Mungu alimwumba mtu
kwa mfano wake. Wakati wa uumbaji
mtu alikuwa mkamilifu machoni pa Muumbaji
na Ulimwengu. “nitakushukuru kwa
sababu nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu na ya kutisha” hivyo ndivyo mfalme Daudi
alivyoelezea kicho chake kwa Mungu aliyemwumba mwanadamu (Zaburi 139:14). Dhambi iliingia na kwa kuingia kwa dhambi
yakaja na mateso ya aina mbalimbali.
Kujaribu kujibu swali hilo hapo juu bila kuonesha anatomi ya
Mfumo wa Mkojo wa Mwanamme kutamuacha msomaji na maswali yasiyojibiwa na
taarifa zisizo wazi. Hivyo hebu
tujifunze anatomi ya mfumo wa mkojo kama ulivyoumbwa na Mungu.
Moyo husukuma damu kwenda katika viungo vyote vya
mwili. Damu inabeba hewa ya oksijeni na
chakula kwa seli za mwili. Hewa ya
oksijeni inatumika kama nishati ya kuunguza chakula ambacho nacho huzalisha
nishati ili kutegemeza seli za mwili.
Kama gari linavyounguza mafuta ili kupata nishati ya kuliendesha, seli
pia huunguza chakula kwa kutumia hewa ya oskijeni ili kupata nishati muhimu kwa
matumizi yake.
Wakati wa hatua hiyo ya kuunguza chakula, uchafu (ambao kama
ukiachwa kulundikana mwilini ungeweza kuwa sumu kwa seli) huwa unazalishwa.
Mungu katika hekima yake aliumba figo ili kuchuja takataka
(sumu) kutoka na kuziondoa mwilini. Damu
inaingia kwenye figo kupitia mishipa ya ateri za mafigo. Damu inachujwa na kuondolewa sumu zote. Maji yaliyochujwa yanayeyusha takataka
zilizochujwa na kuzalisha mkojo. Mkojo
husafirishwa kupitia ureta mpaka kwenye kibofu ili kuhifadhiwa. Wakati kibofu kinakuwa kimejaa (ujazo ni
karibu mililita 500), hisia hufanyizwa ambayo husababisha haja ya kutaka
kukojoa. Ndipo mtu anakwenda mahali
panapokubalika kijamii, na anapokuwa tayari misuli ya kibofu hukaza, na
musulibanifu (kilango) hufunguka na shinikizo linalosababishwa na kukaza kwa
kibofu hulazimisha mkojo kutoka kupitia katika urethra (ujia wa kutolea
mkojo). Wakati kibofu kinapokuwa tupu
musulibanifu hufunga na adha ya kibofu kilichojaa inapungua.
Wanaume wengi wanapata mabadiliko ya mkojo kadri wanavyokuwa
wazee, mabadiliko yanayoweza kusababishwa na uvimbeuchungu au ukuaji wa tezi ya
prosteti (BPH) ni moja tu ya sababu za dalili za matatizo katika mfumo wa mkojo. Hivyo hebu nianze kueleza kwa ufupi tezi ya
prosteti ni nini. Chini ya kibofu cha
mkojo kuna tezi ya prosteti ambayo inapatikana tu kwa wanaume. Kabla ya baleghe tezi hii huwa ni ndogo sana
lakini baada ya hapo inaanza kukua kwa kasi kutokana na mchocheo wa homoni ya
kiume iitwayo “testosterone”. Ujia wa
urethra unapitia katika tezi ya prosteti.
Kadiri ya mtu anavyo ongezeka umri tezi ya prosteti inakuwa kubwa zaidi
na zaidi. Inaweza kuongezeka ukubwa bila
kuwa na ugonjwa ndani yake au inaweza ikakua ikiwa na ugonjwa ndani yake (mfano
saratani). Kadiri inavyokuwa kubwa zaidi
inaufanya ujia wa urethra kuwa mwembamba.
Kubanwa kwa ujia wa kupitia mkojo husababisha matatizo katika kutoa haja
ndogo.
Matatizo haya yanaweza kuanza mapema katika umri wa miaka
arobaini (40) na kwa nadra sana hutokea kabla ya miaka arobaini. Waathiriwa wengi wa tatizo hili katika
mazingira yetu ya Afrika ni kati ya umri wa miaka 55 mpaka 70.
Je, Ni Matatizo Gani Ambayo Hawa Wanaume Wenye Tezi Kubwa ya Prosteti Hukabiliwa Nayo?
Sio dalili zote za haja ndogo zinatokana na mabadiliko
katika tezi ya prosteti. Aidha kuna
wanaume wenye tezi kubwa ya prosteti na bado wanapata dalili chache tu za
matatizo ya mkojo kama zipo.
Dalili za matatizo ya mfumo wa mkojo zinazojitokeza kwa kawaida
ni:
a.
Mchirizi dhaifu na unaokatizwa wa mkojo.
b.
Tatizo la kuanza kukojoa hata wakati kibofu
kimejaa.
c.
Hisia kuwa kibofu bado hakijatoa mkojo wote.
d.
Hitaji la kukojoa mara kwa mara wakati wa mchana
na wakati wa usiku.
e.
Hitaji la kukojoa mara moja au papo kwa papo
mara tu unapohisi kubanwa.
f.
Kuendelea kudondoka kwa mkojo baada ya kukojoa.
g.
Kujisikia kuunguzwa au maumivu wakati wa
kukojoa.
Wanaume wengine wanakuja hospitalini wakiwa na maumivu
makali ya kuzuiliwa mkojo ndani ya kibofu.
Hali hii ni ya maumivu sana na inahitaji huduma ya haraka ya kiafya ili
kuepuka uharibifu wa figo, nk. Wanaume
wengine wanakuja wakiwa na matatizo ya uzuiaji sugu wa mkojo. Taratibu huwawia vigumu zaidi kukojoa mkojo
wote, na mkojo mwingi zaidi hubakia kwenye kibofu baada ya kwenda msalani. Athari zingine za tatizo hili ni pamoja na:
uambukizo wa mara kwa mara wa kibofu cha mkojo, na kufanyizwa vijiwe ndani ya
kibofu cha mkojo.
Ni muhimu kumwambia daktari wako matatizo ya
mkojo kama yalivyoelekezwa hapo juu.
Katika wagonjwa 8 kati ya 10, dalili hizi huashiria dalili za BPH,
lakini pia zinaweza kuashiria matatizo mengine makubwa zaidi yanayohitaji
matibabu ya haraka. Hali hizi, ikiwa ni
pamoja na saratani ya tezi ya prosteti, zinaweza tu kufutiliwa mbali kwa
uchunguzi wa daktari.
No comments:
Post a Comment