Tuesday, February 14, 2017

MALARIA SUGU

ugonjwa wa malaria sugu

Ugonjwa wa malaria unasababishwa na kijidudu kinachoitwa plasmodium parasite ambaye huenezwa na mbu.  Ugonjwa huu mara nyingi huenezwa na mbu usiku wa manane pindi watu wanapokuwa wamelala au hata kipindi cha jioni wakati watu wanapokuwa wamekaa katika maeneo ya wazi yenye wadudu hawa kama vile vibarazani, uwani au hata sebuleni.

Takwimu zinaonesha kuwa malaria ni tatizo kubwa kwenye mabara ya Asia, Afrika na America ya Kusini katika jumla ya mataifa 100 ambayo ni sawa na 40% ya idadi ya watu ulimwenguni.

Lakini pamoja na hayo, madhara ya ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa yanaonekana katika Bara la Afrika ambapo kuna idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na tatizo hilo hususani kwa wanawake wenye ujauzito na watoto wadogo.

Pamoja na jitihada zinazofanywa na wanaharakati mbalimbali katika kupambana na malaria, bado tatizo lipo na linaendelea kusababisha vifo vingi pamoja na ukweli kuwa Malaria inatibika.  Kingine ni kuwa rahisi kujikinga na malaria ikiwa masharti yatafuatwa kwa uaminifu.

Kama yalivyo maradhi mengine, ugonjwa huu una dalili zake kuu: kuhisi homa, kutokwa jasho na viungo kuuma.  Ishara hizo zimegawanyika katika hatua tatu na hivyo wakati mwingine ni vigumu kugundua haraka kuwa umekumbwa na tatizo hilo.

Hatua tatu za malaria sugu hujulikana kama hatua ya baridi, hatua ya joto na hatua ya kutokwa jasho jingi.  Kila hatua ina dalili zake na madhara kwa mgonjwa endapo hatapatiwa matibabu mapema.  Zifuatazo ni hatua za malaria sugu na dalili zake:

Hatua ya baridi

Katika hatua hii ya malaria sugu mgonjwa anaweza kuanza kuhisi maumivu ya kichwa, kutetemeka mwili na kuhisi baridi wakati wote.

Hatua ya joto

Mgonjwa anapokumbwa na hatua hii huanza kujihisi homa kali, kutapika, maumivu ya viungo, kuweweseka, kupoteza fahamu, kichefuchefu na kuhisi kuchanganyikiwa kiakili.

Hatua ya kutokwa jasho

Katika hatua hii ya malaria sugu mgonjwa hutokwa na jasho jingi mwilini na kiwango cha jotoridi huongezeka.  Zingatia kwamba katika hatua zote hizi, mgonjwa hupatwa na malaria inayojirudia kila wakati kama homa ya vipindi.

Soma pia DALILI ZA JUMLA KWA MALARIA SUGU
Share:

No comments:

Post a Comment