Takwimu za Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF) zinaonesha
mtu mmoja kati ya kila 11, ana kisukari.
Kuna zaidi ya watu wazima milioni 425 duniani kote wenye maradhi haya
yasiyoambukiza.
Takwimu hizo pia, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana,
zinabainisha kwamba mmoja kati ya wagonjwa wawili wa kisukari hafahamu kama
anaugua maradhi hayo. Hii ni sawa na
nusu ya wagonjwa wote milioni 425 ambao ni takriban milioni 212.
Hata wajawazito nao hawako salama. Ripoti hiyo inaeleza, ugonjwa huo huathiri
mjamzito mmoja kati ya sita duniani kote ambako kuna zaidi ya
watoto milioni wenye kisukari aina ya kwanza.
Miongoni mwa watu wote wenye kisukari, ripoti inaonesha
theruthi mbili ya wagonjwa hao, sawa na milioni 279 wanaishi mjini ambako
vyakula vya asili ama ni adimu au ghali zaidi hivyo kuongeza uwezekano wa
kupata maambukizi hayo.
Pamoja na ukweli huo, takwimu hizo zinaonesha wagonjwa
watatu katika kila wanne wanaishi kwenye nchi maskini au zenye kipato cha
kati. Wawili kati ya watatu au theluthi
mbili ya wagonjwa hao ambao ni sawa na milioni 327 wana umri wa kufanyakazi
wakiwa na umri kati ya miaka 20 mpaka 64.
Kutokana na ukweli huo, serikali zinatumia gharama kubwa
kukabiliana na maradhi hayo. Inaelezwa,
asilimia 12 ya bajeti yote ya afya huelekezwa kukabiliana na kisukari. Mkuu wa
Kitengo cha Kliniki ya Kisukari katika Hospitali ya M.P Shah ya jijini Nairobi,
Dk Sairabanu Sokwalla anasema wagonjwa wengi bado hawajajigundua kutokana na
kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao.
“Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni
wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Takwimu zinaonesha hali ilivyo huko Asia, Amerika na Ulaya kutokana na
wananchi wake kuwa na utaratibu wa kupima.
Barani Afrika, wengi hawajui kuhusu afya zao,” anasema.
Ukweli kuhusu hilo, unathibitishwa na Winnie Ngiyo, mwanamke
wa miaka 32 anayekiri: “Niliharibiwa ujauzito wangu wa pili. Hapo ndipo nilihitaji uchunguzi ili kujua
sababu, majibu yalibainisha kiwango kikubwa cha sukari mwilini mwangu.”
Mkenya huyo anayeishi Mtaa wa Westlands, jijini Nairobi
amefunguka na kuweka wazi kisa hicho na namna alivyoweza kupambana na kisukari
mwilini mwake, kutoka 23mmol/1 mpaka kiwango cha kawaida, 6.2mmol/1.
Apona kisukari
Baada ya kugundulika miezi 18 iliyopita, jukumu kubwa kwake
lilikuwa ni namna ya kuepukana na kisukari kwa kuwa ipo historia katika familia
yake, aliyojua ni ugonjwa wa kurithi.
Uzito wake kwa wakati huo ulikuwa kilogram 110: “Nimepunguza
kilogram 21, haikuwa rahisi nilianza kunywa maji mengi, kula vyakula kwa
kufuata mpangilio wa lishe hata kwa mume na mtoto wangu wa kiume mwenye miaka
10 pamoja na kufanya zaidi mazoezi.”
Hata hivyo Winnie anasema ni rahisi kuishi na kisukari ikiwa
utazingatia matibabu na kuacha matumizi ya vyakula visivyofaa kwa mfano unywaji
pombe uliokithiri na kutofanya mazoezi.
Yeye anafanya mazoezi mara tatu kwa wiki akitumia saa moja
kuushughulisha mwili wake ili kupunguza mafuta.
Kwa kuwa anaamini ulaji wa baadhi ya vyakula ikiwemo pipi, keki au
chipsi kwa wingi huongeza tatizo, huviepuka.
“Inapaswa kuzingatia ulaji unaofaa, katika kila mlo nazingatia
robo tangu kunakuwa na mbogamboga, matunda na wanga kwa kiasi kidogo sana, zaidi
naepuka vyakula vyenye mafuta,” anasema.
Kupunguza madhara ya hayo, anashauri watu wawe na tabia ya
kupima afya mara kwa mara kujua kama wana kisukari au la pamoja na kufuatilia
matibabu kwa wenye maradhi hayo ili kuchukua hatua za kuudhibiti mapema.
“Tabibu wangu aliniweka wazi kwamba nifuatilie matibabu inavyopaswa
nitapona. Hivi sasa sukari yangu
imeshuka na ni ya kawaida. Sasa nimeacha
kutumia dawa nimepona,” anasema.
Winnie mwenye mtoto mmoja, ana kiu ya kuwa na watoto watano
hata hivyo anasema hajakata tamaa kwani madaktari wamemruhusu kuendelea kuzaa
hivyo kuwa na uhakika wa kuongeza waliobaki.
Baada ya kugundulika kuwa na maradhi hayo, familia yake
ilimuunga mkono kupambana na maradhi hayo.
Anasema mumewe alihakikisha anakula vizuri na kufanya vitu
vinavyotakiwa.
“Tulipopoteza mtoto ilituuma sote hivyo tuliamua kubadili
mtindo wa maisha. Tunaishi maisha mapya,
nilikuwa na safari ndefu kupata,” anasema Winnie. Ili kuhamasisha matibabu ya kisukari, Winnie
ameunda kundi la mtandao wa Whatsapp analolitumia kutoa elimu kwa wagonjwa
walio katika matibabu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Dk Sokwalla anasema ugonjwa wa kisukari husababishwa na
mtindo wa maisha na mara nyingi waathirika wakubwa ni wanawake. Anazitaja sababu kuu za kisukari kuwa ni
uzito kupita kiasi na kutozingatia lishe na ulaji unaofaa huku akitahadharisha
kukua kwa maradhi hayo kitakwimu.
Tanzania
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu anasema kwa bahati mbaya, watu wengi hawajitambui kuwa na ugonjwa
huu na wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema.
Alisema katika nchi kumi zinazoongoza kwa kisukari barani
Afrika, Tanzania inashika nafasi ya nne na hadi mwanzoni mwa mwaka jana, Zaidi
ya watoto 2,000 wameingizwa kwenye rejista za watoto kwenye kliniki.
“Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari wapo
kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Utafiti wa mwaka 2012 uliohusisha wilaya 50 nchini ulionesha asilimia
9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa
kisukari,” alisema Ummy.
No comments:
Post a Comment