Mtindo wa
maisha, vyakula na shughuli za kila siku za mwanadamu ni baadhi ya vitu
vinavyosababisha idadi kubwa ya wake kwa waume kuwa na uzito au unene kupita
kiasi na wakati mwingine kuwa na vitambi.
Matatizo haya
yamekuwa yakiwapata watu wa jinsi zote na kuwanyima raha wanawake wengi, ambao
hufikia hatua ya kutumia mikanda maalumu ya kufunga tumbo au kuhangaika kupitia
njia mbalimbali ili kupunguza kadhia hiyo kwao.
Kutokana na
kuongezeka kwa tatizo hilo, kumezuka dawa nyingi zinazodaiwa kuwa na uwezo wa
kupunguza vitambi na uzito mkubwa, lakini wataalamu wa afya wanaonya kuwa ni
sumu.
Tafiti
nyingi za kisayansi zinaonesha kuwa dawa hizi kwa kiasi kikubwa zina kemikali
kama vile phentermine, sibutramine, phenolphthalein, caffein, hydroxycitric
acid (HCA) na senna ambazo zina madhara makubwa kwa afya ya mwanadamu.
Dk. Phil
McGraw anasema baadhi ya dawa hizo huathiri sehemu ya ubongo inayohusika na
hamu ya chakula. "Hamu ya chakula
ni muhimu kwa ajili ya ubora wa afya na maisha.
Dawa yoyote inayoharibu hamu ya chakula kwa kipindi kirefu, inaweza
kusababisha madhara ya kiafya", anasema Dk. Phil.
Mama mwenye
uzito wa kilo 108, Doreen Shayo anasema amewahi kujaribu dawa za kupunguza
mwili, lakini akapatwa na homa kali iliyohatarisha maisha yake baada ya wiki
moja, hivyo alishindwa kuendelea na dozi hiyo.
"Nilishawishiwa
kununua dawa hiyo ya kupunguza uzito na nilishauriwa kula mbogamboga, matunda
na maji kwa wingi wakati wa dozi, sikuwa nakula wanga wala chakula kamili. Nilipata homa ya ghafla madaktari
wakanishauri kwamba dawa zile hazikuwa nzuri kwangu hivyo niachane nazo, wakati
huo nilikuwa na kilo 120 lakini nilipungua kutokana na maelekezo ya
madaktari", anasema Doreen.
Baadhi ya
madaktari bingwa wa afya ya binadamu wanasema msukumo wa dawa hizo unaowafanya
wahusika kuharisha mafuta mengi kwa wakati mmoja, ni njia isiyo sahihi ambayo
pia huathiri baadhi ya viungo ndani ya tumbo, huku madhara yake yakijitokeza
miaka kadhaa mbeleni.
Tabibu wa
tiba mbadala kutoka kituo cha Fore Plan Clinic, Juma Mwaka anasema asilimia
kubwa ya dawa za kupunguza kitambi na mwili kwa uharaka ni sumu.
"Mtu
anapewa dawa anaharisha sana, swali la kujiuliza nini dawa inafanya tumboni na
kusababisha kupata choo laini au kuyeyusha mafuta kwa muda mfupi? Lazima tujue kwamba zina madhara baada ya
muda, wengi wanauziwa vitu vibaya na mbegu fulani ambazo ni sumu halafu mwili unabadilika
anaharisha sana, anaambiwa dawa ndio inafanya kazi yanatoka mafuta mengi, si
njia sahihi ya kupunguza uzito wa mwili au kitambi."
Dk. Samuel
Shita kutoka Hospitali ya Mwananyamala anasema kwa kawaida kuharisha humfanya
mtu kupunguza maji mengi na chumvichumvi mwilini na hivyo huathiri kazi ya seli
na mfumo wa fahamu.
"Dawa
hizo nyingi hazijaruhusiwa kutumika na Wizara ya Afya na wala hazijathibitika
kwamba ni sahihi kwa matumizi ya binadamu, lakini wanazitumia na madhara yake
yanaanza kujitokeza baada ya kutumia mtu anaharisha sana na yeye anadhani ana
mafuta lakini ule ni uteute unaokaa tumboni unaosaidia tumbo kufanya kazi.
"Utafiti
unaonesha kuwa watu wanaopendelea kula katika migahawa mikubwa ndio wanaoongoza
kuwa na miili mikubwa, teknolojia zipo na dawa zitumikazo lazima ziwe
zimefanyiwa utafiti kwa zaidi ya miaka 10.
Kuna madhara mengi yanayoweza kuwakuta watu ikiwamo ya figo, moyo, ini
na mishipa ya damu."
Dk Shita
anasema kuna njia sahihi za kupunguza tumbo ambazo pia ni salama. "Mtu anatakiwa kufanya mazoezi mepesi na
matumizi sahihi ya vyakula, tunatakiwa kupunguza vyakula vya wanga kupita
kiasi, sukari na mafuta. Pia tunatakiwa
kupunguza mafuta yatokanayo na wanyama kwa kuwa yana Cholesterol nyingi na
ulaji holela."
Anasema
soda, pipi na chocolate ni vyakula ambavyo havitakiwi kutumika kupita kiasi.
Mwaka
anazitaja hatua sahihi za kupunguza kitambi na kuondoa sumu mwilini akisema:
"Kutumia juisi za matango, karoti na nyanya kila siku kwa muda wa mwezi
mmoja sumu zote zinaondoka."
Hata hivyo,
Mwaka anasema mtu anapokula chakula ni lazima kiishe tumboni kabla ya kuingiza
kingine, vinginevyo anakuwa ametunza sumu mwilini kutokana na kuwa na mabaki
maengi ya chakula cha takriban hata mwaka mmoja.
"Mfuko
wa chakula una uwezo wa kutunza chakula kwa muda mrefu, ndiyo maana binadamu
hufa akikosa chakula kwa siku nyingi.
Miongoni mwa vitu vinavyofanya uondoe sumu mwilini ni kufuata sheria za
ulaji na njia za asili za kuondoa sumu hiyo na si njia za haraka kwani zina
madhara," alisema.
Wataalamu wa
masuala ya dawa Deborah Mitchel na David Dadson, katika kitabu chao
kilichochapishwa mwaka 2002 cha "The Diet Pill Guide: The Consumer's Book
of Over-the-Counter and Prescription Weight -Loss Pills and Supplements,"
wanasema:
"Ingawa
ushahidi wa dawa hizi unazidi kuongezeka, bado watu wengi wanaaminishwa kwa
uongo kuwa zina manufaa. Hata hivyo, pia
watu wanaendelea kuamini kuwa dawa hizi zinazotokana na mimea na ni dawa salama
za asili zinazofanyiwa utafiti wa kina na kuthibitishwa na mamlaka za udhibiti
na usalama wa dawa kama nyingine za hospitalini."
Namna ya kupunguza kitambi
Mwaka
anasema maji ya moto yakitumiwa kwa umakini yana uwezo wa kupunguza kitambi,
tumbo au uzito mkubwa wa mwili kwa asilimia 60.
"Maji
ya moto yana uwezo wa kupunguza tumbo kwa zaidi ya asilimia 60, unachotakiwa
kufanya ni kuyachemsha yawe ya vuguvugu kiasi kunywa kati ya glasi nne mpaka sita
na iwe ni katikati ya mlo mpaka mlo ndiyo maana kuna watu wanashauri unywe
asubuhi au iwe katikati ya mlo wa jana usiku na ule utakaokwenda kuula baadaye.
"Lakini
pagumu zaidi ni pale ambako kabla hujakwenda kupiga mswaki ndiyo unatakiwa
kuyanywa haya maji. Tunapata vitamin B12
ambazo zinazalishwa mdomoni wakati binadamu akiwa amelala na mojawapo ya
vitamin hiyo ni pamoja na kusaidia msagiko (mmeng'enyo) ule wa vyakula."
Anasema
tatizo la wengi kukaa na vyakula kwa muda mrefu tumboni, ni moja ya sababu pia
ya kuwa na tumbo kubwa yaani kuwa na mafuta ya ziada tumboni na wengine
wanakuwa na vyakula vingi wanavyoingiza kuliko wanavyovitoa.
"Asubuhi
kabla hujapiga mswaki ukaondoa zile vitamin mdomoni zinywe pamoja na maji,
kunywa maji ya vuguvugu glasi nne mpaka sita kila siku unapoamka asubuhi
mfululizo mpaka siku 21, baada ya muda fanya hivyo kwa wakati mwingine na
wakati ukifanya hivyo pia epuka vile vitu vitakufanya uendelee kuwa na tumbo
ili unachokifanya kiweze kuwa na majibu na si kuoga na kujipaka tope,"
anasema na kuongeza kuwa kupunguza vyakula vya wanga ni njia mojawapo
itakayomfanya mhusika kupata majibu ya haraka.
Naitwa seif niko tanga ni mnene mpaka sina raha wenzangu wanicheka nifanyeje
ReplyDeleteAhsante Bwana Seif kwa swali, unatakiwa upunguze kula vyakula vyenye mafuta na vyakula vya wanga. Pia, unatakiwa uwe unafanya mazoezi mara kwa mara.
DeleteNaomba kufahamu vyakula ambavyo havina wanga. Maana naona kama nimezungukwa na wanga tu mie.. Nini hasa cha kukila walau nipunguze uzito wajameni..
DeleteJitahidi kufanya mazoezi
ReplyDeleteMAZOEZI YAPI NI MAZURI KWA KUPUNGUZA KITAMBI?
ReplyDeleteUgali na wali je vinaongeza uziti na tumbo?
ReplyDelete