Wednesday, June 21, 2017

TATIZO LA ALEJI


athari za aleji


Kwa kawaida kinga ya mwili huulinda mwili dhidi ya vitu mbalimbali vyenye kuleta athari kwa afya kama vile vimelea vya magonjwa kama vile bakteria na virusi, lakini wakati mwingine pia na vitu ambavyo havina madhara yoyote kwa mwili, ambavyo huitwa allergens (mzio).
Mtaalamu wa dawa na tiba kutoka hospitali ya Sanitas, Dk Sajjad Fazel anasema aleji au mzio (allergy) ni matokeo ya kinga ya mwili inapofanya kazi ya ziada ya kupambana na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili pale inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili.
“Kinga ya mwili inapoamua kufanya kazi ya ziada husababisha mtu kuwa na dalili za aleji au mzio katika mwili wake kwa kuona dalili mbalimbali”, alisema Dk Fazel.
Vitu vinavyosababisha mzio
Dk Fazel anasema baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio ni pamoja na vumbi, baadhi ya dawa zenye madini ya sulfer, vyakula, kung’atwa na wadudu kama vile nyuki na baadhi ya uyoga.
Anasema wapo pia watu ambao wanapatwa na mafua karibu kila siku na wengine kushindwa kuvaa aina fulani ya nguo na vitu kama saa,hereni na cheni, kwani mara nyingi husababisha kuwashwa na kuvimba mara wavivaapo.
Anasema watu wenye mzio huwa na hisia zisizo za kawaida za mwili dhidi ya vitu vinavyowaathiri na pindi mwili unapokumbana na vitu vinavyosababisha mzio, mfumo wa kinga wa mwili huzalisha kemikali mbalimbali, mfano histamine ambazo hupambana na mzio.
Mara nyingine watu hupata ugonjwa wa mzio pindi wanapokutana na aina fulani ya mazingira kama yenye vumbi, baridi ya wengine hupatwa na mzio wanapopigwa na jua kali au msuguano wa ngozi unaweza kuwasababishia dalili fulani za mzio.
Dalili zake
Dk Fazel anasema mara nyingi dalili hutegemeana na mgonjwa ana aina gani ya mzio.
Kama mtu atakuwa na mzio katika mfumo wa hewa, huweza kupata matatizo ya kupumua anapokutana na mazingira yenye vumbi, hali inayomsababishia kupiga chafya mara kadhaa, kutokwa na makamasi, kuziba pua, muwasho kwenye pua na koo au kupumua kwa kutoa sauti kama filimbi, kuumwa na kichwa mara kwa mara, kizunguzungu, pumu, kuhisi joto katika mwili na mfadhaiko.
Endapo macho yataguswa, mhusika huhisi hali ya macho kuchoma, kutiririkwa na machozi na muwasho kwenye macho na pindi anapojikuna, macho huvimba na kuwa mekundu.
“Iwapo mtu atakula kitu ambacho ana aleji au atakunywa dawa zenye sulfer na zina mzuru kila azitumiapo, anaweza kuwa na dalili kama ya kuharisha, kichefuchefu, kutapika, kusokotwa au kuumwa na tumbo na hata hali mbaya ya kutishia maisha.
Anasema vitu vinavyosababisha aleji vinapogusa ngozi ya binadamu, vinaweza kusababisha ngozi kuwa na mabaka, kubabuka, kuvimba, muwasho, kutoa vipele, malengelenge, michubuko na ngozi kuwa nyekundu.
Zipo aleji zinazohusisha mwili mzima zinaweza kuwa na mkusanyiko wa dalili zote alizozitaja na wakati mwingine mtu anaweza kuwa na aina fulani ya nguo, hivyo vyema kuziepuka ili kupunguza tatizo hili.
Maambukizi
Kwa kawaida ugonjwa wa mzio huwa ni wa kuzaliwa nao na hauambukizi ikiwa mtu katika familia ana ugonjwa huo, hawezi kumuambukiza mtu mwingine.
Jinsi ya kufanya vipimo
Anasema mara nyingi mgonjwa wa mzio hupimwa kwa kutumia damu kwa sababu katika damu inaweza kutoa majibu ya mgonjwa juu ya mzio alionao na hii ni baada ya mgonjwa kuelezea vitu gani vinavyomsababishia matatizo mara avitumiapo.
“Na hii ni kwa sababu kuna baadhi ya mambo yanayoweza kumsababishia mtu dalili zinazofanana na za mtu aliye na aleji ya kitu fulani,” anasema Dk Fazel.
Kwa mfano, matumizi ya aina fulani ya dawa yanaweza kumsababishia mtu mikwaruzo au michubuko katika ngozi inayofanana na aleji nyingine, au mtu anaweza kuwa na mafua au kikohozi kwa sababu ya maambukizi ya bakteria au virusi na si kwa sababu ya aleji.
Anasema mara nyingine wanapopima damu huangalia ongezeko la immunoglobin E ambayo huashiria uwapo wa vitu vinavyosababisha aleji na kipimo cha damu chenye kuonesha ongezeko la eosinophil iwapo kuna aleji, ambayo ni sehemu ya chembe nyeupe za damu.
Matibabu
Shambulio kali la aleji linaweza kusababisha mhusika kulazwa hospitali na lisipodhibitiwa, kifo kinaweza kutokea kutokana na kupata shida katika upumuaji wake, lakini hii hutokea mara chache kwa wagonjwa wenye mzio katika chakula na mfumo wa hewa.
Anasema tiba kubwa ni kupunguza uwezekano wa kupata aleji kwa kutambua na kuepuka kitu au vitu vinavyokusababishia hali hiyo.
“Kama ni chakula au dawa au kemikali, mgonjwa anatakiwa kuepuka kabisa matumizi yake, na kama ni vumbi ajitahidi kukaa nalo mbali”, anasema Dk Fazel
Anasema zipo pia aina mbalimbali za dawa zinazotumika kutibu na kuzuia aleji, kulingana na jinsi daktari atakavyoona inafaa kwa kuzingatia ukali wa tatizo, dalili zake azipatazo mgonjwa, umri wa mgonjwa pamoja na hali yake ya kiafya kwa ujumla.
Anasema pia wagonjwa hawa hupewa dawa maalum kwa ajili ya kutuliza mcharuko mwilini ambazo huwa katika miundo mbalimbali zikiwamo za kupaka, matone, kuvuta, sindano au vidonge.
Kwa wale wenye mafua na kuziba kwa pua, hushauriwa kutumia dawa zinazosaidia kufungua pua, hata hivyo, dawa hizi hazina budi kutumiwa kwa uangalifu hasa kwa watu wenye magonjwa ya shinikizo la damu au moyo.
Anasema wagonjwa hawa hupewa dawa pia kwa ajili ya kuzuia vitu vinavyosababisha aleji.
“Aina nyingi za aleji hutibika kwa urahisi kwa kutumia dawa.  Wapo baadhi ya watu hususan watoto wanaoweza kujenga hali ya aleji dhidi ya aina fulani za vyakula, hali wanayoweza kuendelea nayo hadi ukubwani na kwa kawaida, kitu kikimletea mtu aleji utotoni, huendelea kumuathiri daima.” Anasema Dk Fazel.
Madhara yatokanayo na mzio
Dk Fazel anasema madhara ya mzio ni pamoja na kupata shambulio kali ambalo linaweza kusababisha kifo kama matibabu hayatafanywa haraka.
Kuna baadhi ya watu ambao wakila baadhi ya vyakula huvimba mwili na kushindwa kupumua mpaka kuhitaji kulazwa hospitali na kusaidiwa kupumua kwa mashine.
Madhara mengine ni pamoja na shida ya kuvuta pumzi au kushuka kwa shinikizo la damu (kupata shock).
Namna ya kujikinga na aleji
Dk Fazel anasema kuna baadhi ya wagonjwa hupata madhara makubwa ya kuungua nje na ndani pindi wanapotumia dawa ambazo zina sulfer na huwasababishia mzio ambao usipotibiwa kwa haraka, kifo kinaweza kutokea.
“Steven Johanson’s syndrome ni mzio hatari na wa kipeke kuliko aina zote na mgonjwa anapopata aina hii ya mzio na ngozi yake huungua nje na ndani na endapo akichelewa kupewa matibabu huweza kupoteza maisha,” anasema Dk Fazel.
Jinsi mzio unavyonyima uhuru wa kufanya kazi
Evelyn Menas mkazi wa Mtoni Kijichi, anasema yeye mara nyingi hupata tatizo la mzio akikaa au kupita eneo lenye vumbi au kutokwa na jasho mwilini, mambo yanayomnyima uhuru wa kufanya kazi katika baadhi ya mazingira.
“Nikitokwa jasho mwili huwasha, najikuna, kukosa uhuru na mara nyingine ninapokuwa sehemu yenye hewa iliyo na asili ya vumbi, napiga chafya mfululizo, kuwashwa uso na macho yanavimba na huwa nashindwa kupumua vizuri kwa sababu pua zinaziba,” anasema Evelyn.
Anasema anajitahidi kuhakikisha chumba anacholala kinakuwa safi muda wote, lakini hali inakuwa ngumu akiwa katika vyombo vya usafiri kama daladala iliyojaza abiria kupita kiasi, kupita sehemu yenye harufu mbaya, au kutimuliwa vumbi barabarani.
Ushauri
Dk Fazel anasema ni vizuri watu wakazingatia na kufanya utafiti ili kuweza kugundua ni kitu gani kinawasababishia mzio au kufika katika kituo cha afya kinachotoa huduma ya vipimo waweze kufanyiwa vipimo na kupata ushauri wa kitaalamu.
Na endapo mtu atatumia dawa zenye madini ya sulfer zikamletea madhara, anatakiwa awahi kumuona daktari ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.   
Share:

No comments:

Post a Comment