Haina mashaka
yoyote kuwa vyakula vya nafaka vinanoga!
Au wewe unasemaje kuhusu wali mweupe, pilau, biriani? Na bado hapo hujagusia chipsi, chapati,
kitumbua, andazi, bagia na ugali wa sembe.
Sina shaka
yoyote ile kuhusu ubaya wa kubugia kwa wingi vyakula vya nafaka. Tukumbuke kwamba sukari, yule adui namba moja
wa afya, chimbuko lake ni nafaka. Naamini
wengi wetu tunajua kuwa sukari ni miongoni mwa vyakula vikuu vinavyosababisha
mfuro (uvimbe) na hii ni moja ya vyanzo vikuu vya mwili inayosababisha
kisukari.
Kisukari ni nini?
Sukari kinachoingia
katika mzunguko wa damu inatokana na vyakula tunavyokula. Inapokuwepo kwa wingi katika mzunguko huo,
mwili kutoa taarifa kwa kongosho ili kufanya kazi ya ziada kuzalisha kiwango
kikubwa cha kichocheo kinachojulikana kama insulin ili kuondoa sukari kwenye
damu na kuipeleka kwenye seli ili itumike kutengeneza nishati.
Hali hii
ikijirudiarudia mara kwa mara, kongosho huchoka na kuanza kufanya kazi chini ya
kiwango au wakati mwingine vipokezi vya sukari katika seli (receptors)
hushindwa kuendana na kasi ya kuletewa sukari kwa ajili ya matumizi ya seli,
hivyo huishia kuikataa.
Hali hii,
kitaalamu hujulikana kama insulin resistance, au pingamizi dhidi ya insulin kwa
tafsiri isiyo rasmi. Kuna baadhi ya
nyakati, vyote hutokea kwa wakati mmoja, yaani kongosho linafanya kazi chini ya
kiwango na pia mgonjwa anakabiliwa na pingamizi dhidi ya insulin. Hapo mgonjwa husumbuliwa na tatizo la sukari.
Hivi karibuni
imebainika kuwa moja ya sababu kubwa sana zinazosababisha vipokezi vya seli
kushindwa kupokea sukari inayoletwa ni kitu kinachoitwa mfuro
(inflammation). Mfuro ni uvimbe kama
lengelenge hivi. Mfano wa mfuro ni pale
unapojikwaa au kujigonga usoni na mwili ukaumuka na kutengeneza nundu.
Vichocheo vya
kusababisha mfuro kwenye seli viko vingi lakini baadhi ni vyakula tunavyokula
kila siku. Vyakula hivi ni pamoja na
sukari na wanga iliyotokana na nafaka iliyochakatwa kwa kiwango kikubwa.
Chimbuko la
nafaka kusababisha mfuro ni sukari aina ya fructose ambayo ama tayari ipo au
inakuwa ni moja ya mazao wakati nafaka inachakatwa ndani ya miili.
Watafiti wanasema
fructose huchochea seli za mwili kuchoma nishati iliyohifadhiwa kwa kasi ya
kutisha na matokeo yake hukumbwa na matatizo ama mshtuko.
Mshtuko huo
husababisha vina saba (DNA) katika hizi seli kusambaratika. Watafiti hawa wanaongeza kuwa DNA
iliyosambaratika hujiunda katika kemikali zinazojulikana kama purines, ambazo
nazo huishia kujiunda kuwa tindikali ya urea, yaani uric acid.
Tindikali ya
urea husababisha seli za mwili kukumbwa na mfuro ambao huharibu mifupa laini
inayounganisha viungo vya mwili, husababisha mishipa ya damu kukumbwa na
mkakamao wa kutokupanuka wala kusinyaa, kitendo ambacho husababisha matatizo ya
mfumo wa mzunguko wa damu.
Kwa upande
mwingine, glukozi au sukari nyingine inayopatikana kwa wingi kwenye nafaka au
mezani, inaweza kuleta shida kwenye ini.
Inaweza ikasababisha unene uliopitiliza na inaweza kuchochea kisukari
cha ukubwani na saratani. Glukozi pia ni
chanzo kikubwa sana cha mfuro ndani ya mwili!
Kwa mujibu
wa tafiti, uchakataji wa glukozi huzalisha kemikali inayoitwa malonyl-coA
hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa mitochondria kudhibiti chembe chembe
zilizobeba umeme hasi (high energy electrons) zinazotumika wakati wa uzalishaji
wa nishati inayoitwa Adenosine Tri-phosphate (ATP), ambayo ni kwa ajili ya
matumizi ya baadaye mwilini. Mitochondria
inaweza kuelezewa kama ni viwanda vya kuzalisha nishati ndani ya seli. Huu umeme husababisha kuzaliwa kwa kiwango
kikubwa cha chembe zilizobeba umeme chanya zinazoitwa free radicals. Chembe hizi zina uwezo wa kubadilisha umbo na
utendaji kazi wa vinasaba kwenye seli (DNA mutations) na kuharibu vimeng’enya
mbalimbali ndani ya mwili. Tafiti zimebaini
kuwa baadhi yetu, miili huchakata ngano bila madhara ukilinganisha na
wengine. Watu wa aina hii husemekana wana
mifumo ya ujenzi na uvunjifu wa kemikali ambazo zinaendana na vyakula vya wanga
hasa itokanayo na nafaka. Njia pekee ya
kujua kama wewe ni miongoni mwa waliomo katika kundi hili au siyo ni kwa njia
ya kipimo cha kutambua mfumo wa ujenzi na uvunjifu wa kemikali mwilini
(metabolic typing test).
No comments:
Post a Comment