Watu wengi walioathiriwa na virusi vya ukimwi (VVU), hupatwa
na maradhi tofauti ya kinywa.
Na wakati mwingine wanapopatiwa matibabu ya kinywa na
madaktari, huwa hawasemi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya usiri wa
mgonjwa kwa daktari kuhusu afya yake kwa ujumla, kukosa umakini kwa daktari ama
sababu nyingine yoyote.
Hivyo, kushindwa kutambua hali hii, husababisha mhusika
kukosa matibabu sahihi, hivyo kuendelea kuumia.
Kwa maana hiyo, ni muhimu kwa waathirika kufahamu ya kwamba,
wanapokwenda kwa daktari wa kinywa na meno kupatiwa tiba, ni vyema wakaelezea
historia nzima ya afya zao.
Hii itamsaidia daktari kupata ufahamu wa kutosha na kumuwezesha
kutoa matibabu husika na kikamilifu.
Kwani baadhi ya maradhi yanayoweza kumkumba muathirika wa
ukimwi kinywani ni pamoja na kinywa kuwa kikavu (Xerostomia), fangasi
(candidiasis), maradhi ya fizi (Periodontal diseases), saratani ya kinywa na
vidonda kinywani.
Ila izingatiwe maradhi niliyoyataja hapo juu si kwamba
huugua watu wenye maambukizi ya VVU au wanaougua Ukimwi pekee la hasha,
yanaweza kumpata yeyote yule.
Ila muathirika yuko kwenye hatari ya kuugua mara kwa mara
kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili.
Madhara
Madhara ya aina mbalimbali huweza kuwakumba waathirika wa
VVU/Ukimwi kwa asilimia 30 hadi 80 kama hawatayatibu haraka.
Hiyo husababishwa na ukimya wa wao kutotoa taarifa kwa
madaktari wanaokwenda kutibiwa.
Utafiti uliofanyika kwa nchi zilizoendelea unaonesha asilimia
9.1 tu ya waathirika ndiyo hupata matibabu sahihi ya maradhi hayo ambayo
hutokea kinywani ikiwa ni matokeo ya maambukizi ya VVU na kuugua Ukimwi.
Hata hivyo, inaelezwa maradhi hayo ya kinywa yameanza
kupungua kwa waathirika tangu yalipoanza matumizi ya dawa za kufubaza virusi.
Tatizo la kinywa
kikavu
Hali ya kinywa kuwa kikavu inayosababishwa na kupungua kwa
uzalishaji wa kawaida wa mate, ni moja kati ya sababu kuu zinazochangia
kutoboka kwa meno kwa waathirika wa VVU/Ukimwi.
Inakadiriwa asilimia 30 hadi 40 ya waathirika wa virusi vya
ukimwi na ukimwi, hupitia hali hiyo ya kuwa na kinywa kikavu cha hali ya
wastani hadi ya juu, hali ambayo husababishwa na baadhi ya dawa za kufubaza
makali ya VVU/ukimwi ikiwamo aina ya didanosine, au husababishwa na kuongezeka
kwa seli za CD8+ kwenye matezi makubwa ya kuzalisha mate kinywani.
Mabadiliko ya wingi na ubora wa mate ikiwamo wa kupambana na
bakteria kinywani, huweza kusababisha pia kuoza kwa meno miongoni mwa
waathirika wa virusi vya Ukimwi na pia kusababisha mardahi ya fizi miongoni.
Fangasi wa aina gani huwakumbwa waathirika wa VVU na Ukimwi.
Fangasi wa kwenye kinywa huweza kutokea katika sura
mbalimbali kama vile vidonda sugu kwenye kona za midomo ama hali ya utando
mweupe usioondoka kwa kupiga mswaki ama kukwangua kwa ulimi.
Halikadhalika, kuna aina nyingine ya fangasi ambayo huwa ni
ngumu kuitambua kitaalamu inaitwa Erythematous candidiasis.
Hizi ni fangasi ambazo mara nyingi huwatokea zaidi watu
walioathirika.
Mgonjwa hutokewa na alama nyekundu inayosambaa kidogo na
kutengeneza duara kwenye sehemu ya juu ya ulimi ama kwenye kaakaa.
Mgonjwa mwenye hali hii huwa analalamika kupata maumivu kila
alapo vitu au vyakula vyenye chumvi, pilipili au kunywa vitu vyenye vya asili
ya tindikali.
Fizi kuvimba na kutoa
damu
Ugonjwa wa fizi kutoa damu husababishwa na kuvimba. Mara nyingi ufizi wenye kutoa damu. Na mara nyingi huwa na rangi nyekundu tofauti
na rangi ya kawaida ya pinki ya ufizi wenye afya.
Kwakua ugonjwa huu hasa katika hali ya mwanzo unaweza
usionekane kama ni tatizo, lakini inapaswa itambulike kuwa ufizi wenye afya
njema hautoi damu wakati wa kupiga mswaki ama uking’ata kitu, hivyo ni muhimu
kuchukua hatua mapema ili kuutibu.
Hii ni kwa sababu ugonjwa huo unapoendelea huweza kuathiri
mfupa wa taya sehemu ambayo jino hujishika.
Ikiachwa pia huweza jino ama meno kulegea na hata kung’oka.
Wakati ni kweli kuwa ugonjwa wa fizi kuvimba na hata kutoa damu
huweza kumpata mtu yeyote yule ambaye hazingatii misingi ya afya bora ya
kinywa, kwa waathirika wa ukimwi hali hii huwatokea zaidi kutokana na kuwa na
kinga dhaifu ya mwili.
Ufizi wenye afya ni imara na una rangi ya pinki
iliyopauka. Kama fizi zimevimba,
zimekuwa nyekundu na zinatoa damu kiurahisi inawezekana mhusika ana tatizo la
ugonjwa wa fizi. Na kwa kuwa ugonjwa huo
mara nyingi hauna maumivu, unaweza kudumu kwa muda mrefu bila kujijua.
Dalili zake ni zipi
Dalili zake ni pale mtu anapobaini kuwa fizi zake zimevimba,
kulainika na kuanza kubonyea.
Wakati mwingine mgonjwa hujihisi fizi hizo zinamuuma au
kutoa damu kirahisi mara anapopiga mswaki au anapoflosi na wakati mwingine
anaweza kutoa damu kwenye mswaki.
Dalili nyingine ni mabadiliko ya rangi ya ufizi kubadilika
na kutoka rangi ya pinki iliyopauka na kuwa nyekundu sambamba na harufu mbaya
ya kinywa.
Kaposi sarcoma
Huu ni aina ya uvimbe unaoambatana mara nyingi na maambukizi
ya virusi vya ukimwi na huweza kutokea sehemu yoyote ya mwili, hata hivyo
hutokea mara nyingi kinywani kuliko sehemu nyingine.
Uvimbe huo huwa na rangi mbalimbali ikiwamo nyekundu na
zambarau na kimaumbile, huweza kuwa na sura ya ama kinundu, ama kidonda ama
hata kiduara cha rangi ya zambarau ama nyekundu bila kuwa na uvimbe.
Kwa kawaida uvimbe huo hauna dalili yoyote ya maumivu na
rangi yake huzidi kukolea kadiri muda unavyoongezeka.
Vidonda vya mara kwa
mara
Hivi ni vile vinavyotokea kinywani na kwa kawaida hujirudia
mara kwa mara hata baada ya kupona.
Halikadhalika, vidonda hivyo huweza kutokea sehemu yoyote ya kinywa. Mpaka sasa sababu ya kwa nini vinatokea
haijajulikana. Lakini inahusishwa na
kupungua kwa kinga mwilini.
Ikumbukwe vidonda hivyo huweza kumtokea hata mtu asiye na
maambukizi na vina dalili sawa. Inaaminika
kuwa msongo wa mawazo ama madabadiliko ya vichocheo (hormone) ambayo hushusha
kinga ya mwili husababisha mtu kuugua.
Vidonda hivyo huwa vinauma hasa wakati wa kutumia vyakula
vya chumvi, pilipili ama vinywaji vyenye asili ya tindikali.
Kwa mtu ambaye hajaathirika vidonda hivyo vinaweza kudumu
kwa siku kati ya saba hadi 14 kupona, lakini kwa muathirika huchukua muda mrefu zaidi.
Madhara ya hali hiyo
kinywani
Hali hii ya maradhi mbalimbali kinywani miongoni mwa
wagonjwa au waathirika wa ukimwi huwa na athari za moja kwa moja kwa afya zao.
Kwani pamoja na mambo mengine, huweza kusababisha yafuatayo
madhara kwa mhusika ikiwamo kukosa hamu ya kula, kwani wengi wao huona kula
chakula ni kama sehemu ya adhabu kutokana na maumivu anayoyapata wakati wa
kula.
Wengi hukata tamaa ya kuishi anapoona hawezi kula kama
kawaida, hali hii humsababishia kudhoofu afya yake na kuhatarisha maisha yake.
Kwani kama mtu anatumia dawa za kufubaza virusi
vya ukimwi halafu hapati lishe ya kutosha, matokeo yake ni kumpoteza.
No comments:
Post a Comment