Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa maradhi sugu
yanayoendelea kuathiri afya za mamilioni ya watu wa nchi nyingi duniani
Tanzania ikiwamo.
Ugonjwa huo unaongezeka haraka kiasi cha kuonekana ni janga
la ulimwengu.
Tunaelezwa kuwa kuna aina mbili za kisukari. Aina ya kwanza huanzia utotoni, na madaktari
hawajui jinsi ya kuizuia. Lakini kuna
aina ya pili ambayo imeathiri watu wengi kwa takribani asilimia 90 ya wanaougua
ugonjwa huo.
Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusianishwa tu na
watu wazima, hivi karibuni imegundulika kuwaathiri pia watoto.
Lakini wataalamu wanasema mtu anaweza kujikinga ili asipatwe
na kisukari.
Pamoja na kwamba ni tatizo kwa watu wengi wa rika na jinsia
tofauti, ila kupanda kwa kiwango cha kisukari kumeweza kuwa tatizo pia kwa
wajawazito kiasi cha kuwasababishia matatizo mbalimbali yeye na mtoto aliyeko
tumboni.
Kisukari cha mimba kinawatokea hata wale ambao awali
hawakuwahi kuugua ugonjwa huo.
Hali hiyo ikitokea humuweka mjamzito kwenye hatari ya kupata
kifafa cha mimba, msongo wa mawazo pamoja na kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Kisukari cha mimba huwakumba asilimia 3 hadi 9 ya wanawake
katika ile miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito.
Huathiri asilimia moja ya wanawake waliochini ya miaka 20 na
asilimia 30 ya walio juu ya miaka 44.
Asilimia 90 ya wanaokumbwa na tatizo hilo huweza kuondokana
nalo baada tu ya kujifungua.
Utafiti unaonesha wanawake wenye kiwango kikubwa cha sukari
kipindi cha ujauzito wapo katika hatari ya kujifungua watoto wakubwa, wenye
kiwango kidogo cha sukari mwilini na wenye manjano. Kisukari cha mimba ni hatari na kama
hakitatibika, kinaweza kusababisha mtoto aliyeko tumboni kupoteza maisha.
Watoto wanaozaliwa baada ya muda kupita miezi tisa, huzaliwa
wakiwa na uzito mkubwa na hupatwa na ugonjwa wa kisukari wakiwa na umri mkubwa.
Nini kinachochea
kisukari cha mimba
Yapo mambo yanayochochea kisukari cha mimba ambayo ni pamoja
na uzito wa kupindukia, historia ya kuwa na kisukari cha mimba katika ujauzito
uliopita, historia ya ugonjwa wa kisukari hasa cha ukubwani katika familia,
uvimbe katika ovari, hali inayofahamika kama polycystic ovarian syndrome,
wanawake wenye umri juu ya miaka 35 wapo katika hatari.
Pia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa katika ujauzito
uliopita, matumizi ya dawa aina ya glucocorticoids na beta blockers au
antipsychotics wakati wa ujauzito, huongeza hatari ya tatizo hilo, kuwa na
kiwango kikubwa cha presha ya damu wakati wa ujauzito ni kichochezi pia.
Matatizo wakati wa
ujauzito
Watoto wanaozaliwa na wanawake wenye kisukari cha mimba
ambao hawakupatiwa matibabu, huwa na uzito mkubwa.
Lakini mjamzito aliyepatiwa matibabu ya tatizo hilo, mtoto
anaweza akazaliwa mdogo ukilinganisha na miezi husika, kupatwa matatizo ya
ukuaji akiwa ndani ya uzazi.
Utafiti unaonesha tatizo la kujifungua watoto wenye uzito
mkubwa huwakumba wajawazito kwa asilimia 12.
Lakini wale ambao hawajawahi kuugua kisukari cha mimba
wanaougua ni asilimia 20 pekee.
Hali ikoje upande wa
watoto
Wale wanaozaliwa na mama zao wenye tatizo hilo, huwa katika
hatari ya kuugua homa ya manjano na huwa na kiwango kidogo cha sukari, kiwango
kikubwa cha chembechembe nyekundu za damu, kupatwa na matatizo katika mfumo wa
hewa na kuathiri upumuaji kwa sababu ya kuzaliwa mapafu yakiwa bado machanga.
Pia huwa na kiwango kidogo cha madini ya kalisiamu pamoja na
magnesium.
Mambo muhimu ya
kuzingatia
Kuhudhulia kliniki mara kwa mara kutokana na maagizo ya
daktari kunaweza kusaidia kulitatua tatizo hilo.
Mama anatakiwa kutunza afya yake kabla na baada ya
kujifungua.
Anatakiwa ajitunze na ahakikishe kiwango chake cha sukari
hakipandi kupitiliza hasa kwa wanawake wenye ugonjwa wa kisukari kabla ya
ujauzito.
Wanatakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyotumia, kufanya
mazoezi na wazuie ongezeko la uzito.
Wanawake wenye mpango wa kubeba mimba na tayari wanaugua
kisukari wanatakiwa kupata virutubisho vya folate hadi kipindi cha wiki mbili
wakati wa ujauzito kusudi kuondoa hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo
kwenye mfumo wa fahamu yanayofahamika kama ‘neural tube defects’.
Kwa kuzingatia haya yote, itasaidia kuondoa matatizo kwa
mama na mtoto kabla na hata baada ya kujifungua.
No comments:
Post a Comment