuwa nafsi hai, hakuwa nafsi hai.  Ajabu ni kwamba, Biblia inatumia kirai hicho hicho kwa wanyama pia: “Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai (nephesh hayah) kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao” (Mwanzo 1:21 soma pia aya ya 24).  Ingawa bila shaka Adamu alikuwa tofauti na nyangumi na kobe kwa namna nyingi, lakini alikuwa nafsi hai kama wao, nephesh hayah.
Kuelewa hivyo kunaweza kutulinda dhidi ya aina mbili za kuvuka mpaka.  Ya kwanza, inaitwa duaslism inasisitiza zaidiupande wa kiroho na hata kutweza vitu vinavyoonekana kuwa ni viovu.  Hata hivyo kuanzia Mwanzo na kuendelea ambapo Mungu aliona kuwa dunia iliyokuwa imekamilika ilikuwa njema sana (Mwa 1:13), Maandiko yanachukulia kuwa vitu vilivyomo ulimwenguni ni matokeo ya uwezo wake wa kuumba.  Hata miili yetu, ingawa imeanguka, bado ni viumbe vya Mungu nab ado inahitaji kuheshimiwa hivyo: “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?  Wala ninyi si mali yenu wenyewe?” 1 kor. 6:19).  Dhana ya miili yetu kuwa miovu, tofauti na nafsi  safi ya milele iliyonaswa katika mwili na kungoja kufunguliwa kwa hamu, ni ya kipagani ambayo inamgawa mwanadamu bila sababu, na kukana umuhimu wa kipengele nyeti na cha msingi cha ubinadamu wetu.
Dhana nyingine inayovuka mpaka ambayo ni kinyume na iliyotangulia, inakana upande wa kiroho kabisa (kama tulivyoona kwa Alex Resenberg) na kuhafifisha ukweli wote, ikiwa ni pamoja na kila kipengele cha binadamu, na kuvifanya si kitu bali molekyuli tu zinazojongea.  Hii pia ni dhana ya kifalsafa au dhana ambayo inategemewa kwa sehemu kubwa na sayansi ya kisasa.
Mtazamo wa Biblia, ambao unasisitiza ukweli na umuhimu wa vipengele vya kimwili, kiroho na kiakili vya utu wetu, ni muhimu sana hasa katika kutafuta afya, uponyaji na furaha.  Akili na miili yetu ni sahemu zisizoweza kutenganishwa za uwepo wetu, na program yoyote inayotaka kutuletea maisha bora inahitaji kuzingatia sehemu zote za ubinadamu wetu tata na wa ajabu.
Afya inajumuisha kila kipengele cha utu wetu.  Kuwa na afya njema ni kuwa sawa kiakili, kuwa sawia kimihemko, kuwa mzima kimwili na kupatana na mwumbaji wetu kiroho.  Afya inahusika na mambo zaidi ya kutokuwepo kwa ugonjwa, inahusu akili, mihemko, miili, na hali zetu za kiroho.

Mwujiza wa uhai
Uchangamano wa ujumla wa utu wetu ulimfanya mwandishi wa Zaburi aandike: “Nitashukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha” (Zaburi 139:14).  Mfalme Daudi (ambaye wala hakuwa mwanafiziolojia) aliwezaje kujua kwamba alikuwa ameumbwa “kwa jinsi ya ajabu na ya kutisha”?  Mtu huyu aliandika takriban miaka 3000 iliyopita, muda mrefu kabla darubini na mashine za eksirei, ukiacha zile za CAT na MRI.  Daudi hakuwa najua seli ni nini, ukiacha mlolongo wa sehemu zake tata na za ajabu.  Alikuwa najua nini kuhusu maana ya kuzaliana  kwa seli au mwunganiko wa protini mbalimbali?  Wala asingeweza kujua protini ni nini?
Daudi hakuwahi kusikia juu ya DNA, na akili yake isingeweza kuelewa (wala yetu haiwezi, kwa kweli) jinsi mwili mmoja wa binadamu unavyoweza kuwa na mita trilioni 20 za DNA, na kwamba seti kamili ya vinasaba ina urefu wa zaidi ya herufi bilioni 3.5.  Alikuwa anajua nini kuhusu chembechembe nyeupe za damu zinazopambana na wavamizi, au kuhusu hatua nyingi za mtiririko wa vimeng’enya vinavyofanya damu igande?
Pamoja na hayo, Daudi alikuwa anajua kiasi cha kutosha kutambua jinsi ilivyokuwa ni muujiza kwa yeye kuwepo.

Uzima katika Ulimwengu Uliobomoka
Pamoja na kuumbwa kwa namna ya ajabu, bado sisi ni viumbe walioanguka katika ulimwengu (tazama Mwanzo 3), na kwa hiyo tunapatikana na maradhi, maumivu na mauti.  Hatimaye ukombozi wa Yesu pake yake, utakaofikia kilele wakati wa ujio wa pili, utaleta urejeshwaji na uponyaji kamili kwetu.  Kabla ya hapo, “wajibu wa kwanza kwa Mungu na kwa viumbe wenzetu ni wa kujiendeleza.  Kila uwezo ambao mwumbaji ametupatia unatakiwa kukuzwa kufikia kiwango cha juu kabisa tunaoweza.  Kwa hiyo ,muda huo unatumika kwa kuleta matokeo mema ambayo hutumika katika kujenga na kuhifadhi afya ya mwili na akili.
Bila shaka, Yule bi kizee aliyeongea na Annie Dillard alisema sawa: “tumewekwa hapa chini” Lakini kauli yake kwamba “hakuna ajuaye kwa nini” ilikuwa potovu kabisa.  Sisi tunajua ni kwa nini.  “Tumewekwa hapa chini; kwa sababu, kama Biblia inavyosema, Mungu “ndiye aliyetuumba” (Zab. 100:3).  Ndiyo, Mungu alituumba, akamfinyanga Adamu kutoka katika “mavumbi ya nchi” na kupulizia uzima na ufahamu katika mavumbi aliyokuwa ameyafinyanga naye akawa “nafsi hai”.  Mungu alituumba kwa makusudi, kufurahia uzima katika ukamilifu na utajiri wake wote, na kuujua upendo wa Mungu katika uzuri wake wote.  Katika kila moyo kuna utupu unaokera ambao ni yeye tu anayeweza kuujaza.  Anapoujaza utupu huo kwa ndani, anakuwa kusudi hasa la kuishi kwetu, na furaha yetu hukamilika.

Kuwepo kwetu ni muujiza, na maisha yetu ni zawadi ya thamani kubwa (mwulize mtu yeyote ambaye anaupoteza).  Na kama zilivyo zawadi zingine zote za thamani kubwa, inatupasa kuipenda na kuitunza, ambapo ni pamoja na kufanya kila tuwezavyo kujenga na kudumisha vipengele vya kimwili, kiakili na kiroho, vya mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu.  Sisi tu mawakili wa karama ya uzima.  Hakuna zawadi nyingine ya thamani na kazi ya muhimu kuliko kuishi maisha ya afya tele ili tuoneshe heshima kwa Mwumbaji wetu, kuwatumikia wengine na kuwa na maisha kamili.  
Share:

No comments:

Post a Comment