Friday, October 14, 2016

KUISHI NA UGONJWA WA BARIDI YABISI

Hali mbaya kabisa ya baridi yabisi ambayo imeathiri mikono

Ugonjwa wa Baridi Yabisi ni Nini?

Ugonjwa wa baridi yabisi ni ugonjwa ambao unaathiri membreni ya sinovio na tishu inayozunguka vifundo (jointi); tishu hizo huwa nene, huganda kwenye kifundo na huharibu na kulemaza kifundo husika.  Ukiachwa bila kutibiwa, ugonjwa huu unaweza kuharibu vifundo vibaya kiasi kwamba havitafanya kazi tena.  Ugonjwa huu unapatikana mara nyingi kwa wanawake wanaoanza kuwa watu wazima hadi wenye umri wa kati.  Ili kutambua ugonjwa huu, daktari wako atakuchunguza, atachukua picha ya X-ray na vipimo vya damu vinaweza pia vikahitajika.


Dalili:

Ugonjwa wa baridi yabisi unaweza ukaathiri vifundo (jointi) vingi.  Lakini watu wanaelekea kuupata zaidi katika vidole na vifundo kati ya mkono wa mbele na kiganja.  Viwiko, magoti na tindi za miguu ni sehemu ambazo huathiriwa pia na ugonjwa huu.  Mara nyingi ugonjwa huu huathiri vifundo vilevile pande zote za mwili.  Dalili zinaweza kuwa ni:

1.       Vifundo kuvimba na kuuma.  Vinaweza kuonekana vyekundu na kuwa na joto.

2.       Vifundo kukakamaa.  Vipindi virefu vya kupumzika au kukitumia kifundo kwa muda mrefu au kwa nguvu sana kunaweza kusababisha kukakamaa.

3.       Vifundo ambavyo vimepoteza sura yake ya kawaida na hali yake ya kujongea.

4.       Kujisikia kuchoka wakati wote.

Kurekebisha Mtindo Wako wa Maisha

Ugonjwa wa baridi yabisi ni tatizo ambalo linaendelea.  Lakini sio lazima likufanye usijishughulishe.  Unaweza kusaidia kuutawala kwa njia ya mazoezi na mtindo wa maisha yenye afya.  Uwe na bidii kuwaona madaktari wako kama unavyotakiwa kwa ajili ya uchunguzi na kazi ya maabara.  Wakati Fulani daktari wako anaweza kukupeleka kwa daktari bingwa wa magonjwa ya athritisi na mengine yanayohusiana.

Fuata Mtindo wa Maisha Yenye Afya

Wakati hakuna hata mmoja anayejua sababu za ugonjwa wa baridi yabisi, vidokezi hivi vinaweza kukusaidia kupunguza dalili zako.

1.       Tafuta uwiano sawia wa mapumziko na kazi.

2.       Jifunze njia za kupunguza au kutawala msongo.

3.       Waombe wanafamilia au marafiki kukusaidia kazi.

4.       Bakia kwenye uzito wako sahihi.

Tumia Vifaa Maalumu

Hata kazi rahisi zinaweza zikawa ngumu kufanya vifundo vyako vinauma.  Vifaa maalumu na visaidizi vilivyo orodheshwa hapa vinaweza kurahisisha mambo kwa kupunguza mkazo na kulinda viungo.  Mwulize mhudumu wako wa afya ni wapi unaweza kupata vitu hivi na vifaa vingine vinavyosaidia:

1.       Vitu vya kuokotea na kushikilia vyenye mpini mrefu.

2.       Vifaa vya kufungulia gudulia na kutungia nyuzi.

3.       Banzi au vijiti kwa ajili ya kifundo vya mikono ya mbele na vifundo vingine.

4.       Vitu vikubwa vya kushikia, penseli, vifaa vya bustani na vifaa vingine vinavyoshikwa kwa mkono.

Anza Kufanya Mazoezi

Mazoezi ya taratibu yanaweza yakafanya iwe rahisi zaidi kutumia vifundo vyako.  Zingatia mambo yafuatayo wakati unapofanya kazi nje:

1.       Chagua mazoezi yanayoimarisha mjongeo wa vifundo na kufanya misuli yako iwe na nguvu zaidi.  Daktari wako au mtaalamu wa mazoezi ya viungo anaweza kukupendekezea mazoezi mengine.

2.       Shughuli zenye athari ndogo kama vile kutembea, kuendesha baiskeli au kufanya mazoezi kwenye maji ya uvuguvugu, ni zenye kufaa.

3.       Usijilazimishe kwa nguvu mno unapoanza.  Jenga ustahimilivu wako taratibu kwa kipindi Fulani.

4.       Wakati hali ya maumivu na kukakamaa ni mbaya sana, punguza kazi zako.

Tiba ya Dawa Inaweza Kusaidia

Madawa hayawezi kuponyesha ugonjwa wa baridi yabisi, bali yanaweza kukusaidia ujisikie vizuri zaidi.  Wakati mwingine zinaweza hata kukomesha ugonjwa, daktari wako anaweza kukuandikia dawa moja au zaidi kati ya hizo.  Hakikisha unazitumia kama ilivyoelekezwa.  Zinasaidia sana kwa kuzuia uharibifu wa vifundo kama zitaanzishwa mapema wakati wa ugonjwa.

Vidokezi vya Kutumia Dawa

Daktari wako anaweza kurekebisha aina ya dozi ya dawa zako kulingana na hitaji.  Kwa matokeo mazuri fuata vidokezi hivi:

1.       Tunza orodha ya madawa yako yote.  Mweleze orodha hii kila daktari unayeonana naye.

2.       Tumia madawa yako kama ulivyoelekezwa tu.

3.       usiruke wala usiache kutumia dawa bila kuzungumza na daktari wako.

4.       Tafuta kujua kama dawa zako lazima zitumiwe pamoja na chakula.

5.       Mwambie daktari wako kama umepatwa na athari kama kizunguzungu na matatizo ya tumbo.

Fanya vipimo vyote vya maabara ambavyo umeagizwa na daktari wako.  Matokeo haya yatamsaidia daktari wako kufuatilia namna ambavyo dawa zako zinakuathiri.

Kama Upasuaji Unahitajika

Kwa watu wenye uharibifu mkubwa wa vifundo (jointi), upasuaji unaweza ukapunguza maumivu na kufanya iwe rahisi kutumia kiungo.  Kwa kawaida kubadilisha kifundo, hasa cha nyonga au goti, ndio ambazo zinafanyiwa mara nyingi upasuaji katika hali hii.  Aina nyingine za upasuaji zinaweza kufanyika ili kusaidia kusaidia kuzuia matatizo mikononi au miguuni.

Vyanzo vya Msaada

Usiogope kutafuta msaada.  Kama una hofu/mashaka kuhusu afya yako zungumza na mhudumu wako wa afya.  Pia zungumza na watu wengine ambao wana ugonjwa wa athritisi ya kirumatoidi.  Wanajua hali unayopitia.  Labda wanaweza kukupatia ufahamu mpya na njia mpya za kusaidia kupambana na hali hiyo.

Ugonjwa wa baridi yabisi ni tatizo linalojulikana na ambalo huathiri ubora wa maisha wa takribani theluthi moja ya wanaume na wanawake .  Mungu ametuahidi kwamba “…………watapata nguvu mpya.  Watapanda juu kwa mbawa kama tai, watapiga mbio wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu wala hawatazimia.” (Isa 40:31).  Mungu akusaidie kuishi maisha ya afya na mtindo wa maisha wenye uwiano sawa, na uepuke kukakamaa kwa viungo na maumivu.
Share:

No comments:

Post a Comment