Monday, February 20, 2017

POMBE KALI HAZIPUNGUZI MAFUTA MWILINI


unywaji wa pombe kali


Ulaji wa mlo wenye mchanganyiko wa vyakula vya aina tofauti ni msingi wa afya njema na huwa na ufanisi zaidi endapo utafanya mazoezi na kuepuka matumizi ya sigara kwa afya ya moyo.
Wapo baadhi ya watu ambao hawafahamu kama pombe siyo rafiki wa moyo.  Baadhi hudhani kuwa kunywa pombe kali kunakata mafuta ya mwili na kuamini wakifanya hivyo wanaepuka magonjwa ya moyo.
Zipo tafiti zinazoonesha unywaji wa glasi moja ya mvinyo mwekundu kwa siku huimarisha afya na moyo.  Ingawa bado sishauri moja kwa moja mtu kunywa mvinyo kama hatua ya kujikinga.
Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kusababisha kupanda kwa msukumo wa damu, kuongeza kiwango cha mafuta katika damu na kuufanya moyo ushindwe kufanya kazi vizuri.
Wengi hunywa pombe kama sehemu ya burudani hivyo kuwa ngumu kwao kuepuka tabia hiyo.
Pale mtu anaposhindwa kuacha kunywa pombe basi ni vizuri akahakikisha anazingatia utaratibu na kunywa kwa kutozidisha glasi moja kwa siku kwa mwanamke na glasi mbili kwa siku kwa mwanaume.
Ieleweke pia, pombe kali ambazo zina kiasi kikubwa cha kilevi zikitumika kupita kiasi zinachangia zaidi kuharibika kwa mishipa ya damu ikiwamo ya moyo.  Nashauri kwa mtu ambaye hajawahi kunywa pmbe ni vizuri asijaribu kuanza kutumia.
Kutokunywa pombe ni njia ya asili ya kukabiliana na magonjwa yanayodhorotesha afya ya moyo ikiwamo msukumo wa damu, kupanda kwa kiwango cha lehemu na kisukari.
Mgonjwa mwenye matatizo haya anatakiwa kushikamana na matibabu na ushauri kwani magonjwa haya yanaongoza kwa kuharibu mishipa ya damu.
Ni vizuri kuwa na vifaa tiba nyumbani ikiwamo cha kupima kiwango cha sukari katika damu na mashine ya kupima shinikizo la damu.
Vipimo hivi vinakuwezesha kujua endapo matatizo haya yanazidi au yanapungua hivyo kukusaidia kuwahi kufika katika huduma za afya au kumjulisha daktaria wako mapema kwa ajili ya matibabu na ushauri.
Mgonjwa anashauriwa kukabiliana na shinikizo la akili ambalo husababisha mabadiliko hasi ya hisia pamoja na kupanda kwa mapigo ya moyo na vijeraha katika kuta za mishipa ya damu.
Mtu mwenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo hujikuta akijitumbukiza kwenye ulevi wa pombe, uvutaji sigara na dawa za kulevya.  Wengi hudhani kuwa mambo haya yanawapunguzia msongo wa mawazo kumbe vinawaongezea hatari ya kupata matatizo ya moyo Zaidi.
Njia sahihi kiafya za kukabiliana na shinikizo la akili ni pamoja na kusikiliza muziki, kushiriki michezo, kutembea, kushiriki burudani mbalimbali, kuongea na kupata ushauri kwa ndugu, jamaa na marafiki.  Mazoezi yanashauriwa kwa waathirika wote.  Fahamu matatizo ya kiafya yanayowakumba ndugu zako wa damu, kwani baadhi ya matatizo ya moyo yanarithishwa kupitia chembe zenye hitilafu pamoja na mitindo ya kimaisha.
Kuyajua matatizo hayo inakusaidia kuchukua tahadhari mapema na kufahamu namna ya kujikinga.  Mbinu ya mwisho ni kuhakikisha unabakia katika uzito ambao ni salama kiafya.  Hakikisha unapima uzito wa mwili mara kwa mara na kuulinda.
Ili kujua kama upo katika uzito wa kawaida ni muhimu kufahamu zao la uwiano wa uzito na urefu wa mwili (Body Mass Index) na unatakiwa kuwa BMI 18.5 na h24.9.      
Share:

No comments:

Post a Comment