Udhibiti makini
wa sukari katika damu husaidia kuzuia athari hasi za kisukari cha unene
(Diabesity) na kuboresha matokeo ya hali ya ujauzito, lakini inaweza kuwa
vigumu kuidhibiti. Mlo usio na
kabohidrati nyingi zilizosafishwa na shahamu iliyokifu, pamoja na mazoezi
kiasi, vinaweza kuboresha afya ya mama na mtoto, kwa sababu mabadiliko ya namna
hiyo katika mtindo wa maisha husaidia kudhibiti uzito wakati wa mimba. Kwa wanawake wanene kupita kiasi (morbidly
obese) na wanataka kubeba mimba, upasuaji unaweza kusaidia kurekebisha uzito na
kuzuia au kugeuza shambulio la kisukari badala ya lishe na mazoezi. Kwa kufuatilia kwa makini na kufuata mipango
ya afya kwa usahihi, inawezekana kuepusha kisukari cha unene na matatizo yake.
Watu wenye
kisukari hawana budi kudhibiti kwa makini kiwango cha sukari katika damu yao na
wakati mwingi kuhitaji sindano za insulin
hasa katika kisukari namba 1. Baadhi
ya wagonjwa wa kisukari namba 2 huhitaji vidonge vya kushusha kisukari, lakini
tiba ya kudumu ni kwenda kwenye mlo wa mimea wenye matunda, mboga na jamii ya
karanga kwa wingi na wenye kiasi kidogo cha kabohidrati zilizosafishwa na
shahamu iliyokifu. Kubadili mtindo wa
maisha kama vile mazoezi na kupunguza uzito vinaweza kuzuia au kuchelewesha
shambulio na kisukari namba 2.
Shirika la
kisukari la Marekani lilijadili umuhimu wa mlo wa mimea na kuona kwamba: Mlo usio na nyama ni uchaguzi wa kiafya, hata
kama una kisukari. Utafiti unaonesha
kuwa kufuata aina hii ya mlo kunaweza kuzuia na kudhibiti kisukari…..Chakula
cha mimea tupu huwa na nyuzinyuzi nyingi kwa asili, hakina shahamu nyingi
iliyokifu, na hakina lehemu ukilinganisha na chakula cha kawaida cha Wamarekani…..Kiwango
kikubwa cha nyuzinyuzi katika chakula hicho kinaweza kusaidia kula kidogo kwa
wakati……Chakula hiki pia huwa na gharama ndogo.
Nyama, kuku, na samaki kwa kawaida ni vyakula vya gharama kubwa
tunavyokula.
Hatua kama
hizo za kubadili mtindo wa maisha huleta manufaa makubwa na si za gharama
kubwa. Wakati vinahitaji dhamira na
muda, husaidia kudhibiti kiwango cha sukari na kuwa karibu na kile
kinachotakiwa na kuzuia uharibifu wa macho, figo, na mishipa ya damu hasa ile
ya viungo vya chini. Daktari na mtafiti
wa Kiingereza Denis Burkitt alikuwa sahihi aliposema, “Kama watu wanaanguka
katika gema unaweza kuweka gari la wagonjwa katika lile gema au kujenga uzio
juu ya lile gema. Tunaweka magari mengi
mno ya wagonjwa chini ya gema.”
Watu wengi
kimsingi wanasema, “Daktari, niache niishi nipendavyo, nile ninachotaka, na
kuvuta na kunywa ninachotaka, kisha nipatie kidonge cha mwujiza kunifanya
nisiugue.” Lakini kuna njia bora zaidi
kuliko kupuuza kanuni za afya na kutarajia matumaini zaidi ya kuwa mzima. Badala yake, tunaweza kujenga “uzio”
kujilinda sisi na watoto wetu dhidi ya maradhi na vifo vinavyokuja kabla ya
wakati kwa kula mlo wa asili ufaao kwa afya, kufanya mazoezi mara kwa mara,
kupumzika vya kutosha, kunywa maji mengi, kuwa na uhusiano mzuri na watu, na
kuwa na imani kwa Mungu anayetujali kabisa.
Tuna changamoto kubwa na pia tuna fursa kubwa. Kuzuia ni bora kuliko gari la wagonjwa. Si bora kuliko tiba tu bali ni tiba. Kama watu wazima, tuna fursa ya kuwaonesha
watoto wetu mienendo ya kiafya itakayowaepusha na janga linalovuma.
Wakati huohuo, afya zetu zitakuwa bora. Tunahitaji kuwa watu wa kujishughulisha mwili
na kuwahimiza watoto wetu kufanya mazoezi pia.
Inatupasa kuwa wabunifu makini wa uchaguzi wao, tukiwapatia vyakula vya
kiafya kabisa kama kipaumbele katika bajeti zetu. Hii ni hasa kwa akina mama wajawazito, ambao
huongoza uchaguzi wa watoto na afya yao ya baadae, au ukosefu wa afya hiyo.
No comments:
Post a Comment