Chupa kupasuka ni neno lililozoeleka katika jamii yetu likiwa na
maana kitabibu kama ngozi au tando laini inayoyazungunguka maji yanayomfanya
mtoto aliye ndani ya nyumba ya uzazi kuelea, imepasuka na maji hayo kutoka.
Tando hii ya ngozi huweza kupasuka kiasili wakati au baada
ya uchungu kuanza. Katika hatua hii si
tatizo bali ni hali ya kawaida kujitokeza na kitabibu hujulikana spontaneous
rupture of membrane.
Pia, tando hii inaweza kupasuliwa na mtoa huduma kwa baadhi
ya wajawazito, kulingana na hali zao. Kwa
mfano, mtoa huduma anaweza kumtathmini mjamzito, kama kuendelea kuwapo kwa
ujauzito huo kunaweza kuhatarisha maisha ya mtoto tumboni.
Na kama chupa itapasuka kabla ya muda wake kufika, huenda
ikawa ni tatizo la kiafya au madhara yatokanayo na hali ya ujauzito.
Kupasuka kwa ngozi laini kabla ya mjamzito kupata uchungu
halisi baada ya kukamilika kwa wiki 37 za umri wa mimba, kitabibu huitwa
rupture of membrane (PROM) na kupasuka kwa chupa mapema kuliko kawaida kabla ya
wiki ya 37 ya umri wa mimba, kwa neno la kitabibu huitwa preterm premature
rupture of membrane (PPROM).
Inakadiriwa kati ya asilimia 8 hadi 10 ya wajawazito hupata
PROM na asilimia mbili hupata PPROM. Hili
ni moja ya tatizo linaloweza kuchangia kuzaliwa mtoto njiti.
Madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito yanaweza kuwapo
kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Kutokea kwa tatizo hili kunamhatarisha mjamzito na mtoto
aliye ndani ya nyumba ya uzazi kupata matatizo likiwamo shambulizi kwenye ngozi laini inayomzunguka na maji maji ambayo mtoto huelea ambayo
kitabibu yanaitwa Chorioamnionitis, kondo la nyumba kujipachika vibaya, kuumia
kihisia, kupata matatizo wakati wa usimuliaji uchungu na kuchelewa kushikamana
kwa mama na mtoto.
Kwa upande wa mtoto, anaweza kuzaliwa baada ya siku saba
tangu kutokea kwa PPROM, hii hutokea kwa asilimia 80 waliopata tatizo hilo.
Madhara anayoweza kupata mtoto ni pamoja na kuzaliwa njiti,
kupata uambukizi mkali wa bakteria ambayo huambatana na homa kali, maji ya
nyumba ya uzazi kuwa machache na kuzaliwa na kasoro usoni.
Matatizo mengine hujitokeza wakati wa kuzaliwa. Kwani anaweza kupata matatizo kwenye mapafu,
kuzaliwa na miguu na mikono yenye ulemavu, kuathirika kwa ukuaji, kuchoropoka
kwa kitovu na mishipa ya damu kuvujisha damu kwenye ubongo. Hali hiyo inayoweza kuchangia kupata jeraha
la ubongo.
Wajawazito walio katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili ni
pamoja na watumiaji wa sigara, watumiaji wa dawa za kulevya na wenye uambukizi
wa viungo vya uzazi.
Dalili kubwa ni kutokwa au kuchuruzika ghafla kwa maji
kwenye sehemu za siri za mjamzito ambayo yanaweza kusambaa mpaka katika maeneo
ya mapajani.
Maji maji hayo yanaweza kutoka pale anapokohoa au kucheza
kwa mtoto kunaweza kusababisha kuchoropoka kwa kitovu cha mtoto.
Sababu ya maambukizi inaweza kuwa mjamzito
ameugua homa, anatokwa na maji maji yenye harufu kali ukeni na maumivu chini ya
kitovu.
No comments:
Post a Comment