Wednesday, January 11, 2017

DAMU KUGANDA KWENYE MISHIPA


Umeamka ghafla unajikuta ukiwa na maumivu makali ya mguu yasiyovumilika, unapovuta kumbukumbu unabaini kuwa haukupata ajali yoyote na wala hakuna jeraha lolote katika mguu huo.

Kama rangi ya mwili ni nyeupe au maji ya kunde unaweza kuona kubadilika rangi ya mguu na kuwa nyekundu, unapogusa eneo hilo huwa na joto zaidi ukilinganisha na maeneo mengine ya mwili.

Kitabibu hali kama hii ni ishara ya uwepo wa tatizo la donge la damu lililoganda na kuziba mishipa ya damu inayorudisha damu chafu yaani ile yenye hewa ya kabonidayoksaidi.

Mishipa hiyo huitwa vein na tatizo hilo hujulikana kama deep vein thrombosis (DVT).  Tatizo linalotokea zaidi katika mishipa ya damu iliyopo miguuni katika kina cha tishu za miguu.

Tatizo hili ni hatari kwani donge la damu iliyoganda katika mshipa inawewza kukwanyuka na kusafiri katika mzunguko wa damu na kwenda maeneo mengine mwilini ikiwamo mapafu na kuziba mishipa ya damu.  Hali inapotokea huleta matokeo mabaya ikiwamo uharibifu wa ogani na kusababisha kifo cha ghafla.

Tatizo hili huwa halitoi dalili ya kuonywa kwa nusu ya wagonjwa wenye nalo, dalili hujitokeza ghafla tu.  Mara nyingi kuvimba kwa mguu katika eneo la chini ya goti ndiyo dalili ya awali.

Mtu mweupe anaweza kubadilika rangi na kuwa mwekundu katika eneo lilipojitokeza tatizo na kuambatana na maumivu makali.

Eneo hilo linapotomaswa husababisha maumivu makali.  Ingawa si mara zote wagonjwa wanapata dalili na viashiria vyote.

Pale inapotokea damu iliyoganda ikakwanyuka katika mshipa ulioathirika na kuzunguka katika mzunguko wa damu na kwenda kuziba katika mtawanyo wa damu katika mapafu madhara makubwa hutokea.  Hali hii hujulikana kitabibu kama Pulmonary Embolism.

Hali hii husababisha kupumua kwa shida, msukumo wa damu kushuka, kupoteza fahamu, mapigo ya moyo kuwa ya kasi, maumivu makali ya kifua na kukohoa damu.

Tatizo hili ni la dharura, mgonjwa akicheleweshwa kufikishwa katika huduma za afya huweza kupoteza maisha.  Hivyo, ni muhimu sana kuomba msaada wa huduma za dharura au mgonjwa afikishwe haraka katika huduma za afya.

Kitu chochote ambacho kitadhuru sehemu ya ndani ya kuta au tando za mishipa ya damu ya vein inaweza kuleta tatizo hili, DVT.

Vitu hivyo ni pamoja na tiba ya upasuaji majeraha au kinga ya mwili ikishambulia kuta za mishipa ya vein.

Kwa mtu ambaye damu yake ni nzito au inayotiririka taratibu yupo kwenye hatari ya kutengeneza damu iliyoganda hasa kwa mishipa ya vein iliyojeruhiwa.

Watu ambao wana aina fulani ya hitilafu za chembe za urithi (vinasaba) au wenye kiasi kikubwa cha kichochezi cha estrogen nao wapo katika hatari ya kupata tatizo hili.

Makundi mengine walio katika hatari ya kupata tatizo hili ni pamoja na watu wenye umri mkubwa, wanene, wanaosafiri na kukaa muda mrefu ikiwamo wasafiri wa ndege, waliofanyiwa upasuaji, wanaolala na kukunja goti, wavutaji sigara na wanaougua saratani.

Share:

1 comment: