Friday, June 24, 2016

AFYA KWA WENYE MIAKA 40 AU ZAIDI


Katika swala la lishe, ajenda kuu kwa watu wenye umri wa miaka arobaini au zaidi, ni kuchukua tahadhari ili vyakula na vinywaji vyao visiwe sababu ya kuongeza lehemu mwilini na kutokuwa na uzito au unene kupita kiasi.

Mtu anaweza kudhibiti kuongezeka kwa lehemu mwilini kama atapunguza ulaji wa nyama nyekundu na vyakula na vyakula vya mafuta yanayotokana na wanyama na atapunguza ulaji wake wa vyakula vilivyokaangwa.

Pia, ataongeza ulaji wake wa matunda na mboga za majani, ataongeza ulaji wake wa vyakula vinavyotokana na mimea, ataongeza ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa njia za asili, na vile vya mchemsho na kuchomwa kwa moto.

Mtu ale matunda angalau vikombe viwili na mboga za majani vikombe vitatu kwa siku.  Pia, anywe maji ya kutosha, afanye mazoezi na apate muda wa kutosha wa kulala.

Kitambi au uzito uliopitiliza kwa asilimia kubwa unatokana na tabia ya kula kwa wingi vyakula vya wanga, sukari na vyenye mafuta, kunywa soda au pombe kupita kiasi, kula kiasi kidogo vyakula vyenye nyuzi nyuzi, kukosa muda wa kulala vya kutosha, kutokunywa maji kiasi cha kutosha na kutokufanya mazoezi.
Uzito na unene kupita kiasi ni kichocheo kikubwa cha magonjwa mengi kama vile kisukari, kiharusi na magonjwa ya moyo.
Mtu anapofikia umri wa miaka arobaini mwili unaingia katika mabadiliko makubwa.

Mwili unapoteza stamina kwa sababu viungo kama vile mapafu huzidi kupungua nguvu ya kufanya kazi.

Pia, macho yanapoteza nuru ya kuona, masikio yanapunguza uwezo wake wa kusikia na kinga ya mwili inapungua.
Vilevile, mifupa huanza kudhoofika, misuli huanza kukakamaa na kupoteza wepesi wake katika kujikunja, ngozi inaanza kujikunja, kitambi na unene vinaongezeka.

Maradhi kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani, kiharusi, magonjwa ya moyo, tatizo la kupungua kwa nguvu za kiume na kike huanza kushika kasi.

Zaidi ya hayo, mtu anapofikia miaka hamsini, moyo wake umepiga zaidi ya mara bilioni moja na nusu, mapafu yake yamepumua zaidi ya mara milioni 400.

Ndiyo kusema, viungo hivyo nyeti vimetumika sana.  Kwa hiyo, mtu asizidi kuviumiza kwa tabia mbaya ya maisha kama vile ulaji usiofaa, kunywa pombe kupita kiasi, kuvuta sigara au kutumia tumbaku, kutokunywa maji ya kutosha, kutokufanya mazoezi na kutokulala vya kutosha.

Hivi sasa hapa Tanzania, idadi ya watu wenye vitambi na unene uliopitiliza inaongezeka kwa kasi kubwa sanjari na kuongezeka kwa magonjwa ya presha, moyo, kisukari, kansa ya utumbo na kupoteza nguvu za kiume na zile za kike.

Waathirika wakubwa ni watu wenye miaka arobaini au zaidi, ambao pia, ndio wenye majukumu makubwa katika familia au taifa.
Athari mbaya kiafya inakuwa kubwa kwa watu ambao wakati wa ujana wao hawakuwa wakijali afya zao kama vile kula kupita kiasi, kutokufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho na kukosa muda wa kutosha wa kupumzika.


Kwa upande wa kina mama, kusimama kupata ada yao ya kila mwezi (menopause) kunaongeza changamoto nyingine za kiafya mtu anapofikia miaka arobaini au zaidi.
Share:

No comments:

Post a Comment