Monday, November 21, 2016

KUEPUKA MADHARA YA JINO KUTOBOKA


Miongoni mwa matatizo ya kinywa yanayowasumbua watu wengi ni hali ya jino kutengeneza tundu kutokana na asidi au tindikali inayozalishwa na bacteria iliyomo kwenye vyakula vyenye sukari.

Kutoboka kwa meno mara nyingi husababishwa na utando wa asidi au tindikali izalishwayo na bacteria waliomo kwenye utando mlaini ambao hutoboa jino husika kuanzia kwenye tabaka la nje la jino na kuingia ndani.

Tatizo hili lisipozibwa mapema huenda likasababisha kung’olewa kwa jino husika ikiwa ni njia ya kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza endapo litaendelea kuwepo kwa mhusika.

Sababu

Licha ya uimara wake, meno yanaoza.  Ikumbukwe kutumia sukari mara kwa mara ni tishio kwa meno.  Siyo vyakula vyenye sukari pekee hata vya wanga navyo ni hatari kwani vinaposagwa hutengeneza sukari ambayo nayo huchangia kuozesha meno.  Hivyo basi kutumia vyakula na vinywaji vyenye sukari kwa wingi kati ya mlo mmoja na mwingine huongeza uwezekano wa kutoboka kwa meno kwani hushambuliwa muda wote na kukosa wasaa wa kupumzika.  Hivyo ni muhimu kujiepusha na matumizi ya vyakula na vinywaji vya sukari kwa siku nzima ili kuimarisha meno.

Meno hutoboka wakati sukari iliyopo kwenye chakula inapotumiwa na bacteria walioko kwenye kinywa ambao baadaye hutengeneza tindikali inayoozesha meno na kuyatoboa.  Kila mara unapokunywa au unapokula ama unapokunywa vitu vilivyo na sukari kwa wingi, tindikali hii huyashambulia meno na kuyatoboa.

Mara nyingi tindikali hii huweza kupunguzwa nguvu na madini ya chumvi yaliyomo kwenye mate ingawa na mashambulizi haya huweza kuchukua hata saa moja baada ya kula vitu vya sukari.

Zipo dalili za maradhi haya ambayo kwa kawaida yakiwa kwenye hatua za awali jino husika huweza kuwa na alama nyeupe kama ya chaki kwenye eneo linalotaka kutoboka.  Alama hii huonwa na daktari wa meno anapopiga mionzi jino husika.  Weupe huu huwa hauna tatizo lolote kwa mhusika mpaka pale tundu litakapojitokeza ambalo nalo huchukua muda kabla halijaanza kuleta madhara yake.

Mgonjwa huanza kujisikia tofauti mara tu tundu lililoko kwenye jino linapofika sehemu ya kati ya jino.  Jino huanza kuwa na maumivu hasa mhusika anapotumia ama vitu vya baridi au moto, au vya sukari au tindikali.

Tiba inahitajika mara tu mgonjwa anapoanza kusikia maumivu ya jino ambayo ni dalili kwamba kuna tatizo.  Kama usipozingatia madhara yatakua makubwa na inawezekana ukapoteza jino husika ambalo lingeweza kuokolewa kama ungewahi.

Licha ya kuokoa jino husika, likiachwa kwa muda mrefu, jino bovu linaweza likachangia maambukizi mengine na kusababisha ugonjwa au magonjwa mengine ambayo yangeweza kuepukika.

Tahadhari na Tiba

Sehemu yoyote na jino huweza kutoboka ingawa maeneo ya kutafunia na kati ya jino na jino ndiyo yaliyo kwenye hatari zaidi kutoboka hii ni kwa sababu mabaki ya vyakula na utando mlaini (plaque) hujishikiza humo.

Matibabu ya jino lililotoboka hutegemea hali yake wakati daktari anapoliona na kulichunguza kitaalamu kisha kushauriana na mgonjwa husika au mzazi endapo ni mtoto.  Katika hatua za mwanzoni kabisa daktari huweza kuliziba jino lililoanza kutoboka kwa kuweka dawa maalumu iitwayo fluoride varnish ili kulisaidia kurudisha madini yaliyopotea.

Kwenye hatua hii, ni muhimu kufuata ushauri na mapendekezo ya daktari wa kinywa na meno juu ya namna ya kujizuia kulingana na hali ya jino husika ili kuzuia maambukizi kuenea kwenye meno mengine na kuongeza idadi ya yatakayotoboka.

Kila mmoja anaweza kuzuia meno kutoboka.  Njia bora kabisa na rahisi ni kwa kupiga mswaki usiku kabla ya kulala na kila baada ya kula kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya floridi.

Inapaswa kuhakikisha maeneo yote ya jino yanasafishwa wakati wa kupiga mswaki na hakuna uchafu wa aina yoyote unaachwa.  

Inapendekezwa kufanya flosi ili kuzisafisha sehemu finyu zilizopo kati ya meno.  Hizi ni sehemu ambazo mswaki wa kawaida hauwezi kufika.

Licha ya kusafisha kwa umakini na kujiridhisha ipo haja ya kumuona daktari wa meno na kinywa kwa ushauri zaidi.  

Inashauriwa kumuona daktari wa meno na kinywa walau mara mbili kwa mwaka.

Kila ufanyavyo hivyo mtaalamu huyu atakupa ushauri ambao unapaswa kuuzingatia ili kujihakikishia afya imara ya meno na kinywa chako kwa muda wote.

Kutofanya hivi ni hatari kwani unaweza kujitengezea mazingira ya kupoteza meno hivyo kuongeza uwezekano wa kuwa kibogoyo ingawa unaweza kutumia meno bandia kama unaweza kuyamudu.

Endapo utalazimika kung’oa jino lililotoboka ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza, huenda ukapoteza mvuto na kuondoa furaha yako baada ya kujiamini kwako kupungua.

Inapohitajika kung’oa jino bovu, unashauriwa kufanya hivyo hospitali walipo wataalamu wa meno badala ya kuliondoa kienyeji kwani kosa dogo lolote unaloweza kulifanya madhara yake yanaweza kuwa makubwa ambayo yatakugharimu muda na fedha.
Share:

No comments:

Post a Comment