Tuesday, January 9, 2018

DALILI HATARI KWA MTOTO

dalili hatari kwa mtoto

Zipo dalili na viashiria ambavyo ni kielelezo vinavyoweza kuonesha mtoto anaumwa sana na dalili hizi zimegawanywa katika sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni dalili za hatari na sehemu ya pili ni ile ya dalili zinazohitaji kupewa kipaumbele.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi au walezi wasio na ufahamu, wengi wao huchukulia dalili hizo ni za kawaida na huchelewa kufanya uamuzi wa kuwapeleka watoto hospitali mapema kufanyiwa uchunguzi sambamba na kupatiwa huduma za afya.

Inapotokea mtoto mwenye dalili za hatari akacheleweshwa kupatiwa huduma za afya, huweza kupoteza maisha au kupata madhara ya muda mrefu.

Hivyo, kuna umuhimu kwa wazazi na walezi kuzijua dalili hizo ili mara anapobaini kuwa zimejitokeza kwa watoto wao, wawahi kuwapeleka kwenye huduma za afya ili wahudumiwe kabla ya madhara makubwa hayajajitokeza.

Na kama itatokea mtoto akawa anashindwa kunyonya kabisa au kunywa chochote hata akilazimishwa inashindikana, hii ni moja ya kiashiria kwamba mtoto ana ugonjwa mkali.

Mtoto anapokuwa na ugonjwa wowote mkali ikiwamo wa malaria kali, nimonia kali au uti wa mgongo, mara nyingi dalili kama hizo hapo juu hujitokeza.

Kwa mfano ni kule kutapika kusiko kwa kawaida, huku akitoa kila kitu alichokula na hutumia nguvu nyingi na matapishi hutoka kwa msukumo mkubwa, hii ni moja ya dalili inayoashiria mwili kushambuliwa na ugonjwa mkali.

Unapoona ametapika kwa namna hiyo, mpeleke hospitali au kwenye vituo vya afya haraka.

Pia, kupatwa na degedege ni dalili inayoashiria uwapo wa ugonjwa mkali unaoathiri mfumo wa fahamu ikiwamo ubongo.  Pale unapoona mtoto amepatwa na degedege, jua ni tatizo la kiafya na si vinginevyo.

Maradhi kama malaria, nimonia, jeraha la ubongo, uti wa mgongo, uwapo wa vimelea katika damu, upungufu wa sukari mwilini na chumvi, huwa na madhara ya kiafya yanayoweza kusababisha degedege.

Mtoto anaweza kukosa nguvu na kuwa mlegevu kupita kiasi na hufikia hatua ya kupoteza fahamu au kuweweseka.

Mambo yanayoweza kusababisha kupoteza fahamu ni pamoja na upungufu wa damu, kukosa hewa ya kutosha, sukari kushuka, upungufu wa maji na chumvi mwilini.

Matatizo hayo husababishwa na maradhi kama malaria, nimonia,uti wa mgongo na uwapo wa vimelea na taka sumu zake katika damu.

Tukiachana na dalili za hatari, dalili ambazo zinapewa kipaumbele kama viashiria vya uwapo wa tatizo la kiafya kwa watoto ambapo mzazi au mlezi atapaswa pia kuchukua hatua atakapoziona kwa watoto.

Dalili hizo ni joto la mwili kupanda, kukohoa mfululizo, kushindwa kupumua au kupumua haraka, mwili kubadilika rangi kuwa wa bluu au manjano, shingo kukakamaa, kuharisha zaidi ya mara tatu, maambukizi ya sikio, kulia mfululizo bila kunyamaza na kutokwa na vipele vingi mwilini.
Share:

No comments:

Post a Comment