Tuesday, July 12, 2016

LINDA NGUVU ZA KIUME KWA KUFANYA HAYA


Mambo muhimu kufanya ili kuzuia usipate ugumba ni pamoja kuepuka matumizi ya tumbaku na uvutaji sigara, ulevi wa pombe uliopindukia na utumiaji wa dawa za kulevya ikiwamo mirungi na kokeine.  Vilevile hivi ni sumu mwilini kwani vinachangia kuharibu utengenezwaji wa mbegu za kiume na hivyo kuzalishwa mbegu chache, vilevile vitu hivi vinapunguza hamu ya tendo la ndoa kutokana na athari katika mfumo wa fahamu.

Tumia kinga kujikinga na magonjwa yatokanayo na ngono zembe.  Magonjwa kama kaswende, kisonono na pangusa ni hatari kwani uwapo wake kunaharibu maeneo ya uzazi ikiwamo mrija wa kusafirisha mbegu za kiume, kokwa na tezi za kiume.

Epuka kufanya kazi au kukaa katika mazingira yenye joto kali, madereva wa masafa marefu wapo katika hatari ya kupata tatizo hili kutokana na injini za magari hayo kupasha moto eneo analo kalia.

Vilevile wafanyakazi wa viwanda vya kuoka mikate nao wanaweza wakapata tatizo la kupata ugumba kutokana na kukumbana na joto kali.


Wafanyakazi wanaofanya kazi viwanda vya madawa ya kilimo, vinu vya mionzi au madini yanayotoa mionzi, viwanda vya rangi za majumbani wanapaswa kuvaa vifaa vya kuwakinga au kutofanya kazi hizo kwa muda mrefu.  Mambo hayo yote yanasababisha kutengeneza mbegu chache zisizo imara hivyo kuwa chanzo cha ugumba.  Ni vizuri wanaofanya kazi katika viwanda hivyo kutambua matatizo haya na kuchukua tahadhari mapema.

Vaa nguo za ndani zisizohifadhi joto na kubana sana ili kuwezesha eneo la uzazi kupata joto kwa wastani na kuepusha mishipa inayopeleka damu eneo hilo kubanwa.  Epuka dawa za steroids za kunenepesha misuli (wabeba vitu vizito vya mazoezi) na matumizi holela ya dawa za kutibu maradhi mengine sababu zipo baadhi ya dawa ndicho chanzo cha kutengenezwa kwa mbegu dhaifu na chache au kusababisha kiwango chake kuwa chini.

Vizuri kwa wazazi kuwaeleza watoto wao ambao waliwahi kufanyiwa upasuaji wa kokwa za kiume zilizokwama baada ya kuzaliwa na maumbile yasiyotimilifu.  Ni muhimu kwa daktari kujua historia hii inampa usahihi wa kumtibu mwenye tatizo la ugumba.  Ni vema kuwajulisha watoa huduma kuchunguza kama mtoto maumbile yake ya uzazi yako kawaida.  Wanamichezo wanatakiwa kujikinga na vifaa maalumu au kupewa mbinu za kujilinda ili wasiweze kujijeruhi maeneo ya uzazi wakati wa kucheza michezo yao.

Pale mtu anapojeruhiwa maeneo ya uzazi katika hatua za awali kunatokea mwitiko hasi wa kinga ya mwili ambao baadaye kinga huweza kuziua mbegu za kiume maisha yako yote hivyo kusababisha ugumba.  Kawaida kinga ya mwili huwa haizitambui mbegu za kiume kama ni sehemu mojawapo ya mwili, ukijeruhiwa eneo la uzazi na ikatokea mbegu zikapita katika mzunguko wa damu huweza kusisimsha kinga ya mwili kutengeneza askari wa kuziharibu mbegu hizo ikidhani ni adui.

Epuka mifarakano ya kimaisha, shinikizo la kiakili na sonona (depression) mambo kama haya yanaweza kukunyima utulivu wa kimwili na kiakili.

Mwili wenye afya bora ndio pia wenye uwezo wa kutengeneza imara na kiasi kikubwa.

Ni muhimu kula lishe ambayo imesheheni makundi yote ya chakula huku ukidhibiti kula vyakula vinavyoongeza uzito wa mwili na kunenepesha.


Ulaji wa mboga, matunda na vyakula vya protini ni muhimu.  Vitamin E na C ni mojawapo ya kirutubisho muhimu katika uzalishwaji wa mbegu bora za kiume.  Vema pia kufanya mazoezi mepesi na unapokuwa na tatizo lolote la kiafya nenda hospitali.
Share:

No comments:

Post a Comment