Wednesday, November 16, 2016

KUHARIBIKA KWA MISHIPA YA DAMU MWILINI

matatizo katika mishipa ya damu

Tatizo la mishipa ya damu ambalo linajulikana kama atherosclerosis ni hali inayosababishwa na uwepo wa mafuta mabaya kwa wingi katika mzunguko wa damu na kujirundika katika kuta za mishipa ya damu inayobeba damu safi yaani arteries.
Kiswahili mafuta haya hujulikana kama lehemu.  Kwa kawaida kuna lehemu mbaya na nzuri.

Mafuta haya yanapokuwa katika mzunguko wa damu kwa wingi hurundikana na kuganda, baadaye hutengeza vichuguu ambavyo hupunguza kipenyo cha mishipa hiyo.

Hali inayoifanya mishipa hiyo iwe myembamba au huweza kuziba kabisa na kusababisha damu kushindwa kupita katika mishipa hiyo.  Mishipa mikubwa mpaka ya wastani ndiyo inaathiriwa zaidi na tatizo hili.


Mishipa kuwa myembamba na kuziba ndiyo chanzo cha magonjwa mbalimbali ikiwamo magonjwa ya moyo kama vile shinikizo la damu na maumivu ya kifua.

Magonjwa mengine ni pamoja na kiharusi, matatizo ya mzunguko wa damu katika miguu na mikono.

Moyo kama ilivyo kwa tishu zingine za mwili huitaji lishe (damu) kupitia mishipa iliyopo hapo ili misuli ya moyo kuweza kufanya kazi yake ya kusukuma damu.

Inapotokea uharibifu wa mishipa hii ikiwamo ile  ya moyo huweza kusababisha tishu za moyo kukosa lishe na hivyo kuharibika na kushindwa kufanya kazi yake ya kusukuma damu.

Kwa kawaida mishipa ya damu yenye afya njema huweza kunepa yaani uwezo wa kutanuka na kuongezeka ukubwa wa kipenyo chake hivyo damu kupita kwa urahisi hata pale inapohitajika ghafla na kwa wingi.  Lakini jambo hili huwa ni vigumu kwa mishipa ya damu iliyopata tatizo hili kwani inakuwa imesinyaa au kukakamaa na kuwa migumu.

Chanzo cha uharibifu wa mishipa hii ni yale mambo ambayo yanaweza kuepukwa, lakini kutokana na mienendo na mitindo mibaya ya maisha ndipo tunajikuta tunatenda mambo hayo hatarishi.

Watu ambao wako katika hatari ya kupata tatizo ni pamoja na wenye wingi wa mafuta (lehemu) mwilini mwao, unene uliopitiliza, kuwa na chembe za urithi zenye dosari.

Mambo mengine ni pamoja na ulaji wa vyakula vyenye lehemu kwa wingi, watumiaji wa tumbaku, unywaji wa pombe, kutofanya mazoezi au kazi za kuushughulisha mwili na ugonjwa wa kisukari aina ya pili.

Dalili za tatizo hili zinaweza kutofautiana kati ya mwanaume na mwanamke, mara nyingi dalili ya kupata maumivu ya kifua ipo zaidi kwa mwanaume.

Wakati hali pumzi kukata (kupumua kwa shida), kichefu chefu na uchovu mkali ni dalili zinazoonekana zaidi kwa wanawake.  Dalili zingine za jumla ni pamoja na kupumua kwa shida, maumivu katika kifua, shingo, taya, chembe ya moyo na mgongo.

Endapo uharibifu wa mishipa hiyo utatokea eneo la mikononi na miguuni dalili zake ni pamoja na kuhisi maumivu, ganzi, baridi na kukosa nguvu.

Tatizo hili limejitokeza katika ubongo dalili za kiharusi cha muda mfupi huweza kuonekana ikiwamo udhaifu, ganzi na kupooza eneo la uso au mguu, na mkono upande mmoja wa mwili.

Kushindwa kuzungumza, kutambua, kushindwa kuona jicho moja au yote mawili, kizunguzungu na kushindwa kutembea.

Ni vigumu kujitambua mapema kama mtu ana tatizo la uharibifu wa mishipa hii mpaka pale mtu anapopata dalili na viashiria vya magonjwa ya moyo na kiharusi.
Share:

2 comments:

  1. Na tatizo la mishipa ya paja sasa ni miez miwili na nusu..chanzo cha tatizo hili ni sindano, ambapo mguu umekufa ganz msaada tafadhal

    ReplyDelete
  2. Je kuna tiba yeyote inayotolewa hosptalin kwa tatizo hilo?

    ReplyDelete