Monday, February 13, 2017

VIDONDA VYA TUMBO

tatizo la vidonda vya tumbo

Miongoni mwa magonjwa yanayoshika kasi katika taifa la Tanzania ni vidonda vya tumbo ambavyo kwa kiasi kikubwa hutokana na mifumo mibaya ya maisha ya binadamu na kutozingatia aina ya vyakula sahihi kwa ajili ya kulinda afya.

Ugonjwa huu huibuka baada ya kutokea vidonda kwenye kuta za utumbo wa mwanadamu ambavyo hutokana na kuzidi kwa kiwango cha tindikali yenye kazi ya kuyeyusha chakula kiingiacho mwilini.

Endapo mgonjwa hatapatiwa tiba mapema tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi hadi kufikia kwenye mishipa ya damu hivyo hali kuwa mbaya zaidi.

Yapo mambo mengi yanayosababisha uwepo wa tatizo hili nayo ni pamoja na; msongo wa mawazo, aina ya chakula na mifumo ya maisha.  Lakini wataalam wa masuala ya afya wanaeleza kuwa chanzo kikubwa cha tatizo hili ni bacteria anayejulikana kwa jina la “Helicobacter pylori” ambaye bado hajapatiwa suluhisho la kitabibu.

Chanzo Cha Vidonda Vya Tumbo

Kwa kawaida tumbo la mwanadamu lina tabia ya kujikinga na matatizo mbalimbali ya kiafya vikiwemo vidonda vya tumbo.  Tumbo hukinga tatizo hili kwa kuzalisha ‘ute‘ ambao hufanya kazi kama kinga ya kuzuia tindikali aina ya haidrokloriki na kimeng’enyo cha aina ya pepsin kutoleta madhara mwilini.  Ikiwa uzalishaji huu hautafanikiwa ndipo vidonda vya tumbo hutokea.

Lakini sababu ya msingi kwa tatizo hili kutokea ni bacteria ‘Helicobacter pylori’ (H. pylori) ambao wana uwezo wa kuishi kwenye ukuta wa tumbo wakiwa chini ya ute unaofanya kazi kama kinga dhidi ya athari za tindikali.

Udhaifu wa mwili katika kuzalisha ute unaotumika kujikinga na madhara ya tindikali wakati wa kusaga chakula tumboni.
Matumizi ya kahawa kwa wingi husababisha uzalishaji wa tindikali kwa kiasi kikubwa.

Kumbuka

Matumizi ya pombe hayajathibitishwa moja kwa moja kuchangia upatikanaji wa vidonda vya tumbo lakini ukweli ni kwamba kilevi huchelewesha hatua za uponaji wa tatizo hili.


Msongo wa mawazo hautajwi kusababisha ugonjwa wa vidonda vya tumbo lakini unaongeza maumivu ya vidonda kwa mgonjwa hivyo ni vema kuepuka na hilo pia.

Soma pia DALILI ZA UGONJWA WA VIDONDA VYA TUMBO
Share:

No comments:

Post a Comment