Wednesday, November 30, 2016

PRESHA YA MACHO HUSABABISHA UPOFU

presha ya macho

Glaucoma au presha ya macho ni ugonjwa unaoweza kusababisha upofu usipotibiwa kwa wakati.

Tatizo hili linatokea kwenye mshipa wa fahamu ambao husafirisha taswira kutoka kwenye retina ya ubongoni kwa ajili ya kutafsiriwa.  Ubongo unapotafsiri taarifa hiyo ndipo mhusika hutambua anachokitazama.

Mshipa huo huitwa optiki

Zipo sababu nyingi zinazochangia maradhi haya ila kwa wengi ni kuongezeka kwa presha ndani ya jicho.

Presha hii hutokea baada ya kuongezeka kwa maji ya ndani ya jicho yaitwayo aqueous humour.  Maji haya ni maalumu kwa ajili ya kuuelekeza mwanga wenye taswira sehemu ya mbele ya ukuta wa nyuma wa jicho yaani retina na kusafirisha virutubisho na hewa safi kwenye chembehai zilizo ndani ya jicho.

Maji haya hutengenezwa na kutolewa jichoni kupitia mirija iliyopo kwenye ukuta wa mbele wa jicho, cornea na iris.

Mirija hii inapoziba, maji haya hujaa jichoni na kusababisha presha au shinikizo liitwalo intraocular pressure likitokea kwa muda mrefu huharibu kuta za optiki hivyo taarifa za taswira kutopelekwa kwenye ubongo kutafsiriwa.

Madhara kwenye mishipa ya optiki yakikithiri taarifa kutoka jichoni hazifiki kwenye ubongo hivyo mhusika kushindwa kuona au kutambua akionacho.

Sababu

Mara nyingi si rahisi kufahamu chanzo hasa cha presha ya jicho ingawa inaweza kuwa ni kutokana na kuziba kwa mirija inayotoa maji jichoni au matumizi ya muda mrefu ya aina fulani ya dawa.
Inaweza pia kusababishwa na kupungua kwa damu kwenye mshipa wa optiki au shinikizo la juu la damu.

Dalili

Dalili za maradhi haya hutofautiana kulingana na aina ya glaucoma.  Ile inayosababishwa na kuziba kwa mirija yakutolea maji jichoni huwa na maumivu ambayo humlazimu mgonjwa kwenda hospitali mara moja.

Kwa ujumla, maumivu makali ya macho au macho kuwa mekundu ni ishara inayohitaji kuchunguzwa.  Au ikitokea unashindwa kuona vizuri ghafla au unaona taswira zaidi ya moja na kuhisi kichefuchefu ni dalili za glaucoma.

Wengine hutapika na kuona rangi zinazofanana na upinde wa jua kuangalia eneo lisilo na kitu huku baadhi wakipoteza uwezo wa kuona vizuri.

Matibabu

Maradhi haya huweza kutibiwa kwa kupunguza presha iliyoongezeka jichoni na madhara yake.  Hii hufanywa kwa kutumia dawa za matone pamoja na za aina nyingine.

Mirija iliyozibwa hufanyiwa upasuaji mdogo kuizibua ili kuruhusu maji yaliyozidi jichoni kutoka.  Matibabu ya glaucoma huwa ni ya muda mrefu kwa sababu tatizo huendelea kuwapo kwani haliponi kabisa.

Mgonjwa wa glaucoma wa kuziba kwa mirija hupewa dawa na kufanyiwa upasuaji wa kuondoa maji yaliyoongezeka jichoni.  Upasuaji huu hufanywa kwa kutoboa sehemu ya ukuta wa mbele wa jicho.

Madhara

Kama matibabu hayatopatikana kwa wakati na kupunguza shinikizo lililopo jichoni, madhara kwenye mshipa wa optiki huongezeka ambayo huweza kusababisha mgonjwa kupoteza uwezo wa kuona.  Yakichelewa zaidi, mgonjwa anaweza kuwa kipofu.

Upofu utokanao na glaucoma hautibiki hivyo mgonjwa hupata ulemavu wa kudumu kwa maisha yake yote yaliyobaki.

Namna pekee ya kujikinga na madhara ya tatizo hili ni kwa kuligundua mapema kwa kufanya vipimo vya macho na uwezo wa kuona mara kwa mara ili kuepuka upofu wa kudumu.

Waliohatarini

Makundi mbalimbali ya watu wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu, mafano wazee wenye umri zaidi ya miaka 50 wapo kwenye hatari ya kupata maradhi haya kwakuwa uwezekano huo huongezeka kadri umri unavyosogea.

Wenye ngozi nyeusi pia.  Tafiti zinaonesha Waafrika au watu weusi wapo katika hatari ya kupata maradhi haya kuliko watu wenye ngozi nyeupe.

Wenye historia ya maradhi ya macho mara kwa mara au waliowahi kujeruhiwa jicho wana hatari ya kupata maradhi haya pia.

Kwa kuwa maradhi haya hurithika, watoto toka familia zenye historia hii wapo kwenye hatari hiyo pia tofauti na aliyetoka kwenye familia isiyo na historia ya maradhi haya.

Maradhi ya muda mrefu yanayoathiri mfumo mfano shinikizo la damu na kisukari huongeza hatari hiyo kutokana na uwezekano wa kuongezeka kwa shinikizo la macho.

Zipo aina kadhaa za maradhi haya kulingana na sababu zake kama zinavyoainishwa kwenye makala haya.

Kuziba kwa mirija

Ipo glaucoma ambayo hutokea baada ya mirija ya aqueous humour kuziba hivyo kuongeza presha ndani ya jicho na kusababisha maumivu makali na kichefuchefu kwa mhusika.

Kama unahisi dalili za kushindwa kuona vizuri kunakoambatana na kuumwa kichwa na kusikia kichefuchefu nenda hospitali ili wataalamu wa macho waangalie kama chanzo ni kuziba kwa mirija ili kuokoa uwezo wa jicho kuendelea kuona.

Kutoziba kwa mirija

Aina hii ya maradhi ya glaucoma hutokana na sababu nyingine lakini siyo kuziba kwa mirija maalumu inayotoa aqueous humour jichoni.  Aina ni ngumu kuitambua na hutokea kwa watu wengi zaidi.

Kutoona vizuri kwa wenye aina hii ya glaucoma huanza taratibu na mara nyingi huwa vigumu kwa mwenye tatizo kujitambua.  Wengi hupoteza uwezo wa kuona kwani dalili zake huonekana baada ya mshipa wa optiki kuathirika.

Kuzaliwa nayo

Wapo wanaozaliwa na maradhi haya.  Hii hutokana na upungufu kwenye mirija ya kutolea aqueous humour hivyo kujaa na kusababisha madhara haya.

Watoto wanaozaliwa na tatizo hili huwa na macho yaliyojaa matongotongo au ukungu.  Wakati mwingine macho yao hutoa machozi kuliko kawaida na kushindwa kuangalia kwenye mwanga.
Mara nyingi, aina hii hurithishwa hivyo hutokea kwenye familia zenye historia ya maradhi haya.

Matatizo mengine ya afya

Presha ya macho pia huweza kusababishwa na maradhi mengine ya afya mfano ajali iliyohusisha macho au dawa za kutibu maradhi mengine ya mwili.  Inaweza kuwa saratani ya jicho, mtoto wa jicho au upasuaji wa jicho ambao haukufanyika vizuri.

Wakati mwingine maradhi haya hayasababishwi na madhara ya kuongezeka kwa presha ndani ya jicho ingawa hutokea kwa watu wachache.

Sababu za kutokea ugonjwa huu bila kuhusisha ongezeko la presha jichoni bado hazifahamiki.  Tafiti chache zilizofanyika zinaonesha zinabainisha upungufu wa damu kwenye mshipa wa optiki unaoua chembehai zinazokosa virutubisho na hewa safi.  


Share:

No comments:

Post a Comment