Matumizi ya dawa za antibiotiki yasiyozingatia maelekezo ya
daktari hufanya vimelea kuwa sugu, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema. Tahadhali hii inatolewa baada ya shirika hilo
kuorodhesha bakteria sugu wasiotibika kwa dawa zilizopo.
Kutokana na kushamiri kwa matumizi ya dawa hizi, baadhi ya
wagonjwa wamekuwa wakizitumia bila kufuata utaratibu unaoshauriwa hivyo kuongeza usugu wa vimelea ambao ni tatizo jingine kwa afya ya binadamu.
WHO inatahadharisha, iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa,
hadi kufikia mwaka 2050, tatizo hilo linaweza kusababisha vifo vya zaidi ya
watu milioni 10 kila mwaka.
Shirika hilo linatoa wito, kila mtu kuchukua hatua ikiwamo
kuepuka matumizi ya dawa za antibiotiki kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo,
kwa sababu si kila ugonjwa anazitegemea kwa tiba, mfano mafua.
Namna sahihi ya kutumia dawa hizo, WHO inaelekeza, ni lazima
iwe kwa kufuata maelekezo ya daktari.
“haishauriwi kukatisha kutumia dawa kabla ya kupona kabisa,” linasema
shirika hilo.
Miongoni mwa tahadhali inayotolewa na WHO kuhusu dawa hizi
ni pamoja na kutozihifadhi kwa matumizi ya watu wengine.
Wataalamu wamekwenda mbele zaidi kuhusu usugu wa dawa za
antibiotiki kwamba unachangiwa na ulaji wa nyama ya mnyama aliyetibiwa kwa dawa
hizo, hivyo sekta za kilimo na mifugo zinachangia kwa kiasi kikubwa usugu wa
dawa hizo kwa binadamu.
Mganga mkuu wa Serikali, Profesa Muhammed Kambi anasema
Wizara ya Afya imeingia rasmi kwenye mapambano dhidi ya suala hilo. Anasema binadamu anaathirika zaidi na usugu
wa vimelea kutokana na kuzitumia kwa wingi kutoka kwenye mifugo kwa sababu
hutumika kuwatibu kabla hawajachinjwa na kuliwa.
Anafafanua, binadamu akinywa maziwa ya ng’ombe aliyetibiwa
kwa dawa za antibiotiki au akila nyama ya mnyama aliyetibiwa kwa dawa hizo huwa
ngumu kutibika antibiotiki kwa sababu bakteria wanakuwa wameizoea dawa na
kujipanga kupambana nayo.
“Kwa magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya hewa kutoka kwa
mgonjwa mmoja kwenda kwa mwingine, bakteria wa mgonjwa aliyepata usugu wa dawa
vikienda kwa mtu mwingine havitatibika kwa sababu vitakuwa vimehama vikiwa
sugu,” anasema Profesa Kambi.
Serikali imezindua mpango kazi wa miaka mitano kupambana na
usugu wa dawa hizo unaowahusisha wataalamu kutoka idara tofauti zikiwamo kilimo,
mifugo na afya kujadili namna Tanzania itakavyokabiliana na usugu huo. Mpango huo unatekelezwa kuanzia mwaka huu
hadi 2022.
Mganga mkuu huyo anasema Serikali itashiriki kwa kufanya
utafiti wa dawa na chanjo, kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye dawa na vifaa
tiba.
Mkuu wa Sekta ya Afya ya Ubalozi wa Uswisi, Thomas Teuscher
anasema ipo haja kwa wadau wa sekta binafsi na umma kuungana ili kukabiliana na
janga hilo kwa sababu linagusa wengi.
Anasema Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) inatakiwa kuongeza
umakini wa ukaguzi ili kuhakikisha dawa bandia haziingii nchini kwa sababu
huchangia kurudisha nyuma juhudi za kupambana na usugu huo.
Anasema kutumia dawa za antibiotiki kiholela, kutomaliza
dozi iliyopendekezwa na kutumia dawa bandia kunachangia usugu na huchukua muda
kubainika.
Dawa feki za antibiotiki zinapotumika, anasema, zinajenga
usugu wa mgonjwa anapotumia dawa halisi hawezi kupona kwa sababu hapo awali
hakutumia dawa sahihi.
“Kwa sababu wao ndiyo wana jukumu la kusimamia uhakika wa
dawa, wana nafasi kubwa kwenye mapambano haya ya matumizi sahihi ya dawa za
antibiotiki,” anasema Teuscher.
Mwakilishi wa WHO nchini, Dk Richard Banda anazitaja familia
12 za bakteria ambazo zinahitaji dawa mpya kutokana na zilizokuwapo kutokuwa na
makali yanayohitajika.
Anasema WHO imetoa orodha ya bakteria hao ili kuwapa mwanya
watafiti, Serikali na wadau wa sekta ya afya kutafuta mbadala wa dawa hizo.
Baadhi ya bakteria waliomo kwenye orodha isiyotibika kuwa ni
pamoja na waliokuwa wanatibiwa kwa dawa za mchafuko wa tumbo, maambukizi katika
njia ya mkojo na kaswende.
“Orodha hii itahamasisha na kuwashawishi watengenezaji wa
dawa kubuni aina mpya,” anasema Dk Banda.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Kilimo na
Mifugo, Dk Abdu Hayghaimo anawataka wazalishaji wa vyakula vya mifugo kutumia
vifaa vya asili kutengeneza dawa badala ya kemikali.
Pia anataka mamlaka husika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
ikiwamo kuchukua sampuli za vyakula vya mifugo kama vinakidhi viwango.
Katika kuhakikisha mpango kazi huo unaeleweka vema kabla ya
kuanza kuufanyia kazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya anasema baadhi ya malengo ya
mpango huo wa miaka mitano ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii.
Anasema wahusika watafanya utafiti wa kuangalia namna sahihi
ya kupunguza maradhi yanayosababishwa na bakteria sugu na kuelimisha kuhusu
matumizi sahihi ya dawa hizo kwa binadamu na wanyama ili kupunguza mwingiliano
unaosababisha usugu kutokana na wanyama na mimea.
“Mpango utaangalia jinsi ya kuongeza upatikanaji, utafiti wa
dawa; za zamani na mpya, upatikanaji wa vifaa tiba, chanjo na njia nyingine
mbalimbali za kukabiliana na tatizo hili,” anasema Dk Ulisubisya.
Anafafanua kuwa mpango kuelekeza maeneo ya vipaumbele na
namna ya utekelezaji. Mwaka 2000,
anasema usugu wa dawa hizo ulikuwa asilimia 20 tu nchini lakini sasa ni
asilimia 80.
Baada ya kuona ongezeko la tatizo hilo kwenye mataifa mengi,
anasema WHO imeandaa One Health, na Wizara nayo kuja na mpango utakaosaidia
kuwaunganisha wataalamu kutambua njia sahihi za kukabiliana na tatizo hilo.
“Shida tuliyonayo ni usugu ambao umeanza kuonekana kwenye
dawa nyingi kwa kasi kubwa kuliko uwezo wa wataalamu kugundua dawa nyingine
zinazoweza kutibu maradhi hayo,” anasema.
Baadhi ya athari zitakazojitokeza kutokana na usugu huu wa
dawa ni kuongezeka kwa gharama za matibabu kunakotokana na kuugua muda mrefu
au kutumia dawa ghali ili kudhibiti zilizozoeleka.
Athari nyingine ni kutumia muda mwingi kwenye matibabu hivyo
kutojishughulisha na uzalishaji mali, na kuongezeka kwa hatari ya kupoteza
maisha endapo dawa stahiki hazitopatikana.
Katibu mkuu huyo, anasema mpango huo utasaidia kuongeza
hamasa kwa watafiti na watengenezaji wa dawa kuongeza jitihada za uvumbuzi wa
dawa mpya zitakazokuwa na tija.
No comments:
Post a Comment