Spinachi |
Uzito kupita kiasi ni jambo la hatari kiafya kwa kila mtu,
lakini zaidi kwa watu wenye umri mkubwa, wagonjwa na wale wanaoishi na Virusi
Vya Ukimwi (VVU).
Watu wenye uzito kupita kiasi wako katika hatari ya kupata
magonjwa mbalimbali yakiwemo shinikizo kubwa la damu, magonjwa ya moyo,
kiharusi, kisukari cha ukubwani, miguu kuuma au kuvunjika mifupa.
Uzito kupita kiasi pia, unaweza kuchangia kupunguza hamu na
nguvu za kufanya tendo la ndoa kwa wadau wote wawili, hivyo ndoa inaweza kuwa
katika wakati mgumu.
Mara nyingi uzito kupita kiasi unasababishwa na mtu kukosa
kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, kuvuta sigara, kunywa pombe kwa wingi
na ulaji usiofaa.
Ulaji usiofaa ni pamoja na kula kwa wingi vyakula vya wanga,
sukari na vile vyenye mafuta. Kula kiasi
kidogo vyakula vyenye nyuzi lishe kama vile mboga za majani na matunda ni
muhimu.
Zaidi walio katika hatari ya kupata uzito kupita kiasi ni
wale wale wanaotumia vyombo vya usafiri kwa muda mwingi, wanaokaa ofisini au
dukani kwa muda mwingi, wasiokuwa na taarifa za kutosha kuhusu afya na lishe
bora na wenye msongo wa mawazo. Vilevile
kuwa na marafiki wasiojali afya zao ni hatari kubwa zaidi ya kuwa na uzito
kupita kiasi.
Ulaji saladi ya spinachi, matunda ya epo na parachichi
unaweza kumsaidia mtu kuwa na uzito
unaotakiwa kiafya.
Matunda ya Apple |
Kabla mtu hajaanza kula mlo wake wa asubuhi, mchana au usiku
anashauriwa aanze na mboga za majani za spinachi au aina nyingine.
Saladi iwe chakula cha hamu.
Ulaji wa namna hii unamuwezesha mtu kula kidogo vyakula vyenye wanga,
sukari au mafuta ambavyo vina mchango mkubwa wa kuongeza uzito.
Vyakula vyenye wanga vinavyoliwa sana hapa nchini ni kama
vile wali, ugali, mikate, maandazi, vitumbua, chapati, viazi vitamu, viazi
mbatata, ndizi na chipsi.
Vyakula vyenye sukari ni pamoja na soda, keki, biskuti na
asali. Vyakula vyenye mafuta mengi ni
vile vilivyokaangwa ikiwemo chipsi kuku au mayai.
Mlo wa mboga za majani kama vile spinachi unajaza tumbo na
kumfanya mtu ajisikie ameshiba na hivyo kuzuiwa tabia ya kutamani kula vyakula
vya wanga au sukari.
Mboga za majani za spinachi, pia, zina kirutubisho
kinachoitwa thylakoids, ambacho kinachochea mwili kuzalisha homoni inayopunguza
hamu ya mtu kutaka kula, hasa vyakula vyenye sukari.
Kuhusu matunda ya epo, kwa siku mtu akila tunda moja ni
jambo zuri. Matunda ya epo yana maji na
nyuzi lishe ambazo zinalifanya tumbo kujisikia limeshiba. Matunda ya epo pia yana kirutubisho cha
pectin, ambacho kinakifanya chakula kilichopo tumboni kusagwa kwa muda mrefu na
kumfanya mtu kujisikia ameshiba.
Mtu akila tunda zima la epo, (sio juisi) kabla ya mlo, atajisikia
hali ya kushiba na hivyo atakula kidogo chakula cha wanga au sukari.
Kwa upande wa matunda ya parachichi, kula nusu ya tunda hilo
kwa siku kunaupa mwili mafuta bora kiafya na nyuzi lishe ambazo zinamfanya mtu
ajisikie ameshiba muda mwingi na kutokutamani chakula mara kwa mara.
Unapokula kwa wingi vyakula vya wanga, sukari au
mafuta, ndipo mwili unaongezeka uzito kupita kiasi.
No comments:
Post a Comment