Tatizo la
kutokuwa na uwezo wa kuona vitu vilivyo mbali ni changamoto ya uonaji
inayowasumbua watu wengi sana Tanzania na duniani kwa ujumla.
Changamoto
hii hutambulika kwa mtu kushindwa kuona vitu vilivyo mbali. Watu hawa wanapoangalia mbali hushindwa
kutambua taswira zilizo mbali.
Tatizo la
kutokuwa na uwezo wa kutoona vitu vilivyo mbali hutokea pale macho au jicho
linapokuwa kubwa au sehemu ya jicho inayoruhusu mwanga wenye taswira kuingia
ndani ya jicho; yaani cornea, kuwa imekunjika kuliko kawaida hivyo kushindwa
kuelekeza mwanga wenye taswira kutua kwenye eneo la nyuma la jicho linalohusika
na kusafirisha kile kinachoonekana kwa ajili ya kutafsiriwa kwenye ubongo.
Hali hizi
mbili husababisha mwanga wenye taswira unaoingia kwenye jicho kutoweza kufikia
eneo la nyuma ya jicho yaani retina.
Hii
husababisha retina kushindwa kupeleka taarifa zenye taswira kwenye ubongo na
matokeo yake hushindwa kutafsiri taswira ambayo mtu anajaribu kuitazama. Matokeo yake ni wewe kushindwa kutambua
unatazama nini.
Mpaka sasa
sababu ya kwa nini watu wengine wanakuwa na macho makubwa, haijajulikana ila
kuna hisia kuwa hali hii hutokana na vinasaba na ndiyo maana tatizo hili
huoneakana zaidi kwenye familia zenye watu wenye tatizo hili.
Watu ambao
kwenye familia kuna historia ya tatizo hili ndio wako hatarini kukumbwa na hali
hii. Kama mzazi mmoja au wote wawili
wana tatizo hili (na wanavaa miwani) basi kuna uwezekano wa karibu asilimia 95
kwa mmoja wa watoto kuwa na tatizo hilo pia.
Wengine ni watu
wanaotumia muda mwingi sana kujisomea na wale wanaokosa muda wa kutoka nje na
kupata fursa ya kuangalia mbali mara kwa mara.
Dalili za
kutokuwa na uwezo wa kuona mbali ni kushindwa kutambua taswira halisi ya vitu
vilivyo mbali, kufinya macho au kukunja sura mara unapotaka kuangalia mbali,
kuumwa kichwa kutokana na kutumia nguvu nyingi kujaribu kutambua taswira ya
vitu vilivyo mbali na kushindwa kuona nyakati za usiku.
Kwa watoto
changamoto hii mara nyingi hutambulika tangu mtu mwenye tatizo hili akiwa mdogo
kabisa kiumri au anaonekana akiwa amekunja uso au kufinya macho au anasogea
karibu na runinga wakati anatazama au darasani mtoto anaonekana akisogea karibu
na mwalimu.
Dalili ya
tatizo hili kwa watoto pia ni kutofahamu kabisa yanayoendelea mbali na mahali
alipo au kufikicha macho mara kwa mara.
Tatizo hili
hugunduliwa kwa vipimo vya kawaida tu vya macho vinavyopatikana katika
hospitali maalum za matibabu ya matatizo ya macho.
Vipimo hivi
hupatikana kirahisi zaidi tukilinganisha na vipimo vya kupima tatizo
la kutoona vitu vilivyo karibu.
Hata hivyo
mtu yeyote mwenye matatizo ya macho anapaswa kwenda hospitali ili kuchunguzwa
na kupatiwa matibabu sahihi. Mgonjwa
yeyote wa macho anapaswa kuepuka kutumia miwani hata kama inaonekana kumsaidia
kutatua tatizo hadi amepatiwa na mtaalamu hospitalini.
No comments:
Post a Comment