Pombe, maradhi na ulaji wa vyakula usiozingatia maoni ya
wataalamu wa afya na tiba lishe ni baadhi ya mambo yanayotajwa kusababisha
upungufu wa nguvu za kiume.
Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume linatajwa kushika kasi
na limesababisha baadhi ya wanaume kadhaa kuishi maisha ya unyonge yaliyojaa
hofu hasa kuhusu hatima ya uhusiano wa ndoa zao.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya waathirika hao wameendelea
kuhangaika kurejesha heshima kwenye ndoa zao kwa kusaka tiba, wengine hosptali
na wengine kwa waganga wa jadi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa tumbo na kifua wa Hospitali ya
taifa ya Muhimbili, Maurice Mavura anasema tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume
lipo.
“Haya matatizo yalikuwapo, isipokuwa inaonesha wengine
waliougua tatizo hilo waliogopa kwenda hospitali kusaka tiba,” anasema Dk
Mavura.
Anasema: “pengine walishindwa kujitokeza kwa kuhofia
unyanyapaa au kuona aibu, lakini kwa sasa wengi wao uoga umewatoka wanafika
kutibiwa matatizo hayo ikiwamo tezi dume,” anasema.
Dk Mavura anasema kutokana na sababu hizo, ni vigumu kueleza
idadi ya wenye matatizo ya nguvu za kiume kama wameongezeka ama wanapungua.
“lakini pia kwa sasa kujitokeza na kuja kutibiwa huenda
uelewa umeongezeka baada ya kupata elimu na sasa wameona umuhimu wa matibabu,”
anasema Dk Mavura.
Matibabu
Anasema wanatibu matatizo hayo kwa njia mbalimbali, lakini
upasuaji wa kuweka vipandikizi vya mrija kwenye uume bado hawajaanza kuufanya
nchini, licha ya kufanyika katika hospitali zingine za nje ya nchi.
“Upasuaji huo kuna baadhi ya nchi zenye vifaa hivyo
zinafanya, hapa kwetu bado hatujaanza,” anasema Dk Mavura.
Daktari Anna Sarra wa Muhimbili anasema tatizo hilo ambalo
kitaalamu linaitwa Ericticle Dysfunction husababishwa na mambo mengi ikiwamo
maradhi.
Anayataja maradhi hayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la
damu (BP), uti wa mgongo (Spinal cord) na kuharibika kwa mishipa kutokana na
upasuaji.
Dk Sarra anasema ili mwanaume amudu kushiriki tendo la ndoa,
anatakiwa mfumo wake wa damu uwe kwenye mzunguko unaotakiwa, pia ubongo,
mishipa ya fahamu na homoni.
“Kutokana na kuugua maradhi niliyotaja, pia kuna dawa
zinazochangia kupunguza nguvu za kiume. Zipo
ambazo husababisha homoni kushindwa kuwa katika mfumo wake wa kawaida, hivyo
kumletea athari mwanaume,” anasema na kuongeza:
“Pia, kuna baadhi ya miili ya watu inatambua sukari kama
adui, hivyo husababisha kuchomwa sindano ya DM I, kwa kawaida hupatwa na ganzi,
wengine hupatwa matatizo ya kisaikolojia, hivyo hupoteza hisia za mapenzi,”
anasema Dk Sarra.
Mtindo wa maisha
unavyomuathiri mwanaume
Dk Sarra anasema mtindo wa maisha wa baadhi ya wanaume,
ikiwamo unywaji wa pombe kupita kiasi, kuvuta sigara na dawa za kulevya aina
zote huchangia tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
Anasema mtindo wa ulaji wa vyakula bila kuzingatia ushauri
wa wataalamu wa afya na tiba lishe, hasa ulaji wa nyama nyekundu, ni miongoni
mwa sababu zinazochangia upungufu wa nguvu za kiume.
Wanaume wenye umri
gani wapo hatarini Zaidi
Dk huyo anasema wanaume wenye umri kati ya miaka 40 na
kuendelea ndiyo hukumbwa na tatizo hilo.
Hata hivyo, anasema wapo wengine ambao si wengi sana wenye
umri chini ya miaka 40 hukumbwa na tatizo hilo.
Dk Sarra anasema tatizo hilo linaweza kutibiwa kama mtu
atakubali kufanyiwa uchunguzi na wataalamu.
Anasema matatizo ya nguvu za kiume yanatibika kwa njia
mbalimbali, ikiwamo mhusika kutibiwa kwa dawa aina ya Viagra.
“Viagra inatibu tatizo hilo kwa vipimo maalumu vinavyotolewa
na daktari, lakini wapo ambao wamebaini hiyo ni dawa, huamua kuitumia bila
maelekezo ya daktari na hujikuta wakipata matatizo zaidi,” anasema Dk Sarra.
Njia nyingine ya kutibu tatizo hilo ni kwa muathirika
kufanya mazoezi ya kutosha.
Anasema matibabu hayo huwaelekeza waathirika kuyafanya kwa
ratiba maalumu.
“Mazoezi ni muhimu na ni tiba nzuri kwa sababu husaidia
kufanya mzunguko wa damu kwenda vizuri mwilini hali inayosaidia mishipa ya
viungo kufanya kazi inavyotakiwa,” anasema Dk Sarra.
Waganga wa tiba asili
nao walonga
Tabibu wa tiba za asili, Omari Kuyunguyo wa jijini Dar Es
Salaam anasema tatizo la nguvu za kiume linawakumba wanaume wengi hivi sasa
tofauti na miaka 15 iliyopita ambayo amekuwa akiifanya kazi hiyo.
“Huu ni mwaka wangu wa 16 nafanya kazi ya kutibu, hapa sina
daftari lakini nakuhakikishia, wanaume wengi wanaofika kwangu kusaka tiba ya
tatizo la nguvu za kiume ni wengi,” anasema Kuyunguyo.
Anasema kati ya wanaume 100 wakiwamo vijana wanaofika
kutibiwa kwake kwa mwezi, 80 wanakabiliwa na upungufu wa nguvu za kiume.
“Sababu za kuugua zipo tofauti, lakini wanaume wengi
wanaugua tatizo hilo na mimi nimewahi kuugua,” anasema Kuyunguyo na kuongeza:
Tabibu mwingine, Sheikh Swalehe Kayumbo wa Tanga anasema
amefanya shughuli hiyo miaka 45, lakini ni jambo la kushangaza kuona wanaume
wengi wanaofika kwake wanasumbuliwa na upungufu wa nguvu za kiume.
“Hasa waishio mjini kwa sababu wengi wanakula vyakula vya
kukaanga na kukoboa, pia hata viungo vinavyotumika kwenye mboga vingi vina
kemikali, mfano ndimu ya unga huwezi kufananisha na ile ya tunda, matokeo yake
ndiyo hayo wanaume wengi wanajikuta wanashindwa kutotimiza wajibu wao,”
anasema.
Kayumbo anabainisha kuwa gharama za tiba anazotoza ni
kuanzia sh 50,000 ingawa pia inaweza kupanda kulingana na ukubwa wa tatizo.
“tatizo hili linaweza kuepukwa kwa wanaume kujikita kula
vyakula vya asili ikiwamo asali na maziwa ya ng’ombe halisi kila siku,” anasema.
Anasema wakipenda chipsi na nyama choma hasa
kuku wa kisasa ambao wengi hula na kutafuna hadi mifupa, wajiandae kubeba hadi
gharama za matibabu.
No comments:
Post a Comment