Tatizo hili kitabibu hujulikana kama Deep Vein Thrombosis au
kwa kifupi, DVT. Wanawake wako katika
hatari ya kupata DVT hasa wanapokuwa wajawazito na wiki ya nne mpaka ya sita
baada ya kujifungua.
Inakadiriwa, kwa kila wajawazito 1,000 mmoja anapata tatizo
hili ingawa kwa uzoefu wangu bado kwenye jamii ya Kitanzania kuna kesi chache
zaidi za DVT zinazoripotiwa.
Takwimu zinaonesha, asilimia 80 ya wajawazito wanapata
tatizo hili katika mguu wa kushoto.
Endapo halitagundulika na kutibiwa mapema, madhara hatarishi yanaweza
kujitokeza.
Mojawapo ya madhara hayo ni kukwanyuka kwa donge la damu
kutoka miguuni na kusafiri katika mzunguko wa damu na kwenda kuziba katika
mishipa inayotawanya damu kwenye mapafu ambayo hujulikana kama Pulmonary
Embolism (PE).
Tatizo hili linapotokea huwa ni jambo la dharura kwani
linaweza kusababisha kifo cha ghafla kwa mjamzito husika hivyo kumpoteza mama
na mtoto endapo huduma za kumuokoa mtoto hazitatolewa kwa wakati.
Sababu kubwa inayochangia tatizo hili kwa wajawazito na
waliojifungua (wazazi) ni uwapo wa kiasi kikubwa cha kichochezi cha estrogen.
Kichochezi hiki ni moja ya kihatarishi cha kugandisha damu
kwa urahisi hasa pembezoni mwa mwili, ikiwemo miguu.
Sababu nyingine ni uwepo wa shinikizo kubwa kutoka kwa
nyumba ya uzazi inayoongezeka kadri mimba inavyokua. Hali hii husababisha utiririkaji wa damu kuwa
wa taratibu katika mishipa ya damu hasa iliyopo miguuni. Mazingira ya namna hii yanachangia kuganda kwa
damu kirahisi.
Wakati wa kujifungua, wajawazito hupoteza damu nyingi huku
uwezo wa mwili kugandisha damu huwa ni mkubwa ukilinganisha na inavyokuwa
wakati mwingine wa kawaida. Hali hii ni
moja ya sababu ya kujitokeza kwa DVT kwa wajawazito wakati wa kujifungua au
kipindi kifupi baada ya kujifungua.
Bado wanasayansi hawajui ni kwa nini wakati wa ujauzito
kiwango cha protini zinazosaidia damu kuganda kinakuwa juu wakati zile protini
zinazosaidia damu kuyeyuka zinakuwa chini.
Vilevile, mabadiliko ya jumla ya damu kipindi cha ujauzito
pamoja na matatizo mengine ya damu yanawaweka wajawazito katika hatari ya
kupata DVT.
Wajawazito wapo katika hatari ya kupata tatizo hili pamoja
na wale ambao familia zao zina historia ya kupata tatizo hilo, wenye umri zaidi
ya miaka 35 na wanene au uzito uliokithiri.
Wengine ni wavutaji wa sigara, wenye tishio la kifafa cha
mimba au shinikizo la juu la damu. Pia,
wanaopewa mapumziko ya muda mrefu kitandani, wenye magonjwa ya mishipa ya damu,
waliojifungua kwa upasuaji, waliopoteza damu nyingi au walioongezewa damu.
Habari nzuri ni kwamba tatizo hili na madhara
yake ambayo ni tishio ikiwamo la kuzibwa kwa mishipa ya damu katika mapafu (PE)
yanaweza kuzuiwa kutokea na kupatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment