Elimu haina mwisho hivyo ndivyo unavyoweza ukasema baada ya
kufanyika kwa utafiti ambao umebaini kwamba runinga ina uwezo wa kumsababishia
mtoto kuwa na uzito wa mwili.
Wengi tunaamini kwamba mtoto akiwa mzito ni kutokana na
ulaji wa chakula, ila inabainishwa katika utafiti uliofanywa na wanasayansi
mjini London nchini Uingereza kwamba runinga ni moja wapo ya sababu ya
kumuongezea uzito mtoto akiwa chumbani.
Wazazi hufanya kila jitihada kuonesha mapenzi ya dhati kwa
watoto wao ili kuwaridhisha kwa wale wenye uwezo wamejitahidi kuwawekea runinga
kwenye vyumba vyao ili watulie majumbani mwao.
Mtoto anapokuwa na runinga katika chumba chake anakuwa huru zaidi
kuangalia kwa muda anaoutaka na huenda wengine wanakosa muda wa kula na hata kulala
kwa wakati.
Pamoja na mapenzi hayo kwa watoto wazazi watambue kuwa
watoto wenye runinga katika vyumba vyao wana uwezekano mkubwa wa kuwa na uzito
wa kupindukia kuliko wale ambao hawana hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa
na wanasayansi.
Utafiti huo uliofanywa na wanasayansi hao umebaini kuwa
runinga humsababishia mtoto kuwa na uzito kupindukia.
Watafiti hao kutoka chuo cha wanasayansi walibaini kuwa
watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi kwa kuangalia runinga kwa muda mrefu
hivyo wanakuwa na uwezekano mkubwa wa uzito wa miili yao kuongezeka.
Watafiti wanasema kuna kila sababu ya kuchunguza uwezekano
huo kwa watumiaji wa vipakatanishi (laptops) na simu za mkononi (mobiles). Wanasema mbali na uzito kupindukia wakati
watoto wanapotumia muda mrefu kutazama runinga hupata madhara mengi ya kiafya.
Hata hivyo, watafiti hao wanasema hawawezi kuwa na uhakika
kuhusu nini kinachosababisha uhusiano baina ya kutazama runinga na kuongezeka
kwa mwili, lakini wanasema huenda sababu ikawa ni watoto wenye runinga vyumbani
kusinzia kwa muda mfupi wakitumia muda kuitazama.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Kimataifa la
International Journal of Obesity ulitathmini data kutoka kwa watoto wadogo zaidi
ya 12,000 nchini Uingereza.
Wanasayansi hao walibaini kuwa zaidi ya nusu ya watoto
waliokuwa na runinga katika vyumba vyao vya kulala wakiwa kwenye umri wa miaka
saba.
Baadae watoto walipofikia umri wa miaka 11, watafiti
walipima viwango vya uzito wao wa mwili kulingana na kimo chao cha urefu kwa
kuangalia asilimia ya mafuta ya mwili waliyonayo.
Wasichana waliokuwa na runinga ndani ya vyumba vyao wakiwa
na umri wa miaka saba walibainika kuwa asilimia 30 ya uwezekano wa kuwa na
uzito wa mwili wa kupindukia wanapofikia umri wa miaka 11, wakilinganishwa na
watoto wenzao ambao hawakuwa na runinga vyumbani mwao huku wavulana wakiwa
asilimia 20.
Mtafiti Dk Ania Heilmann, amesema utafiti unaonesha kuwa
kuna ushahidi wa wazi wa uhusiano baina ya kuwa na runinga chumbani kwa mtoto
na kuongezeka kwa uzito wa mwili wa mtoto.
Wataalamu nchini
Dk Fazeel Sajeed kutoka hospitali ya Sanitas anasema anaunga
mkono utafiti huo kwa kusema mtoto anapotazama runinga mara nyingi anakuwa
katika mazingira ya kula.
Anasema mtoto ambaye anaangalia runinga huku anakula huwa
anakula chakula kingi ukilinganisha na yule ambaye anakula bila kuangalia
runinga.
Anasema hii ni kutokana na akili ya yule mtoto kuwa katika
runinga muda wote mtu ambaye anakula bila kutizama runinga ni tofauti na yule
ambaye anaangalia na akili yake haifikirii kwenye chakula.
“Nakubaliana na utafiti huu kwani mtoto anapokuwa karibu na
runinga anakuwa na uzito mara nyingi watoto hupenda kuangalia huku wanakula na
unakuta vyakula wanavyokula ni vile vyenye sukari na mafuta, mfano viazi
(chipsi)” anasema
Dk Sajeed anashauri wazazi wawapunguzie watoto muda wa
kuangalia runinga sio muda wote mtoto anakuwa kwenye runinga hasa kwa wale
ambao zipo vyumbani mwao.
Anaongeza kuwa si vibaya mtoto kutazama runinga ila
anatakiwa kutazama vitu ambavyo atajifunza kama mtoto na sio kuangalia kwa
masaa mengi hali ambayo itamletea madhara kiafya.
“Kama chumbani kwa mtoto kuna runinga basi ni jukumu la
mzazi kuhakikisha kwamba mtoto anapangiwa muda wa kuangalia na mzazi anajukumu
la kuhakikisha mtoto haathiriwi na ile runinga aliyomuwekea chumbani”
Anasema mzazi kuwa makini na mtoto pia itaepusha tabia za
kuangalia tv bila kuwa na muda wa kutosha kupumzika au kuvifanyisha viungo
mazoezi kuliko kukaa sehemu moja kwa muda mrefu hali inayosababisha uzito wa
mwili kuwa mkubwa kuliko umri alionao.
Kwa upande wake dokta Katoto Nestory kutoka Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya (NHIF) anasema huenda kweli mtoto kuwa na runinga chumbani kwake itamsababishia uzito kwa sababu mtoto anakuwa amekaa sehemu moja kwa muda
mrefu
“Ifahamike kuwa uzito wa mwili hupungua kwa kufanya mazoezi
kwa hiyo kama mtoto anachukua muda mwingi kukaa akitazama runinga ina maana
mwili unakuwa umetulia hivyo kusababisha uzito kuongezeka”
Dk John Vicent anasema suala la mtoto kuwa na uzito
kupindukia halina uhusiano wa moja kwa moja na mtoto kuangalia runinga kwa muda
mrefu lakini huenda likachangia.
Anasema mara nyingi watoto wanapokuwa likizo au siku ambazo
hawajaenda shule hutumia muda mwingi kuangalia tv ikiwamo katuni kwa hiyo
anaweza kutumia hata zaidi ya saa moja.
Anadai kwamba mtoto anapokaa kwa muda mrefu sehemu moja
anajijengea tabia ya uvivu hii inafanya hata chakula anachokula kutomeng’enywa
vizuri na hatimaye mtoto anakuwa na uzito mkubwa na hata kunenepa zaidi.
Dk Vicent anaongeza kuwa tatizo la kuwa na uzito mkubwa si
kwa watoto pekee bali hata kwa watu wazima ambao wanakaa sehemu moja kwa muda
mrefu.
Nashauri wazazi wawe makini na watoto wao suala la afya kwa
mtoto linahitaji umakini wa hali ya juu watambue kuwa mtoto anapokuwa na tv
ndani ya chumba chake sio tu kuongezeka kwa uzito kama utafiti unavyoeleza bali
inaweza kuvunja maadili ya mtoto.
Wazazi wazungumza
Mkazi wa Temeke Jijini Dar Es Salaam Maimuna Shabani amesema
mzazi kumuwekea mtoto tv katika chumba cha kulala sio tu itamsababishia madhara
kama hayo ya kuwa na uzito wa kupindukia lakini pia hata maadili hayatakuwepo.
Anasema ni vyema wazazi wakatumia utafiti huu kujifunza na
kutambua kwamba runinga chumbani kwa mtoto si jambo jema.
“wanasayansi wamefanya kazi yao kwa kutafiti juu ya madhara
yatokanayo na mtoto kuangalia tv kwa muda mrefu awapo chumbani kwake sasa ni
jukumu la mzazi kuwa makini”
Maimuna mama wa watoto watatu anaongeza kuwa yeye watoto
wake huangalia runinga kwa muda mfupi.
No comments:
Post a Comment