Monday, May 11, 2015

KIPI BORA KATI YA TUNDA NA JUISI YAKE?




Matunda na juisi asilia, vyote vina manufaa, lakini kimoja kinakuwa bora kuliko kingine kutegemea hali inayomkabili mtumiaji.

Matunda na mbogamboga ni katika vyakula bora kabisa kutokana na wingi wa vitamin, madini, sukari ya asilia na virutubisho vingine.

Mtu mwenye matatizo katika kutafuna anapokunywa juisi ya asilia, anavipata virutubisho hivyo kwa wingi zaidi katika glasi moja kuliko akila kipande cha tunda ambacho kitamchosha kutafuna na ashindwe kutumia kwa kiwango kinachotosheleza.

Kwa hiyo juisi ni chakula kizuri sana kwa mgonjwa ambaye mara nyingi meno yake hayawezi kutafuna vizuri na mahitaji ya nishati ya mwili wake ni makubwa.

Juisi hasa iliyotengenezwa na matunda halisi bila ya kuwekwa sukari au yenye sukari kidogo ni kinywaji kizuri na kina faida kubwa kwa wagonjwa na wenye afya bora.

Juisi inaongeza maji mwilini, inasafisha damu, inatoa sumu na vitu vingine vibaya mwilini.  Zaidi ya hayo, juisi za matunda na mbogamboga zinamsaidia mwili kuzalisha mkojo mwingi, hivyo zinasaidia kuondoa sumu mwilini pale atakapokwenda haja ndogo.

Pia, juisi ya asilia ni kinywaji mbadala kinachoweza kumuepusha mtu kujenga mazoea ya kunywa soda au juisi za viwandani.
Kwa upande mwingine, ulaji wa matunda kwa kutafuna na utumbo kusaga chakula vizuri ni bora kwake kula matunda badala ya kunywa juisi.

Katika mchakato wa kutengeneza juisi, baadhi ya virutubisho muhimu vinaharibika, vinapotea au vinaonekana kuwa ni uchafu na kutupwa.

Baadhi ya matunda ngozi zake zinaweza kuliwa na ni chanzo muhimu cha virutubisho.  Matunda hayo ni kama vile apple, blueberries, zabibu, strawberries, embe, pera na zambarau.

Ngozi ya matunda hupokea mwanga wa jua na kutengeneza virutubisho vyenye rangi mbalimbali ambavyo ni muhimu sana kwa ujenzi na ulinzi wa afya ya binadamu.

Mfano wa virutubisho hivyo ni carotenoids na flavonoids ambavyo vinasaidia kuimarisha kinga na afya ya mwili kwa ujumla.  Vitamin C inahitaji uwepo wa flavonoids ili kufanya kazi vizuri mwilini.

Ngozi ya matunda kama zabibu zinasaidia kulinda afya ya ngozi ya binadamu na kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa saratani.
Ngozi na nyama za ndani za matunda kama machungwa ni chanzo kizuri cha nyuzi lishe, ambazo hupotea wakati wa kuchuja juisi.

Nyuzi lishe zinasaidia usagaji wa chakula tumboni, humwezesha mtu kupata haja kubwa na kuepuka saratani ya utumbo mpana.  Zinapunguza pia kasi ya sukari kutoka katika utumbo na kuingia katika damu, na zinapunguza wingi wa nishati.

Kwa hiyo nyuzi lishe zinachangia kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa kisukari, unene na uzito kupita kiasi.

Ulaji wa matunda na mbogamboga unajaza tumbo na kumfanya mtu kujisikia ameshiba kwa muda mrefu.  Juisi inaleta shibe ya muda mfupi na kuongeza nishati mwilini kwa haraka.

Ili kupata manufaa ya matunda na juisi asilia, watu wale matunda na mboga za majani aina tofauti kila siku.  Pia, wanywe juisi asilia glasi moja kwa siku au kila baada ya siku mbili.

Tahadhari ni kwamba; imethibitishwa kisayansi kuwa unywaji wa juisi uliokithikiri unaweza kuchochea ugonjwa wa kisukari kwa wakubwa na watoto, unene na uzito kupita kiasi.


Share:

No comments:

Post a Comment