Wednesday, November 30, 2016

JINSI YA KUKABILI FANGASI KWENYE VIDOLE VYA MIGUU


Tunapozungumzia maradhi ya fangasi wengi wetu hatujisikii vizuri kabisa yaani kwa kifupi hili somo siyo kipenzi cha watu wengi.  Hii inatokana na jinsi maradhi haya yanavyojionesha.  Mara nyingi hutokea kwenye sehemu ambazo ni aibu kuzizungumzia au kuzionesha.  Bahati nzuri ni kuwa wala hatutakiwi tuone aibu kuzungumzia magonjwa haya kwani wengi wetu wanapata maradhi haya na yanahitaji matibabu.  Inasemekana Mtanzania mmoja kati ya watano hupata maradhi ya fangasi zaidi ya mara moja katika kipindi cha maisha yao.
  Ingawa wengi wetu tunaona vibaya kuongelea maradhi yaletwayo na fangasi, viumbe hivi vinafurahisha sana ukivisoma na kuvifahamu.  Zamani kabla ya sayansi haijaendelea wanasayansi walidhani fangasi ni mimea lakini baada ya maendeleo ya vifaa vya uchunguzi, walitolewa kwenye kundi la mimea.  Leo ninazungumzia kuhusu tatizo la fangasi wa vidole vya miguuni ni tatizo sugu kutokana na kuwakumba wengi hapa nchini na kuwasababishia usumbufu mkubwa.

Aina hii ya fangasi hushambulia vidole vya miguu peke yake na mara nyingi hushambulia maeneo ya katikati ya vidole vya miguu hasa kati ya kidole cha tatu na nne na kile kidogo, tunachokihesabu ni cha tano.

Fangasi hawa husababisha eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha, ngozi kutoka na kubadilika kwa rangi ya ngozi na kuwa nyeupe.
Mara nyingine huweza kusababisha malengemalenge kutokea pia.
Fangasi za miguu hushambulia ngozi iliyo na majimaji hivyo ni rahisi zaidi kupata mashambulizi kama ngozi ya miguu inakosa ukavu.

Mifano michache ya mambo ambayo husababisha ngozi isikauke ni kama vile kuvaa viatu vya kufunika muda mrefu na kuruhusu jasho kutoka kwenye miguu bila miguu hiyo kukauka.

Namna nyingine ni kuvaa viatu vya kujifunika mara tu baada ya kujimwagia maji miguu bila ya kuikausha.

Wengine ni watu wenye tatizo la kutoka jasho kwa wingi mwilini, kufanya kazi katika mazingira yanayolazimisha miguu kuwa kwenye kwa muda mrefu na wanaooga kwenye bafu zinazotumiwa na watu wengi kama vile shule za bweni na kambi.

Tatizo jingine ni wale wanaotembea pekupeku kwenye ardhi iliyoloana au yenye maji kwa muda mrefu na wale wanaoshirikiana kuvaa viatu au soksi.

Haya ni makundi machache ya wale wanaoweza kupata maambukizi ya maradhi haya.  Kuna wengine ambao hatuwezi kuwaweka kwenye kundi na hii inatokana na ukweli kuwa maradhi haya huweza kuambukizwa kirahisi.  Mara nyingi maradhi haya hutambulika kwa macho.  Kwa eneo ambapo maradhi haya yameshambulia na mwonekano wa ngozi unaweza kutambua ni tatizo la fangasi.


Matibabu ya maradhi haya ni rahisi.  Kinachohitajika ni ukavu wa eneo husika na baada ya hapo ni uwekaji wa dawa ambazo zinapatikana kwa wingi kwenye maduka ya dawa.       
Share:

3 comments: