Tuesday, January 10, 2017

DALILI ZA UGONJWA WA ZIKA NA JINSI YA KUJIKINGA UNAVYOAMBUKIZA

ugonjwa wa zika


Ugonjwa wa zika unasababishwa na virusi vinavyoitwa zika ambavyo huenezwa na mbu wajulikanao kama Aedes.

Kwa mara ya kwanza ugonjwa huu uligundulika kwa nyani nchini Uganda mwaka 1947, wakati wa kutafiti ugonjwa wa homa ya njano.

Si jambo la kushangaza kwa ugonjwa huu kugundulika hapa nchini kwani baada ya kugundulika kuwapata nyani, baadae mwaka 1952 ugonjwa huu uligundulika kuwapata binadamu nchini Tanzania na Uganda.

Mwaka juzi ugonjwa huu ulianza kuwa gumzo tena, baada ya taarifa za kitabibu kuonesha kuwa kuna wagonjwa wenye maambukizi nchini Brazil.

Mara nyingi mbu anayeeneza virusi vya zika huwa na kawaida ya kuwauma wanadamu nyakati za asubuhi, mwishoni mwa mchana na jioni.  Kama ilivyo kwa magonjwa ya malaria, njano, dengue na chikungunya yanayoenezwa na mbu ambazo ni homa, kutokwa vipele, macho kuwa mekundu yenye machozi, uchovu, kichwa kuuma, maumivu ya misuli na maungio.

Bado kitaalamu haijulikani muda wa kupata maambukizi mpaka kuibuka kwa dalili.  Kwa kawaida dalili na viashiria huweza kudumu kwa siku 2-7.

Ugonjwa huu si mkali unapompata mtu, mwili wenyewe unaweza kukabiliana nao kwa kutumia mfumo wa kinga ya mwili.

Ugonjwa huu umekuwa ukijadiliwa maeneo mbalimbali duniani na kila kukicha wanasayansi wanaendelea kuufanyia utafiti.

Taarifa mpya zinaeleza kuwa ugonjwa huu unahusishwa na kuzaliwa kwa watoto wenye hitilafu au maumbile yasiyo timilifu.

Hitilafu ya kuzaliwa inayojulikana ni ile ya mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo, kitabibu hujulikana kama "microcephally".

Vilevile maambukizi ya zika yanahusishwa katika kuchochea kutokea kwa ugonjwa unaoathiri mfumo wa fahamu ambao husababisha udhaifu na kupooza kwa viungo vya mwili (miguuni), tatizo hili hujulikana kitabibu kama "Guillain-Barre syndrome".

Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa pia kwa njia ya kujamiiana, kwa kuongezewa damu bado tafiti zinaendelea kuthibitishwa.

Utambuzi wa ugonjwa huu hujikita zaidi kwa kuangalia dalili na viashiria vya ugonjwa pamoja na historia ya kusafiri au kutembelea maeneo yenye mlipuko wa ugonjwa wa zika.

Uwepo wa maambukizi ya ugonjwa huu unaweza kuthibitishwa kwa kutumia vipimo vya maabara kwa kupima sampuli ya damu au majimaji mengine ya mwilini ikiwamo mkojo, mate na majimaji ya sehemu za siri.

Kama nilivyoeleza hapo awali, maambukizi ya zika hayasababishi kuumwa sana bali huwa ni kawaida na hakuna matibabu maalumu ya kuangamiza virusi hivyo.

Mgonjwa hushauriwa kupumzika sana, kunywa maji mengi au vyakula vyenye majimaji ikiwamo juisi za matunda.  Dawa za matibabu zinazotolewa ni zile za kuondoa maumivu ya mwili na homa tu.

Inapotokea dalili zimekuwa mbaya zaidi mgonjwa apelekwe haraka katika huduma za afya kwa uangalizi wa kitabibu.  Mpaka dakika hii hakuna chanjo ya zika ingawa tafiti zinaendelea kusaka chanjo.

Mbinu za Kujikinga

Mbinu za kujikinga na ugonjwa huu ni kama zile za kuzuia maambukizi ya homa ya malaria.

Njia hizi ni pamoja na kuvaa mavazi yanayokinga mwili kuumwa na mbu, kuishi katika nyumba yenye madirisha yenye wavu wa kuzuia mbu kupenya na kufunga madirisha na milango ya nyumba. Watu walale ndani ya chandarua kilichowekwa dawa maalumu ya kufukuza mbu kiambata dawa kiitwacho DEET, IR 3535 au Icaridin.  Wazazi au walezi watoe msaada wa kuwakinga watoto na wazee au wagonjwa ambao hawawezi kujikinga wenyewe. Tahadhali za mapema zichukuliwe kwa wasafiri au watalii wanaotembelea maeneo yenye mlipuko wa zika.

Vilevile ni muhimu sana kuangamiza maeneo yanayochangia mazalia ya mbu ikiwamo kuondoa maji yanayotuama na vitu vinavyobeba maji kutuama ikiwamo vipande vya vyombo, vifuu na matairi.

Jamii inatakiwa kushirikiana na serikali za mtaani katika maeneo yao kwa kuweka mazingira yao wanayoishi ikiwamo kupulizia dawa za kuua mbu na kukata nyasi zinazozunguka maeneo wanayoishi.  Ikumbukwe kuwa pale unapokabiliana na ugonjwa wa zika vilevile inakusaidia pia kukabiliana na magonjwa mengine ikiwamo homa ya dengue, chikungunya na njano pamoja na malaria. 
Share:

No comments:

Post a Comment