Aina ya utokaji mimba itakayoelezwa ni ile ijulikanayo kama
utokaji mimba usio kamili ‘incomplete abortion.’
Yawezekana mjamzito alikuwa ana tatizo la mimba kutishia
kutoka lakini baadaye hali hiyo inaweza kubadilika na mimba hiyo kutokana na
kuharibika, ikabakisha mabaki yaliyoharibika kwenye nyumba ya uzazi.
Hali hiyo inapojitokeza ina maana ujauzito huo umeharibika,
hakuna uhai wa mimba hiyo lakini mwili nao umeshindwa kutoa mabaki yote ya
kiumbe kilichopo katika nyumba ya uzazi.
Utokaji mimba usio kamili mara nyingi hutokea katika muhula
wa kwanza wa ujauzito. Sababu za utokaji
mimba wa aina hiyo ni sawa na aina zingine za utokaji wa mimba changa ikiwamo
ile inayotishia kutoka.
Utokaji mimba usio kamili huambatana na utokaji wa damu kwa
wingi ukeni ambao si wa kawaida ukilinganisha na utokaji wa damu ya hedhi.
Mgonjwa hutokwa na damu mfululizo ikiwa na mchanganyiko wa
mapande ya tishu yaliyochanganyika na damu huku ikiambatana na maumivu makali
yasiyovumilika wala kupotea katika eneo la chini ya kitovu na kusambaa kiunoni.
Tabibu au daktari anayekuhudumia pale atakapochunguza
atagundua mlango wa nyumba ya uzazi umefunguka huku mabaki ya kiumbe mengine
yakiwa yamebaki ndani ya nyumba ya uzazi.
Wakati mwingine hali hii inapotokea inaweza kuambatana na
homa, kuhisi kishiwa nguvu, kuonesha dalili za hofu au kuchanganyikiwa.
Hivyo ni vizuri pale unapoona dalili hizi, chukua hatua ya
haraka kufika hospitali upate matibabu.
Matibabu yake huwa ni rahisi na ni jambo linaloruhusiwa
kisheria, pale inapobainika mimba imeharibika na kutoka yote, mgonjwa
atalazimika kusafishwa kwa kuzingatia maadili ya kitabibu.
Usafishaji huu una lengo la kuondoa mabaki yote yaliyopo
ndani ya nyumba ya uzazi.
Uwapo wa mabaki katika nyumba ya uzazi unaweza kuzidi
kusababisha damu kutoka kwa wingi na pia kuwa makaribisho ya maambukizi ya
bakteria.
Mgonjwa atatakiwa amsimulie historia nzima kwa daktari ili
abaini chanzo ili kusudi tatizo hilo lisijitokeze katika mimba zingine hapo
baadaye.
Uchunguzi unaweza kufanyika ili kujua kama chanzo ni
maambukizi ikiwamo kaswende na virusi mbalimbali vinavyochangia mimba kutoka.
Dawa za kudhibiti maumivu na dawa za antibiotiki hutolewa
ili kukukinga na maambukizi ya bakteria baada ya kusafishwa.
Ni muhimu kwa mgonjwa wa tatizo hili kufikishwa katika
huduma za afya zinazotambulika ikiwamo vituo vya afya vya Serikali.
Ikumbukwe kuwa matibabu ya vichochoroni yanafanyika kwa
kutozingatia kanuni za kitabibu, hivyo mgonjwa anakuwa katika hatari ya
kusafishwa na vifaa vyenye maambukizi ya vimelea mbalimbali ikiwamo virusi vya
ukimwi.
No comments:
Post a Comment