Utafiti umeonesha kuwa karibu nusu ya saratani zote
zingezuilika kwa njia ya mabadiliko katika mtindo wa maisha. Zaidi ya theruthi moja ya vifo vinavyotokana
na saratani ulimwenguni kote vimehusishwa na mambo kadhaa hatarishi ambayo
yangeweza kurekebishwa. Mambo hayo ni
pamoja na: lishe mbaya, uvutaji sigara/tumbaku, matumizi ya pombe, unene,
kukosa mazoezi na uchafuzi wa hewa, ngono isiyo salama, na kujianika
juani. Katika nchi zinazoendelea mambo
hatarishi zaidi ni uvutaji sigara/tumbaku, matumizi ya pombe, na ulaji kidogo
wa matunda na mboga za majani. Katika
nchi zilizoendelea uvutaji sigara/tumbaku, matumizi ya pombe na unene ndiyo
yanayoongoza.
Saratani
Saratani ni tatizo la kiulimwengu linalohusika na asilimia
12.5 ya vifo vyote ulimwenguni.
Kiulimwengu inaua watu wengi zaidi kuliko HIV/AIDS, kifua kikuu, na
Malaria vikiungana pamoja. Shirika la
Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa ifikapo mwaka 2020 viwango vya saratani
vitaongezeka maradufu kwa idadi ya wagonjwa wapya milioni 20 kwa mwaka. Zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa hao wapya
itakuwa katika nchi zinazoendelea ambako serikali hazijajiandaa kupambana na
mzigo unaozidi kuongezeka wa saratani.
Kila mwaka watu milioni 11 wanagunduliwa kuwa na saratani (bila kujumlisha
saratani ya ngozi) na kumbukumbu zinaonesha kuwa karibu watu milioni 7 wanakufa
kutokana na saratani. Hivyo, saratani
inaonekana kuwa ugonjwa mpya wa mlipuko katika nchi zinazoendelea.
Visababishi vya
Saratani
Saratani ni neno la jumla la kundi kubwa la magonjwa
yanayoweza kuathiri sehemu yo yote ya mwili.
Saratani ni ugonjwa wa jeni, ambazo zina uwezekano mkubwa wa mabadiliko,
hasa katika kipindi cha maisha marefu ya mwanadamu.
Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa ni viwango vidogo tu vya
saratani vinaweza kurithiwa. Sababu za
kimazingira ndizo za muhimu sana katika kusababisha saratani na zinaweza
zikabadilishwa. Mazoea ya mtu binafsi,
kama vile uvutaji sigara na matumizi mengine ya tumbaku, matumizi ya pombe, Chakula kisicho na afya, kutoushughulisha mwili, uzito mkubwa mno wa unene,
vina sehemu kubwa zaidi. Vitu vingine
hatarishi vya saratani ni: visababishi vya uambukizo kama vile virusi vya homa
ya Ini (viral hepatitis B) na uambukizo wa kirusi cha papiloma, mnunurisho
ioni; kemikali na uchafuzi wa viwandani, na madawa.
Vipengele Vinavyohusiana na Mtindo wa Maisha
Kwa sehemu kubwa, Saratani hutokea kama matokeo ya mtindo wa
maisha, na hivyo ni matokeo ya hali ambamo watu wanaishi na kufanya kazi. Mivuto ya mitindo ya maisha inahusika sana
kwa saratani nyingi. Mingi ya mielekeo
hiyo inazo athari kwa saratani na hata kwa magonjwa mengine. Kuchukua mtindo wa maisha yenye afya ambao
unajumuisha lishe ya afya, mazoezi ya mwili, uzito unaofaa wa mwili na
kuepukana na mazoea hatarishi, kunaweza kupelekea maisha marefu yenye
uchangamfu.
Miongoni mwa shughuli za uzuiaji, msisitizo unapaswa kuwekwa
juu ya mapendekezo yafuatayo ambayo yanahusiana na mtindo wa maisha:
1. Acha Matumizi ya Tumbaku
Moja ya mazoea ambayo ni wazi
yanasababisha saratani ni uvutaji sigara na matumizi mengine ya tumbaku. Tumbaku inasababisha karibu asilimia 20 ya
vifo vyote vya saratani, na vinavyokadiriwa kufikia watu milioni 1.2
kiulimwengu mwaka 2006.
Zaidi ya asilimia 80 ya saratani
mapafu kwa wanaume na asilimia 50 kwa wanawake husababishwa na uvutaji
tumbaku. Asilimia 90 ya saratani ya mdomo inatokea baada ya kukutana na tumbaku au pombe au vyote viwili.
Kuacha tumbaku ndio njia bora
zaidi ya kupunguza saratani. Kwa kawaida
vijana wanaanza mazoea ya kuvuta sigara katika makundi ya wenzao, na wanapaswa
washauriwe wasianze kuvuta. Uzuiaji wa
saratani lazima usisitize juu ya umuhimu wa kuzuia matumizi ya tumbaku kitaifa
na kimataifa.
2.
Epuka Matumizi ya Pombe
Upo ushahidi thabiti kuwa vinywaji
vya pombe ni sababu ya saratani ya mdomo, koromeo, zoloto, umio, matiti, na ya
utumbo mpana na rektamu kwa wanaume.
Vinywaji vya pombe vinaeleka kusababisha saratani ya ini na ya utumbo
mpana na rektamu kwa kina mama.
Zipo taarifa thabiti za kweli
zinazopendekeza kuwa vinywaji vyenye kileo visinywewe. Pendekezo hili linajumuisha vinywaji vyote
vyenye kilevi iwe ni bia, mvinyo, na pombe kali n.k. kipengele muhimu ni kiwango cha Ethanol
kilichonywewa. Hatari inazidishwa zaidi
wakati wanywaji wa pombe ni wanavuta tumbaku pia.
3.
Dumisha Uzito Ufaao wa Mwili
Upo ushahidi mkubwa kwamba uzito
mkubwa wa mwili na unene (kuongezeka kwa mafuta mwilini kupita kiasi) ni sababu
ya saratani ya utumbo mpana na rektamu, umio, endometrial, kongosho, figo, na
matiti. Utunzaji wa uzito wa mwili ufaao
kiafya katika maisha yote inaweza kuwa moja ya njia muhimu sana za kujilinda
dhidi ya saratani.
Hii itakuwa pia ni kinga dhidi ya
magonjwa mengine ya kawaida ambayo ni sugu.
Tunapaswa kuweka uwiano sawa kati ya nishati tunayoingiza mwilini
kutokana na chakula tulacho na nishati tunayoingiza kupitia shughuli za
kimwili.
4.
Shughulisha Mwili
Shughuli za kimwili ni tendo la
kutumia misuli iliyounganishwa na mifupa.
Maisha ya kukaa tu si maisha ya afya.
Ukweli mkuu ni kuwa shughuli za mwili au mazoezi yanakinga dhidi ya
saratani ya matumbo. Inaweza pia
kupunguza hatari za saratani ya matiti na ya mji wa mimba. Kwa kuwa kuushughulisha mwili na mazoezi
hutukinga dhidi ya ongezeko la uzito, uzito kupita kiasi, na unene, pia
hutukinga dhidi ya saratani ambazo hali hizo huongeza uwezekano wa kukumbwa
nazo. Ushahidi wa ziada unathibitisha
kuwa maisha ya kukaa tu bila kujishughulisha yanaongeza hatari ya ongezeko la
uzito, uzito kupita kiasi na unene.
Shughulisha mwili, fanya mazoezi
angalau dakika 30 kila siku. Mazoezi ya
mwili ya wastani yanaweza kuingizwa katika maisha ya kila siku. Sio lazima kutenga muda wa moja kwa moja wa
nusu saa kila siku kwa ajili ya mazoezi ya wastani. Kwa mfano, tembea kwa nguvu njia yote au
sehemu ya njia kwenda kazini, au shuleni: chukua pumziko la matembezi mchana au
jioni; tumia ngazi badala ya lifti.
5.
Kula Mlo Kamili
Milo yetu (hasa vyakula vilivyo na
kiwango cha juu cha nishati, yaani, vile ambavyo vimekobolewa, na vinywaji
vyenye sukari nyingi) vinaongeza hatari ya kupatwa na baadhi ya saratani, ikiwa
ni pamoja na saratani ya tumbo, matumbo, mdomo na koromeo. Kadhalika, vyakula vya mboga na matunda na
vyakula vingine vilivyo na nyuzinyuzi, huenda hutoa kinga dhidi ya saratani
kadhaa.
·
Kula
matunda na mboga kila siku: hivi ni vyanzo bora sana vya nyuzinyuzi na
vitamin. Kula sehemu 5 – 9 kila
siku. Vyakula visivyokobolewa ni bora
zaidi kuliko ambavyo vimekobolewa.
·
Punguza
chakula cha nyama: upo ushahidi mkubwa kuwa nyama ya makopo na nyama
nyekundu zinasababisha saratani ya utumbo mpana na rektamu. Jaribu kula samaki na kuku kwa kiwang kidogo.
·
Punguza
matumizi ya chumvi: chumvi na
vyakula vilivyo hifadhiwa kwa chumvi huenda ni visababishi vya saratani ya
tumbo. Epuka vyakula ambavyo
vimechafuliwa na sumu ya “aflatoxins” kwani vinasababisha saratani ya ini.
·
Lishe ya
Ziada: zipo taarifa za kweli kwamba
dozi kubwa ya baadhi ya virutubishi vya ziada inapunguza hatari ya baadhi ya
saratani. Chagua vyakula na vinywaji
vilivyo na virutubishi vingi badala ya lishe ya ziada.
6.
Kunyonyesha Maziwa ya Mama
Ushahidi kwamba kunyonyesha maziwa
humkinga mama dhidi ya saratani ya maziwa kwa umri wote ni mkubwa sana. Upo ushahidi kidogo unaoashiria kuwa
kunyonyesha maziwa kunamkinga mama dhidi ya saratani ya ovary (vifuko vya
mayai). Huenda kunyonyeshwa maziwa ya mama
huwakinga watoto dhidi ya kuwa na uzito kupita kiasi na unene, na hivyo kuwakinga
dhidi ya zile saratani ambazo husababisha na kuongezeka uzito, uzito kupita
kiasi na unene. Uzito kupita kiasi na
unene kwa watoto huelekea kuendelea mpaka maisha ya utu uzima.
7.
Punguza Kujianika Juani
Saratani ya ngozi katika aina zake
zote ni aina ya saratani inayofahamika pote ulimwenguni. Sababu kuu ya saratani ya ngozi ni kujianika
mno kwenye mnunurisho wa mwanga wa jua.
Hali nyingi za ugonjwa huu zingeweza kuzuiliwa kama watu wangejikinga
wanapokuwa juani na wahakikishe kuwa hawaunguzwi na jua kati ya saa 5:00
asubuhi na saa 9:00 alasiri na uvae kofia na miwani ya jua, n.k.
8.
Ngono
Kasi ya saratani inaweza kuwa
inaongezeka katika baadhi ya sehemu za Afrika kama matokeo ya moja kwa moja ya
mlipuko wa HIV/AIDS. Saratani
zinaonekana kuongezeka kutokana na HIV ni Kaposi’s sarcoma, Limfoma, saratani
ya tundu ya haja kubwa na uvimbe wa jicho.
Saratani nyingi za shingo ya kizazi zinasababishwa na kirusi cha
papilloma kinachosababisha uvimbe kwa wanadamu, na sababu kubwa ya saratani ya
ini ni kirusi cha ugonjwa hepatitis B.
virusi vyote hivyo huambukizwa kwa njia ya ngono. [Epuka zinaa].
9.
Punguza Msongo
Roho ya kujali na kujenga
itamsaidia mgonjwa wa saratani kuendelea kuishi. Hasira, kutokusamehe na ukali vinauweka mwili
katika hali ya msongo na kitindikali.
Jifunze kuwa na roho ya kupenda na kusamehe. Jifunze kuburudika na kufurahia maisha.
10.
Uchunguzi
wa Kila Mara wa Saratani
Uchunguzi wa saratani unaweza
kupunguza hatari na kuboresha utambuzi wa mapema. Programu za uchunguzi kama za shingo za kizazi,
uchunguzi wa utumbo mpana na rektamu, uchunguzi wa matiti, uchunguzi wa tezi na
prosteti ni wa muhimu. Kwa mfano,
saratani ya shingo ya kizazi ni mwuaji namba moja kwa wanawake wa Afrika na
uchunguzi rahisi tu shingo ya kizazi unaboresha utambuzi wa mapema na kuokoa
maisha.
Hitimisho
Sasa tunafahamu kiasi juu ya
sababu za saratani na namna ya kuzuia kwa ajili ya uingiliaji kati ya ufaao
kuwa na matokeo yenye maana. Angalau
theluthi moja ya waathirika wapya wa saratani wanazuilika kwa njia kama kuzuia
matumizi ya tumbaku na pombe, kuwa na kiasi katika lishe, kuushughulisha mwili
kila siku, kuchanjwa dhidi ya kirusi cha hepatitis B, na elimu juu ya mambo ya
ngono na uzazi. Pia inawezekana
kupunguza zaidi theluthi moja ya wagonjwa wapya kwa utambuzi wa mapema na tiba
ya haraka.
Mpango wa Mungu wa awali wa lishe
ya mimea ndio njia bora kuliko zote ya kujenga afya njema na kuzuia magonjwa
sugu kama saratani. Ikiwa tutafuta kwa
ukaribu zile njia 8 za tiba ya asili kama zilivyopendekezwa na E.G. White, mtindo
huo wa maisha wenye uwiano kiafya ungetusaidia kuondoa kabisa au kupunguza
visababishi vya saratani.
No comments:
Post a Comment