Monday, February 19, 2018

HAYA NI MATATIZO YA KUTOPATA HEDHI


Ni Dhahiri kuwa kukosa au kutopata kabisa hedhi ni tatizo linalowapata wanawake wengi.

Kwanza kabisa ni vyema mwanamke akatambua ukweli kuwa, kukosa hedhi ni tatizo la kiafya, hata kama lisipoambatana na maumivu yoyote lakini mwanamke anapaswa kulitilia umakini wa hali ya juu.

Kwa sababu, kibaiolojia hedhi ya kila mwezi inatokana na mfumo unaojiendesha wenyewe ndani ya mwili pasipo ridhaa ya mwanamke husika, hivyo kutopata hedhi kunaashiria kuwa kuna tatizo kwenye moja ya mifumo aidha wa homoni au wa uzazi na kusababishwa na matatizo mengine.

Tatizo hili kwa kitaalam linaitwa amenorrhea, ni kukosekana kwa mzunguko mmoja au zaidi ya hedhi.  Kwa mwanamke aliyekosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo na kwa wasichana walio na umri zaidi ya miaka ya wastani wa 15-18 ambao hawajapata hedhi kwa pamoja, wapo kwenye kundi hili.

Sababu kuu ya kukosa hedhi ambao wengi pia tumeizoea ni ujauzito.  Kwa kawaida mwanamke hapati hedhi kwa kipindi chote cha ujauzito, kutokana na sababu za kibaiolojia.

Lakini sababu zingine zinaweza kuwa ni matatizo ya kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla au tezi zinazosaidia kuratibu viwango vya homoni mwilini kama nilivyoeleza hapo awali.  Ni muhimu kupata ushauri wa daktari ili kuchunguza moja ya matatizo haya.

Mwanamke hupitia dalili mbalimbali zinazoashiria kuwa ananyemelewa na tatizo hili, ikiwamo kutoa kiasi kidogo cha damu wakati wa hedhi, lakini pia mwanamke anaweza kupata dalili zingine kama vile uke kutoa ute wenye rangi ya maziwa mara kwa mara na hata wakati wa hedhi, maumivu ya kichwa, matatizo ya kuona maumivu kwenye kiuno na mgongo na kutokwa na chunusi usoni.

Tatizo la kutopata hedhi linaweza kutokea kwa sababu tofauti, baadhi ni za kawaida zinazojitokeza kwenye maisha ya mwanamke wakati mwingine yakisababishwa na matumizi ya dawa na matatizo mengine kiafya.

Kwanza kabisa, tatizo hili husababishwa na sababu za asili.  Katika kipindi tofauti, mwanamke anaweza kujikuta anakosa hedhi kutokana na sababu za ujauzito na kufikia umri wa kupoteza uwezo wa kuzaa kutokana na sababu za kiumri.

Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango.  Baadhi ya wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango wanaweza kukosa hedhi kwa kipindi fulani.  Na hata njia nyingine za uzazi wa mpango kama vile sindano na vipandikizi vinaweza kusababisha kukosa hedhi.

Aina fulani ya dawa ni kama vile dawa za magonjwa ya akili, tiba ya magonjwa ya saratani, dawa za sonona, dawa za shinikizo la damu na dawa za aleji.

Hivyo ni kawaida kwa mwanamke anayetumia dawa hizi kukosa hedhi kwa kipindi chote cha tiba.  Lakini pia sababu za aina ya maisha pia zinachangia kukosa hedhi.  Mathalani uzito uliopungua kupita kiasi.
Share:

No comments:

Post a Comment