Mwanadamu anakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile za
kiuchumi, kiafya na kijamii. Changamoto zote
hizo huongezeka pindi mwanadamu anapofikia umri wa utu uzima, kwa maana ya
kubebeshwa majukumu ya kimaisha, kama vile kusaidia wanafamilia, wanaukoo na
jamii kiujumla.
Hata hivyo, changamoto kubwa za kiafya zinazomkabili
mwanadamu huyu, karibu kote ulimwenguni ni ugonjwa wa mkazo, ambao umezoeleka
kwa wengi kama ‘stress’ ambazo zinaweza kumfanya mtu kupatwa na shinikizo la
damu.
Baadhi ya vitu vinavyosababisha ugonjwa huu wa mkazo kwa
mujibu wa wataalamu wa afya ni hofu au wasiwasi, kuhusiana na jambo lolote
linaloweza kumkumba mwanadamu, hasa ukosefu wa fedha au kutamani utajiri ambao
hajui ataupataje.
Pia, ratiba za shughuli za kiuchumi na huduma zenye mambo
mengi yasiyokuwa na mpangilio huweza kumsababisha ugonjwa huo mwanadamu. Jambo jingine ni ugomvi usiokwisha ndani ya
familia, kukumbana na matukio ya kutisha kama vile ya ugaidi na kadhalika.
Watu wengi ulimwenguni wamezoea kutumia kilevi, kama vile
pombe, tumbaku na vileo vingine ili kukabiliana na maradhi hayo ya mkazo na
kupanda kwa shinikizo la damu.
Hali hiyo, inatokana na wengi wao hao kushindwa hata kula
vizuri, huku baadhi yao wakilazimika kutumia muda mwingi kuangalia matukio katika
televisheni au kutumia vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za
mkononi kwa muda mrefu ili kujisahaulisha na msongo wa mawazo kichwani.
Mkazo na kupanda kwa shinikizo la damu, ni vitu
vinavyoendana katika maisha ya binadamu.
Ndiyo maana ili kudhibiti magonjwa hayo, mhusika hushauriwa kwanza
kudhibiti hali yake ya mkazo. Kituo kimoja
cha matibabu ya akili kilichopo nchini Uingereza, kinaeleza kwamba katika kila
kundi la watu watano ulimwenguni, mtu mmoja hukumbwa na maradhi ya mkazo,
yanayotokana na mazingira ya mahali pake pa kazi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kushindwa kukabiliana na hali
hiyo ya mkazo mwingi, mtu mmoja kati ya watu wanne, hujikuta akilia peke yake
bila kupigwa wala kukasirishwa na yeyote, akiwa kazini kwake.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mwanadamu ameumbwa kwa
njia ya kipekee kabisa, kwa kuwekewa mifumo mbalimbali mwilini inayofanya kazi
mbalimbali usiku na mchana ili tu kumweka vizuri na salama katika maisha yake.
Kwa mfano, mwanadamu amewekewa mfumo wa hisia za dharura,
ambao ni kichocheo kikuu cha mwili pindi mwanadamu huyu anapopatwa na mkazo
mwingi.
Vichocheo hivyo, ndivyo vinavyomfanya binadamu huyo
anapopatwa na hali hiyo aweze kupumua haraka, moyo wake uende mbio na hali
inayochangia kuongezeka kwa shinikizo la damu.
Vichocheo hivyo, ndivyo huongeza chembe za damu na sukari kwenye damu.
Kwa kawaida, mfumo huo wa hisia za dharura unafanya kazi
kubwa ya kumtayarisha mwanadamu kukabiliana na kitu chochote au mtu yeyote
anayemsababishia hali hiyo ya mkazo.
Hata hivyo, baada ya jambo hilo linalosababisha mkazo
kupita, mwili hurudi katika hali yake ya kawaida, ingawa baadhi ya wataalamu
wanaweka wazi kuwa endapo hali ya hisia za dharura inajirudia mara kwa mara,
mtu anaweza akakumbwa na ugonjwa mwingine wa hofu au wasiwasi, ambao kitaalamu
unajulikana kama ‘Anxiety Disorder’.
Kwa hiyo, kwa kila binadamu ni muhimu kujifunza mbinu za
kukabiliana na maradhi hayo ya mkazo na kupanda kwa shinikizo la damu.
Njia 10 kuepuka ‘stress’
Kwa sasa zipo njia kuu rahisi 10 za kukabiliana na hali hiyo:
Mosi, ni kuhakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala usingizi. Kutopata usingizi wa kutosha kunaathiri
hisia, akili, kiwango cha nishati mwilini pamoja na afya kwa ujumla. Wataalamu wa afya wanashauri mtu mzima apate
usingizi wa walau saa nane katika masaa 24 za siku.
Pili, katika kujipangia mipango ya maisha, unashauriwa
kutanguliza mambo muhimu yanayokuwezesha kuishi kwa kula kwa kiasi.
Kwa maneno mengine, binadamu anatakiwa kufikiri jinsi ya
kurahisisha maisha yake, pengine kwa kupunguza gharama za maisha pamoja na
kupunguza muda anaotumia kazini kwake.
Tatu,
jifunze mbinu za kupumzisha mwili. Kutafakari
kwa kina, mazoezi ya kuvuta pumzi na yoga ni njia imara za kuondoa mkazo.
Nne, mtu inampasa kuimarisha mtandao wake wa kijamii. Kujiunga na vikundi mbalimbali kama vile vya
masomo, kutoa misaada kama vile kwa watoto, yatima na wajane au vikundi vya
wajasiriamali.
Mwaka 2008, baadhi ya watafiti raia wa Uingereza waligundua
njia moja ya kubaki imara pindi mtu anapopatwa na mkazo. Katika utafiti wao, wanasema moja ya njia ya
kubaki imara, ni kujitolea kuwasaidia wengine kwa njia fulanifulani.
Tano, mtu inampasa kuelewa vizuri hisia za wengine, kitu
kitakachosaidia kupunguza hasira, na wakati huohuo awe mwepesi kusamehe kwa
kuwa ni jambo jema pia kimaisha.
Utafiti uliofanywa mwaka 2001 nchini Uingereza, ulionyesha
kuwa mtu anapokuwa na kinyongo fulani kwa mtu, humsababishia kupanda kwa
shinikizo la damu pamoja na kuongezeka kwa mapigo ya moyo. Hali hiyo, kwa mujibu wa utafiti huo, inaweza
kuondolewa kwa mtu kuwa mwepesi wa kusamehe haraka.
Sita, kwa gharama yoyote, mtu anatakiwa kujiepusha na ugomvi
wa aina yoyote ile. Kugombana na wengine
kunaweza kumletea au kumsababishia mtu mkazo mwingi. Mtu anapokuchokoza, jitahidi kutulia,
usimwage ugali kwa kuwa yeye kamwaga mboga.
Inashauriwa kujitenga naye kwa kukaa faragha, hivyo kusuruhisha mambo
kwa hekima na busara nyingi.
Saba, jipangie ratiba ya matumizi ya muda kwa kuandaa muda
wa kutatua matatizo ya familia na ya kazini, kwa kutumia mbinu bora za
makubaliano. Aidha, mtu anaweza akatunza
muda wake wa kazi na familia kwa ufanisi, hivyo kupunguza kiwango cha mkazo
kwake.
Nane, inampasa mtu ajitahidi kupunguza hali
zitakazomwongezea mkazo kadri awezavyo, kwa kutoruhusu hali za kuongeza
mkazo. Kwa mfano, kujiepusha kuwaza
mambo mabaya yanayoweza kutokea na kuchota hisia zake.
Tisa, ni kuhakikisha mwili mzima unatunzwa. Baada ya kazi nzito, jitahidi kuukanda mwili
kwa maji ya uvuguvugu, kabla ya kula chakula.
Mazoezi ya kutembea na kusikiliza muziki ni muhimu kwa sababu
unaifurahisha nafsi yako.
Kumi, ni kuondokana na woga wa kuomba msaada kwa jamaa na
marafiki au majirani. Baadhi ya tafiti
zinaonyesha kwamba kuzungumza na marafiki au watu wa familia kuhusu hali
inayokupata, husaidia kuondoa ugonjwa wa mkazo.
Inashauriwa endapo mkazo na hali ya wasiwasi itaendelea, ni muhimu
kutafuta msaada zaidi kwa daktari.
No comments:
Post a Comment