Mjamzito mwenye msongo wa mawazo anaweza akapoteza kiumbe
chake. Ndiyo, ujauzito unaweza
kuharibika kutokana na mawazo mazito ya mama mwenye nao.
Licha ya ukweli kwamba ni ngumu kuishi pasi na mawazo lakini
yakipitiliza ni hatari kwa mustakabali wa mama mjamzito. Watafiti wa sayansi ya tiba wanalihusisha
suala hilo pia na ulemavu wanaozaliwa nao watoto toka kwa aliyekuwa na msongo
wa mawazo muda mwingi wa ujauzito wake.
Utafiti ulioongozwa na Dk Dorthe Hansen na matokeo yake
kuchapishwa kwenye Jarida la The Lancet Medical ulijikita kuchunguza na
kuthibitisha ukweli wa dhana hiyo.
Watafiti hao walitumia taarifa mbalimbali za kitabibu
zilizohifadhiwa kipindi cha miaka 12 kati ya mwaka 1980 mpaka mwaka 1992 kutoka
masjala ya kitabibu. Watafiti hao
waliweza kuwatambua wajawazito waliokumbwa na changamoto za kimaisha wakati wa
ujauzito hata miezi 16 kabla ya kupata ujauzito.
Matatizo makubwa ya kimaisha yaliyochunguzwa ni pamoja na
msiba wa ndugu, jamaa au rafiki wa karibu, kulazwa kwa mara ya kwanza baada ya
kugundulika na saratani ya aina yeyote na ndugu au jamaa wa karibu kupatwa na
mshtuko wa moyo.
Mambo haya yalichunguzwa kwa kigezo kuwa, mjamzito yeyote
aliyewahi kukumbana nayo ana hatari ya kupata msongo wa mawazo bila kujali
tabia yake, kama hana watu wa kumfariji au uwezo wa kukabiliana na hali hiyo.
Watafiti hao wa magonjwa walibaini kuwa msongo mkali wa
mawazo wakati wa ujauzito unaweza kusababisha hitilafu kwenye uumbaji hatimaye
mtoto kuzaliwa akiwa mlemavu.
Ripoti yao inazidi kuthibitisha matokeo ya tafiti zilizopita
kuwa mama mwenye msongo wa mawazo wakati wa ujauzito kutokana na kuachishwa
kazi, kutengana na mwenza wake au kufiwa, au sababu nyingine yoyote ana hatari
ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu.
Miongoni mwa ulemavu unaoweza kujitokeza kwa mtoto husika ni
midomo sungura au matatizo kwenye uti wa mgongo.
Kwenye utafiti wao, jopo hilo lilichunguza maendeleo ya
mimba kutoka kwa wajawazito wenye msongo uliotokana na sababu zilizobainishwa
na wale ambao hawakukutwa na jambo lolote linaloweza kuwapa msongo.
Wajawazito 3,560 ambao walikumbana na matukio yasababishayo
mawazo mazito walihusishwa sambamba na wengine 20,299 ambao maisha yao
yaliendelea bila kikwazo chochote kinachoweza kusababisha msongo.
Matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa ulemavu na hitilafu za
viungo kwa watoto waliozaliwa ulikuwa mara mbili miongoni mwa kundi la
wajawazito ambao hawakuwa na hali hiyo kwa kipindi chote cha ujauzito wao.
Utofauti mwingine ulijitokeza kwa wanawake waliokumbwa na
msongo wa mawazo mara nyingi zaidi. Wale waliowahi kukumbwa na hali hiyo kwenye mimba ya mbili
zilizotangulia, mfululizo, walikuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuzaa watoto
wenye ulemavu wa viungo tofauti na wale waliowahi kupatwa na hali hiyo mara
moja au wale ambao hawakupata.
Tukio lingine lililoongeza uwezekano wa kuzaliwa mtoto
mwenye ulemavu wa viungo mjamzito kufiwa na mtoto wake mkubwa ndani ya miezi
mitatu ya mwanzo wa ujauzito alionao.
Hatari ya kuzaa mtoto mlemavu iliongezeka iwapo kifo cha
mtoto mkubwa kingetokea bila kutarajiwa kwa mfano kwa ajali au janga jingine
lolote pasipo kuugua kwa muda mrefu.
Watafiti wanakwenda mbali zaidi na kueleza kuwa msongo mkali
wa mawazo huchangia kuathiri uumbaji wa mtoto aliye tumboni kwa kusisimua
uzalishaji wa kichochezi cha cortisone ambacho
huongeza kiwango cha sukari kwenye damu na kupunguza oksijeni.
Kuongezeka kwa sukari kwenye damu na kupungua kwa hewa safi
inayosambazwa na kumfikia mtoto aliye tumboni husababisha kutokea kwa hitilafu
ya uumbaji wa viungo vyake hatimaye ulemavu wa viungo atakapozaliwa.
Msongo wa mawazo, kwa mujibu wa utafiti huo, imebainika
kumuongezea mjamzito uwezekano wa kutumia vileo au uvutaji sigara na lishe duni
kutokana na kupoteza hamu ya kula, hivyo huongeza madhara kwa kiumbe kilichopo
tumboni.
Hata hivyo, Profesa Peter Heper wa Chuo Kikuu cha Queen’s
cha Belfast, anasema hakushangazwa na matokeo ya utafiti huo.
“tunafahamu msongo wa mawazo husababisha mabadiliko hasa
fiziolojia kwenye mfumo wa mwili wa mjamzito hivyo hakuna kitakachozuia
yasimfikie mtoto aliye tumboni kupitia kondo la nyuma na kumwathiri,” anasema.
Matokeo haya yanathibitisha dhana ya muda mrefu kuhusu
madhara ya uumbaji wa viungo vya mtoto kwa mjamzito mwenye msongo wa mawazo kwa
muda mrefu.
Kutokana na ukweli huo, ipo haja ya namna ya kuwasaidia
wajawazito kuondokana na hali hiyo ili waweze kujifungua watoto wenye afya
njema na salama.
Hilo lisipofanyika jamii nzima italazimika kutumia
rasilimali nyingi kwa ajili ya kuwatunza watoto watakaozaliwa kutimiza mahitaji
yao kwa kuanzisha vituo vya kuwalelea au kujenga shule nyingi zaidi kwa ajili
yao na kuongeza idadi ya wataalamu kwa ajili yao.
Dk pamela Daniel, mtaalamu wa tiba za watoto anaeleza, ili
kufanikisha vita ya kukabiliana na msongo, pamoja na jitihada nyingine, ni
vizuri mjamzito awahi kupata huduma za afya kwenye hospitali za uhakika ili
apewe ushauri nasaha utakaomsaidia kuokoa afya ya mwanaye mtarajiwa na uhakika wa kujifungua salama.
Anafafanua njia nyingine ya kukabiliana na
msongo wa mawazo ni pamoja na kuwa muwazi kwa watu wa karibu ambao kwa namna
moja wanaweza kumpa ushauri na kumtuliza kiakili kwa kipindi chote kilichobaki
cha ujauzito wake.
No comments:
Post a Comment